WABUNGE WANG'ANG'ANIA WENZAO WALIOKULA RUSHWA WAADHIBIWE...

Presha ya kutaka wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa waadhibiwe, limeendelea bungeni jana kwa baadhi ya wabunge kusisitiza umuhimu wa wabunge hao kutajwa na ikiwezekana wafukuzwe bungeni.
Mbali na kutajwa na kufukuzwa bungeni, wabunge pia walitaka kamati zingine zinazotuhumiwa kwa rushwa zivunjwe ikiwamo ya Hesabu za Mashirika ya Umma na ya Hesabu za Serikali za Mitaa.
Kutokana na nguvu za kampuni zinazodaiwa kuwahonga wabunge hao, wabunge pia wamesisitiza umuhimu wa miondombinu ya Shirika la Umeme (Tanesco), ilindwe na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini walindwe.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Uongozi ya Bunge, jana ilikutana kujadili taratibu zitakazo fuatwa katika kushughulikia suala la kugongwa kwa wabunge na kampuni za mafuta ili kuhujumu Tanesco na uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini.
Wabunge hao walianza kushinikiza hatua dhidi ya watuhumiwa hao kuchukuliwa mara baada ya maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu makadirio ya bajeti ya Wizara wa Afya na Ustawi wa Jamii kusomwa na Msemaji wa kambi hiyo katika wizara hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Conchesta Rwamlaza (Chadema).
Kabla ya hapo wabunge kadhaa walisimama kuomba mwongozo wa Spika ambapo walipopewa nafasi, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM), kutokana na tuhuma hizo, wakipita mitaani wananchi wanawanyanyasa na kuwadhalilisha kutokana na kikundi cha watu wachache.
Mbunge huyo alisema ili kuepuka kunyanyaswa kutokana na kikundi kidogo cha wabunge, ni vyema wabunge hao watajwe ili wajulikane na ikiwezekana wafukuzwe bungeni.
Naye Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), alisema kutokana na tuhuma hizo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alivunja Kamati ya Nishati na Madini na kuongeza kuwa zipo kamati zingine sita zina tuhuma hizo kwa nini zisivunjwe.
Katika hoja hiyo, Nassari alitaja kamati mbili, Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa inayoongozwa na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP).
Nassari alishauri baada ya kuvunjwa kwa kamati hizo, wajumbe wake wapelekwe katika kamati zingine za Bunge ambazo hazisimamii mambo yenye mikataba alizoziita zinazodharauliwa na kutoa mfano wa Kamati ya Huduma za Jamii na Kamati ya Sheria Ndogo.
Kwa mujibu wa maelezo ya Nassari, wabunge wengi wamekuwa wakikimbilia kamati hizo zinazohusika na mikataba na kukimbia kamati zingine zinazodharaulika. Alitaka wabunge wanaopinga rushwa kwa dhati, ndio wapelekwe katika kamati hizo zilizovunjwa za mikataba.
Naye Mbunge wa Lindi, Salum Barwany (CUF), alisisitiza kuwa Watanzania wanataka kujua ni kina nani.
Kutokana na hoja hizo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai aliwataka wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Uongozi kwenda katika mkutano na Spika Makinda ili kujadili utaratibu huo na kushauri Bunge.
Akizungumzia hoja ya kulinda miundombinu ya Tanesco, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), kwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aliaminisha Watanzania kuwa hakutatokea mgawo, amepata taarifa kuwa kuna mpango wa kumuangusha waziri huyo, ili mgao utokee.
Kwa mujibu wa Lugola, baada ya Waziri Muhongo kusigina mirija ya rushwa wizarani na Tanesco, wahujumu hao walitaka kulitumia Bunge na baada ya kushindwa, wameandaa mpango wa kuharibu miundombinu ya Gridi ya Taifa.
Naye Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema mafisadi sasa wanapigana vita ndani na nje ya Bunge na kuomba Serikali itoe agizo miundombinu ya Tanesco, ikiwemo vyanzo vya umeme vilindwe na JWTZ.
Alitaka Waziri Muhongo na naibu mawziri wa Nishati na Madini, George Simbachaene na Steven Maselle, wapewe ulinzi wa uhakika ili kesho na keshokutwa Watanzania wasilie.
Alisema ushahidi wa mazingira kwamba mafisadi wanapigana kujilinda upon a ishara ni habari za baadhi ya vyombo vya habari kwamba mgawo wa umeme utakuwepe Watanzania wapende wasipende.
Kamati ya Uongozi wa Bunge iliyokaa mchana, ilipitia hoja mbalimbali za wabunge ikiwemo ya mgomo wa walimu na tuhumza rushwa na kutoa ushauri kwa Spika.
Kuhusu hoja ya Mbunge wa Chwaka, kuomba Bunge lijadili mgomo wa walimu, Naibu Spika Ndugai alisema Kamati ya Uongozi ilijadili na kushauri suala hilo lisijadiliwe kwa kuwa mahakamani.
Kuhusu hoja ya Nassari, kutaka kamati zingine Bunge zinazotuhumiwa kwa rushwa zivunjwe, na hoja ya Barwany kutaka wabunge watuhumiwa wa rushwa watajwe, Ndugai alisema Kamati ya Uongozi ilirejea katika uamuzi wa Spika Makinda alioutoa Jumamosi iliyopita.
Katika uamuzi huo, Spika alipeleka hoja hiyo katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa jili ya uchunguzi ambao alisema ukimalizika majina yatabainishwa na kutangazwa.
Ndugai alisema Kamati hiyo inayofanya kazi ya uchunguzi itawaita wabunge kwenda kuisadia na kwamba watakaoitwa sio watuhumiwa bali wanasaidia kamati ili kazi hiyo ianze mara moja.
Hata hivyo, Ndugai alisema Spika ataangalia suala la baadhi ya wajumbe wenye mgongano wa kimaslahi, ili wasishiriki katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, ambaye yupo katika Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa kwa tuhuma za rushwa, lakini pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Ndugai alisema mbali na kazi ya uchunguzi inayofanywa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Serikali kwa upande wake kupitia Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), imeanza kuchunguza na tayari baadhi ya wabunge wameanza kuitwa.
Kuhusu ulinzi wa mitambo ya Tanesco na uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini, Ndugai alimshukuru Lugola kwa kulitonya Bunge na ameitaka Serikali kuchukua hatua za kiulinzi na kiusalama na ikiona inafaa, itoe taarifa kwa Bunge.
Kuhusu hoja ya Rage, kwamba kiongozi mmoja wa Bunge amewataja wabunge wa CCM tu na kuwahusisha na rushwa na kuacha wa Chadema, Ndugai aliwashauri wabunge kuwa na utaratibu katika kuzungumzia tuhuma hizo za rushwa.
Alisema atakayeamua kutaja majina, azungumze kwa haki na kuhadharisha kuwa wakigeuza suala hilo kuwa la chama cha siasa, wajue hakuna chama chenye sera ya rushwa.
Aliwataka wabunge wasiwataje majina wenzao kwa ajili ya kukomoa chama cha mtu bali kwa kukemea tabia ya mtu ambayo haikubaliki na jamii.
Kwa upande wake, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imewataja wabunge saba inaodai wana mgongano wa kimaslahi hivyo hawawezi kukwepa tuhuma zinazoelekezwa kwa wabunge kuhusu ufisadi Tanesco.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lisu, alisema kutokana na mazingira hayo kwa namna moja au nyingine wabunge hao huwezi ukawatenganisha na tuhuma za ukosefu wa maadili zinazoelekezwa kwa wabunge hivi sasa.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, aliwataja kuwa ni wabunge wote kutoka CCM wakiwamo wawili wa Viti Maalumu. Kwa kuwa gazeti hili limeshindwa kuwapata wabunge hao kuzungumzia tuhuma hizo, haiwezi kwa sasa kutaja majina yao.
"Wabunge hawa wote ambao walikuwepo kwenye Kamati ya Nishati na Madini wamejihusisha kwenye mgongano wa kimaslahi, hivyo hawezi kukwepa kuwepo kwenye tuhuma hizi za ukosefu wa maadili. Tuna ushahidi nao," alidai Lissu na kusisitiza kuwa Sheria na Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995 inakataza mgongano wa maslahi kwa viongozi wa umma.
Mnadhimu huyo alidai Kambi ya Upinzani imejiridhisha kuwa wabunge wake watatu waliokuwa kwenye Kamati ya Nishati na Madini hawakushiriki kwa namna yoyote katika uvunjifu wa maadili na kuwa kama kuna mtu ana ushahidi tofauti na wao wawapatie na wataufanyia kazi.
Aliwataja wabunge hao kuwa ni Mbunge wa Viti Maalumu, Mwanamrisho Abama, Mbunge wa Mbozi Magharibi David Silinde na Mbunge wa Ubungo John Mnyika, ambao alisisitiza ni wasafi.

No comments: