UFISADI WA MKURUGENZI MKUU WA TANESCO ALIYESIMAMISHWA HUU HAPA...


Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco aliyesimamishwa, Mhandisi William Mhando.
Uozo zaidi wa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Umeme (Tanesco) aliyesimamishwa, William Mhando umeibuliwa jana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Akizungumza jana wakati wa kujibu hoja za wabunge kuhusu makadirio ya bajeti ya wizara hiyo, Profesa Muhongo alisema uozo wa Mhando, si tu kuipa kampuni ya mkewe zabuni ya ugavi wa vifaa vya ofisi vya Tanesco kwa gharama ya Sh milioni 884, bali alifanya madudu zaidi.
Alisema Mtendaji huyo wakati akiisimamia Tanesco, shirika hilo lilikuwa likinunua nguzo kutoka Iringa na kuzisafirisha kwenda Mombasa nchi jirani ya Kenya na kisha kuzirudisha nchini na kutoa maelezo kuwa zimenunuliwa kutoka Afrika Kusini.
Profesa Muhongo aliyekuwa akizungumza kwa kujiamini huku akiwaambia wabunge kuwa anao ushahidi wa kutosha, alisema Tanesco pia chini ya Mhando, iliagiza vipuri nje ya nchi na kulipa pauni za Uingereza 50,000, sawa na zaidi ya Sh milioni 120, lakini wakapokea kasha la misumari badala ya vipuri.
Alisema kutokana na utendaji usio wa uwajibikaji wa Mhando, waliona kuwa umuhimu wa kuchukua hatua za haraka ambapo Bodi ya Tanesco, iliitisha kikao cha dharura na kumsimamisha kazi.
Tuhuma zingine za Mhando zinazochunguzwa kwa mujibu wa Profesa Muhongo ni pamoja na kukumbatia wafanyabiashara na kushindwa kutenganisha maslahi binafsi na ya umma.
Mbali na hayo, Profesa Muhongo ambaye alisema hata Bodi ya Tanesco nayo itavunjwa kutokana na uozo ulioko huko, alisema pia waligundua kuwa baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, walikuwa wanafanya biashara na Tanesco.
Kwa mujibu wa Profesa Muhongo, mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo (hakumtaja, ingawa jina tunalo) aliingia mkataba wa kuiuzia Tanesco matairi ya magari.
Alisema hata baada ya kupata mkataba, mbunge huyo ambaye hakumtaja jina, aliiuzia Tanesco matairi ya kiwango cha chini na akapandisha bei ya kuuzia ikawa kubwa kuliko iliyokuweko katika mkataba.
"Nawaomba wabunge waache kufanya biashara na Tanesco ili waisimamie kwa uhuru, vinginevyo watajiweka katika mazingira magumu ya kimaslahi," alisema.
Kuhusu kuundwa tume ya uchunguzi, Profesa Muhongo alisema hakuna haja ya tume au kamati maalumu kwa kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amepewa kazi hiyo.
Akina Mobutu bungeni
Kuhusu mpango uliosukwa na baadhi ya wabunge wanaodaiwa kuhongwa ili kumwajibisha yeye na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, Profesa Muhongo alianza kwa kuwagawa wabunge katika makundi ya viongozi wa zamani wa Afrika.
"Hapa kuna makundi mawili, moja la watoto wa Mwalimu Julius Nyerere, Edward Sokoine na Rashidi Kawawa na kundi la Mobutu Seseko, Sani Abacha na Bokasa," alisema Muhongo.
Kwa mujibu wa Profesa Muhongo, wabunge waliokuwa wakitetea Tanesco na Mhando ambao kawafananisha na akina Mobutu, walikuwa wakitetea upuuzi na kuhoji wanatetea vipi shirika ambalo tangu lianzishwe mwaka 1930 hadi leo asilimia 20 tu ya Watanzania ndio wana umeme.
Alisema yeye na Maswi, walijiandaa na hoja ya kuwajibishwa kwa kukiuka sheria kama ingefikishwa bungeni na wabunge hao na kuna barua moja kutoka kwa Mfilisi wa Kampuni ya IPTL, Mamlaka ya Ufilisi, Vizazi na Vifo (RITA) ambayo ndiyo ingewaokoa.
"Pamoja na kwamba mimi si mwanasheria, kwa kusoma soma magazeti na vitabu nilifanikiwa kuwa mwanasheria pori, tulikuwa na barua moja ilikuwa kama nondo ya mwisho ya kujitetea mimi na Maswi kama suala hilo lingefikishwa bungeni," alisema.
Alisema barua hiyo iliweka wazi kuwa mnunuzi wa mafuta ya IPTL, ni Wizara na kufafanua kuwa hawakuingilia utaratibu wa Tanesco wa zabuni, wala kuikataza isinunue mafuta kutoka katika kampuni ilizoona zinafaa.
Alifafanua kuwa Tanesco haikuwa na fedha za kununua mafuta na yeye na Maswi kwa kutoa fedha za wizara walikuwa huru kuchagua mahali pa kununua ambako ni Kampuni ya Puma Energy ambayo Serikali ina hisa asilimia 50 na ilikuwa inauza kwa bei nafuu.
Mbali na kuuza kwa bei nafuu, alibainisha kuwa hata moja ya kampuni ambazo zilishinda zabuni ya Tanesco, kuiuzia IPTL mafuta kwa Sh 1,800 kwa lita, ilikuwa inanunua mafuta hayo Puma Energy na kuuzia IPTL kwa bei ya juu.
Aliwashukuru wabunge kwa kumpa ushirikiano na kuongeza kuwa anataka baada ya muda Serikali iwe inachukua gawiwo kutoka Tanesco na kuacha kutafuta fedha za bajeti kila siku katika bia.
Wizi Tanesco
Profesa Muhongo alisema Tanesco kuna wizi mkubwa wa umeme kupitia mita za Luku zisizosajiliwa na shirika hilo.
Aliwataja wateja watano wakubwa waliokamatwa na kufikishwa Polisi kwa wizi wa umeme kuwa ni pamoja na shule za St. Mary’s International School zinazodaiwa kuiba umeme wa Sh milioni 10.5. Mtandao wa shule za St. Mary’s unamilikiwa na Mchungaji Dk Gertrude Rwakatare ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu.
Wengine ni Benki ya Access iliyopo Matumbi Tabata Sh milioni 13.5, duka la Shree lililoko mtaa wa Aggrey, Kariakoo Sh milioni 8 na Hoteli ya Akubu ya Kariakoo pia Sh milioni 25.3.

No comments: