BABU WA MIAKA 95 ATAKA MTOTO KWA BIBI WA MIAKA 81...

Babu aliyeoa mwaka jana akiwa na umri wa miaka 94, Mathias Kisokota, mkazi wa Kitongoji cha Isunta, Namanyere wilayani Nkasi ameibuka na kudai kuwa mwaka mmoja wa ndoa yake na mkewe Uria Mwimanzi (81) umekuwa wa furaha mno, isipokuwa kwa sasa anaomba miujiza ili kuzaa na mkewe huyo.
Anasema kuwa, ingawa katika hali ya kawaida mkewe ameshapitisha umri wa kuzaa, anaamini Mungu anaweza kumfanyia miujiza na kumpatia mtoto kama baraka ya ndoa yao ya uzeeni.
Wanandoa hao ambao waliacha gumzo baada ya kufunga pingu za maisha katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Anthony alasiri ya Juni 18, mwaka jana mjini Namanyere, Nkasi, kabla ya kuoana waliishi pamoja na kubahatika kupata watoto kadhaa, akiwemo kitinda mimba wao, Agnes mwenye umri wa miaka 31. Mtoto mkubwa wa Kisokota aitwaye Adriano ana umri wa miaka 69.
Akizungumza nyumbani kwake Isunta, Kisokota alisema ingawa dhamira ya awali ilikuwa kuingia katika ndoa kwa lengo la kumpendeza Mungu, sasa anadhani mtoto anaweza kuongeza furaha katoka ndoa yao iliyobarikiwa.
"Kweli tuna umri mkubwa, lakini nguvu bado ninazo … ndio maana natamani sana kama tungebahatika kupata mtoto katika ndoa yetu hii," alisema mzee huyo ambaye bado anaonekana mwenye siha njema.
Wanandoa hao ambao kabla ya kuishi `kinyumba’ kila mmoja alibahatika kuwa na watoto, kwa pamoja wana wajukuu 30 na vitukuu 40, wengi wao wakiwa wanaishi nchi jirani ya Zambia ambako wanandoa hao walikutana na kuanza mahusiano yao ya kimapenzi.
Mke wa Kisokota, akionekana kuchoka kiafya kwa kile alichokieleza mwenyewe kusumbuliwa na magonjwa ya uzeeni, anasema kama miujiza itatokea, hana tatizo la kumzalia mumewe.
Hata hivyo anaongeza kuwa, katika siku za hivi karibuni amekuwa akishindwa kwenda kanisani akisema anasumbuliwa na tatizo la mapafu kujaa maji, hivyo kufanya miguu yake ivimbe na kushindwa kutembea.
Lakini ukiondoa tatizo hilo linalokuja na kuondoka, wanandoa hao wameelezwa kuwa ni wenye furaha katika ndoa yao.
Kwa upande wa waumini wa Kanisa analosali Mzee Kisokota, wanamwelezea mzee huyo kuwa ni mcha Mungu kwani hakosi ibada ya Misa Takatifu kila Jumapili ambapo ana mazoea ya kusali Misa ya Kwanza.
"Kanisani huwa kivutio cha kipekee hasa pale unapofika muda wa kutakiana amani ambapo huinuka kitini na kumpa mkono kila muumini aliyehudhuria misa hiyo," anasema mmoja wa wajukuu wa Kisokota, Lucas Ignatus (20).
Kwa mujibu wa mjukuu wake huyo babu yake hawezi kula hata pipi au kitu chochote bila kupiga ishara ya msalaba ikiwa ni ishara ya kubariki chakula pia anasali sala rozali takatifu hata baadaye husahau kula .
"Kwa kweli babu tunampenda wote kwanza ni mcheshi lakini pia ni mcha Mungu anasali sana hivi sasa anaomba ashuhudie nafunga ndoa kanisani kabla hajakufa, " alisema mjukuu huyo.
Mjukuu huyo na majirani wamemmwagia sifa babu huyo kuwa ni msafi kupindukia kwamba kwake uchafu ni adui yake mkubwa hata chakula anachokula inadaiwa lazima ahakikishiwe kuwa kimeandaliwa katika mazingira ya usafi .
Mabinti wa babu huyo, Maria na Agnes ambao wanaishi na wazazi wao, wanasema bado wana kumbukumbu nzuri za ndoa ya kihistoria ya wazazi wao, wakisema mpaka sasa bado kuna wanaoizungumzia ndoa hiyo.
Maria, akielezea anasema wazazi wake waliamua kufunga pingu hizo za maisha ili kuwa mwili mmoja.
Wakati baba ni Mkatoliki, mkewe ni muumini wa madhehebu ya Moravian na kwamba kwa sasa, baada ya kuwa wameoana rasmi, wanapata huduma zote za kiroho ikiwemo kupokea Mwili wa Bwana tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma.
Mjomba wa wazee hao ambaye ndiye msemaji wa familia hiyo, Filbert Lambert alisema wazee hao pamoja na kwamba wameanza kupoteza baadhi ya kumbukumbu muhimu katika akili zao, lakini walisisitiza kwamba sasa wanaufaidi uamuzi wao wa kufunga pingu za maisha kanisani kwani sasa wanapata huduma zote muhimu za kiroho kama ilivyo kwa Wakristo wengine hususani Wakatoliki.
Pia vijana kadhaa wa madhehebu mbalimbali ya dini mjini Namanyere waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi wamekiri kuwa wanandoa hao wamewapatia changamoto ya wokovu, kwani wameweza kubadilika kitabia na kutenda matendo mema na ya kupendeza.

1 comment:

homework help websites said...

I like your style: brief and informative. Good job!