MWENYEKITI UVCCM AUAWA KWA KUPIGWA MAWE...


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Linus Sinzumwa
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kata ya Ndago wilayani Iramba katika Mkoa wa Singida, Yohana Mpinga (30), ameuawa kwa kupigwa kwa mawe katika vurugu zilizotokea katika mkutano wa hadhara wa Chadema, uliokuwa ukihutubiwa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Mkutano huo ulikuwa umeandaliwa na Chadema na kufanyika katika Kijiji cha Ndago katika Jimbo la Iramba Magharibi.
Mbali na Mnyika, viongozi wengine wa Chadema waliokuwapo ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Dk Kitila Mkumbo na Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Mwita Waitara.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Linus Sinzumwa, alisema katika fujo hizo zilizotokea juzi, Mpinga alikufa baada ya kutokea fujo na kurushiana mawe kati ya wanachama wa Chadema na CCM.
Katika mkutano huo kwa mujibu wa madai ya Kamanda Sinzumwa, viongozi wa Chadema walipokuwa wakihutubia walianza kumkashifu Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba, hali iliyosababisha wanachama wa CCM kushindwa kuvumilia hali hiyo na kutokea fujo.
Sinzumwa alidai katika fujo hizo Mpinga alipigwa kwa mawe na kupoteza maisha katika nyumba ya Mwalimu Shume Manase alipokimbilia kuhami maisha yake.
Kutokana na mauaji hayo, watu 18 wanashikiliwa na Polisi kwa ajili ya mahojiano na baada ya upelelezi kukamilika watu hao watafikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma zinazowakabili.
Juzi Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Iramba ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Yahaya Nawanda, alikiri kutokea kwa mauaji hayo.
Hata hivyo, Chadema wamedai hawahusiki na fujo hizo na kudai kushangazwa kusikia habari za kuhusishwa na fujo hizo wakati uchunguzi haujafanyika ili kuwabaini waliohusika na fujo hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwita alidai mbali na mkutano huo kuwa na baraka za Polisi, lakini pia walikuwa na taarifa juu ya mpango wa kuvurugwa mkutano huo.
Alidai waliwatahadharisha askari waliokuwapo kwenye eneo hilo kuwa kuna vijana ambao walikuwa wameandaliwa kufanya fujo ili kuhakikisha kuwa mkutano huo haufanyiki.
Kwa mujibu wa madai ya Mwita, taarifa hizo zilieleza kuwa kuna kikundi cha vijana kilichokuwa kimeandaliwa na kununuliwa pombe pamoja na kukodiwa gari ili kiharibu mkutano huo kwa kuhakikisha haufanyiki.
Alidai pamoja kutoa taarifa hizo, hakuna hatua yoyote ya makusudi iliyochukuliwa na Polisi waliokuwapo karibu na eneo la mkutano, hali iliyosababisha fujo kutokea mara tatu kabla ya mkutano huo kuendelea na kukamilika salama na wao kuondoka katika eneo hilo.
“Lakini kutokana na vurugu zilizokuwa zikisababishwa na kikundi cha vijana ambao tayari walishatolewa taarifa yao kwenye mkutano huo mbele ya Polisi, askari waliokuwapo hawakuthubutu kuchukua hatua kwa vijana wale,” alidai Mwita.
Alidai wakati wakiendelea na mkutano huo na baada ya kutoa taarifa kwa OCD na RPC, askari waliokuwa tayari kuzuia fujo walifika, lakini tayari fujo zilishatulia na mkutano uliendelea kama kawaida.
Kutokana na fujo hizo ambazo Mwita alidai zilitokea mara tatu, waliamua kufungua jalada Polisi lenye namba NDG/RB/190/2012 na katika jalada hilo walitaja majina ya watu waliokuwa wakifanya fujo mbele ya mkutano huo kwa lengo la kufanya mkutano huo usifanyike.
Aliwataja watu aliodai waliohusishwa na fujo hizo na walionaswa na kamera zilizokuwa zikitumiwa kuchukua kumbukumbu ya mkutano huo kuwa ni Daniel Sima, Tito Nitwa, Bakili Ayubu, Yohana Makala Mpande, Ernest Kadege, Abel John, Athumani Ntimbu, Martin Manase, James Ernest, Simon Makacha, Anthon John na Frank Yesaya.
“Kwa hakika askari wa Ndago waliokuwepo mkutanoni mbali ya kutochukua hatua yoyote, fujo za sisi kupondwa mawe zilizidi, askari wote walikimbia akabaki OCS pekee ambaye naye alionekana dhahiri kutochukua hatua stahili,” alidai Mwita.
Alisema mpaka wanaondoka katike eneo la mkutano hakukuwa na taarifa yoyote juu ya fujo ilizosababisha mtu kupoteza maisha na waliendelea na mkutano mwingine katika Kijiji cha Kinampanda na waliporudi hotelini walipofikia jioni mjini Singida walianza kusikia taarifa zinazoeleza kuwa kuna mtu au watu wamepoteza maisha katika mkutano wao wa  kwanza.
Mwita alidai Chadema inalaani taarifa zilizosambazwa kuwa chama hicho kinahusika katika kupoteza maisha ya mtu huyo kwani hakikujihusisha kwa aina yoyote katika kufanya fujo na muda wote kilikuwa kikiomba msaada kutoka kwa askari ili kutuliza fujo hizo.
Alisema kutokana na habari zinazosambazwa kwa kuihusisha Chadema, kuwa kinahusika katika kupoteza maisha ya mtu huyo, chama hicho kimebaini kuwepo mbinu chafu ya kuvihusisha vyombo vya Dola katika kuwatisha wananchi ili wasikiunge mkono katika kuleta mabadiliko ya kweli ndani ya jamii.
Alisema tayari chama chake kimeshapokea taarifa kutoka Jeshi la Polisi ya kusitishwa kwa ziara yake ambayo kwa jana ingefanya mikutano miwili katika kijiji cha Shelui na Kiomboi na wanatii amri hiyo.

No comments: