Raia wa Kenya, Joshua Mulundi (21) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kumteka na kutaka kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dk Stephen Ulimboka.
Mulundi alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Agnes Mchome.
Wakili wa Serikali, Ladislaus Komanya alidai kuwa, usiku wa Juni 26 mwaka huu katika eneo la Leaders Club, Mulundi ambaye ni mkazi wa Murang’a nchini Kenya alimteka Dk Ulimboka.
Katika shitaka la pili ilidaiwa kuwa, Juni 26 mwaka huu, akiwa katika eneo la Msitu wa Mwabepande Tegeta jijini Dar es Salaam huku akijua ni kinyume cha sheria Mulundi alijaribu kumuua Dk Ulimboka.
Hakimu Mchome alisema mshitakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo isipokuwa Mahakama Kuu.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo Mulundi alidai kuwa kosa aliloshitakiwa nalo siyo sahihi, lakini Hakimu Mchome alisema kuwa shauri hilo litasikilizwa Mahakama Kuu ambapo atawasilisha malalamiko yake.
Shauri hilo limefunguliwa katika Mahakama hiyo kwa hatua ya upelelezi na baadaye litahamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Mshitakiwa alirudishwa rumande na kesi hiyo itatajwa tena Agosti 5 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment