MGOMO WA MADAKTARI WAELEKEA UKINGONI...

Mgomo wa madaktari sasa unaelekea ukingoni baada ya Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kutangaza rasmi madaktari wake kurejea kazini na kuendelea na kazi.
Pamoja na taasisi hiyo kutangaza kutokuwapo mgomo, gazeti hili jana lilishuhudia wagonjwa wakifika hospitalini hapo kupata matibabu huku madaktari wakiendelea kutoa huduma kama kawaida.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Moi, Balozi Charles Mutalemwa, alisema katika taasisi hiyo hakuna mgomo wa madaktari kwa kuwa madaktari wote 61 wako kazini na wanaendelea na kazi.
"Napenda ifahamike, kuwa tangu mgomo huu wa madaktari uanze Juni 23, katika taasisi hii madaktari wote bingwa 18 walikuwa kazini wakitoa huduma kwa wagonjwa wa ndani na wa dharura," alisema Balozi.
Alikiri kuwa madaktari wengine waligoma na mahudhurio yao yalikuwa yakisuasua hali iliyosababisha katika taasisi hiyo baadhi ya vitengo kama vile kliniki na operesheni za kawaida kufungwa kwa muda kutokana na uchache wa madaktari.
Kwa mujibu wa Balozi Mutalemwa, Menejimenti ya hospitali hiyo baada ya kuona hali hiyo, iliitisha mkutano wa Bodi na kukubaliana kuomba madaktari wa Moi warejee kazini huku madai yao yakiendelea kushughulikiwa na Serikali.
Alisema baada ya ombi hilo, kuanzia juzi madaktari hao walianza kuripoti kama kawaida na hadi jana wote 61 wakiwamo 18 bingwa, walikuwa kazini wakiendelea na huduma.
Alisema mgomo unaoendeshwa na Jumuiya ya Madaktari wa Tanzania uko nje ya uwezo wa taasisi hiyo na walichokubaliana na madaktari wa Moi ni makubaliano baina ya mwajiri na mwajiriwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Profesa Lawrence Museru, alisema pamoja na kwamba madaktari hao wamerejea kazini, bado mwitiko wa wagonjwa si mzuri kutokana na dhana waliyonayo ya mgomo kuendelea.
Alisema katika kitengo cha dharura pekee, taasisi hiyo ilikuwa ikipokea wagonjwa zaidi ya 30 kwa siku lakini tangu juzi madaktari hao waliporejea kazini, wagonjwa katika kitengo hicho wamekuwa hawazidi watano na kutoa mwito wajitokeze kwani huduma zinaendelea.
Hata hivyo, katika upande wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), hali ilikuwa tofauti kidogo kwa kuwa madaktari walikuwa wachache huku idadi ya wagonjwa ikionekana kupungua.
Juzi Msemaji wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha alikiri kuwa huduma katika hospitali hiyo zilikuwa katika kiwango cha kati kutokana na uchache wa wagonjwa hali iliyojidhihirisha wazi jana.

No comments: