ILIVYOPOKELEWA MTAANI KUKATIKA KWA UMEME BUNGENI...

Katika hali iliyowaacha midomo wazi mamilioni ya Watanzania waliokuwa wakifuatilia matangazo ya kikao cha Bunge kupitia kituo cha televisheni cha TBC majira ya jioni, ghafla umeme ukakatika 'mjengoni' humo.
Ilikuwa ni baada ya matukio mawili ya kukumbukwa kwa siku ya jana kuwa yametokea katika kikao ambacho kiliongozwa na Naibu Spika, Mheshimiwa Job Ndugai. Tukio la kwanza ni lile ya kutolewa nje na kupigwa marufuku kuhudhuria vikao vitatu, Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile. La pili ni pale Naibu Spika alipomtolea uvivu Mbunge wa Kawe, Mheshimiwa Halima Mdee kufuatia kuvunja kanuni za Bunge.
Wakati Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Profesa Anna Tibaijuka akijibu maswali ya wabunge kuhusu bajeti ya wizara yake majira kama ya saa moja kasorobo usiku, ndipo umeme ukakatika ghafla.
Kwa takribani dakika kumi hivi Watanzania waliokuwa wakifuatilia matangazo hayo walilazimika kusikiliza sauti pekee bila kuona chochote ndani kufuatia giza kubwa lililokuwa limetanda ndani.
Ndipo katikati ya giza hilo hilo, zikasikika sauti za wabunge mbalimbali ambao walianza kujibizana kwa lugha zilizochukua umaarufu katika siku za karibuni mpaka kufikia vikao hivyo kuitwa 'Kariakoo' zikashika kasi kwa dakika mbili tatu.
Hatimaye baada ya kuonekana kama tatizo hilo ni kubwa, Naibu Spika akasikika akitangaza rasmi kusitisha shughuli za Bunge hadi leo saa tatu asubuhi.
Penye wengi pana mengi, huku mtaani tukio hilo limepokewa kwa mtazamo tofauti kabisa. Jamaa mmoja mara baada ya umeme kukatika akasikika akisema, "Afadhali, Naibu Spika kazidi bwana. Leo kakutana na kiboko yake. Yeye si kajifanya kumtoa Mbunge wetu nje, naye kaamua kumkomesha kaenda kunyofoa nyaya za umeme nje na kuharibu jenereta!" Akioanisha tukio hilo na kutolewa nje kwa Dk. Ndugulile.
Kwa jinsi ulinzi ulivyo imara pale bungeni, mimi siamini kama kweli, ila nadhani ni hitilafu tu imetokea ambayo itafanyiwa kazi. Sijui huko mtaani kwenu mmepokeaje hilo!

No comments: