HOTUBAYA WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI, MHESHIMIWA PROF. ANNA KAJUMULO TIBAIJUKA (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Bunge lako likubali kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa kazi za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika mwaka 2011/12 na malengo ya Wizara katika bajeti ya mwaka 2012/13. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2012/13.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia Waheshimiwa Wabunge kuwa na afya njema na hivyo kuweza kushiriki mkutano huu wa nane wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba nitangulize dua zangu kwa Mwenyezi Mungu kuwa azipokee na kuzilaza pema roho za Waheshimwa Wabunge waliotangulia mbele ya haki tokea mkutano wa Bajeti wa mwaka 2011/12 ulipofanyika.
Mheshimiwa Spika, pili, naomba nitumie fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais; na Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, Waziri Mkuu na Mbunge wa Mpanda Mashariki, kwa uongozi wao mahiri. Nawashukuru kwa ushauri, maelekezo na ushirikiano wanaonipa, ulioniwezesha kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa ya kuongoza sekta hii muhimu katika maendeleo ya nyanja zote za maisha katika Taifa letu. Kwa namna ya pekee namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kubwa aliyoionesha kwangu kwa kuamua niendelee kuongoza Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati wa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri aliyoyafanya mapema mwezi Mei 2012. Napenda kumhakikishia kuwa nitaendelea kujenga timu yenye nguvu ili kwa pamoja tujenge sekta ya ardhi yenye tija kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na taratibu.
Mheshimiwa Spika, nakupongeza kwa umahiri na umakini ambao umeonesha katika kuongoza shughuli za Bunge. Hongera sana, na Mwenyezi Mungu aendelee kukuongoza na kukupa hekima zaidi. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Mbunge wa Kongwa na Naibu Spika wa Bunge letu kwa kazi nzuri katika kuendesha shughuli za Bunge pamoja na wenyeviti wote.
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Waziri wote walioteuliwa na Mheshimiwa Rais katika Baraza la Mawaziri kushika nyadhifa hizo kufuatia mabadiliko aliyoyafanya mwezi Mei 2012: Vilevile, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki na Bunge la Afrika. Ni matumaini yangu kuwa watatuwakilisha vyema kwa maslahi na manufaa ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, napenda nitumie fursa hii kuwashukuru kwa dhati wananchi wa Jimbo la Muleba Kusini kwa kunipa ushirikiano wa karibu katika kutimiza majukumu yangu nikiwa Mbunge wao. Ninawashukuru sana kwa uelewa na ushirikiano, na uongozi madhubuti wa madiwani na wenyeviti wa vijiji kuunda Mifuko ya Maendeleo ya Kata ambayo italeta mapinduzi katika kupunguza umaskini na kutuletea maendeleo endelevu. Pamoja na kuwa na kazi nyingi za kitaifa, wananchi wa Jimbo la Muleba kusini wamekuwa wakinipa ushirikiano mzuri na kujitahidi kukutana nami ninapopata nafasi kufika jimboni kwa kuhudhuria vikao na mikutano katika tarafa zao au kupokea wageni na wataalaam waelekezi ninaowatuma kufika kusukuma maendeleo yetu. Ninawashukuru sana kwa uelewa na ushirikiano na uongozi madhumuti wa madiwani na wenyeviti wa vijiji kuunda Mifuko ya Maendeleo ya Kata, taasisi ambayo italeta mapinduzi katika kupunguza umaskini na kutuletea maendeleo endelevu. Ninawapongeza Madiwani ambao tayari wamesajili taasisi hiyo katika kata za Mubunda, Kyebitembe, Rulanda, Muleba, Bureza, Magata Karutanga, Kimwani, Mazinga, Nyakabango, Nshamba, Biirabo, Kishanda, Buganguzi, Burungura, Buhangaza, Kashasha, Ijumbi na Muleba Mjini. Ninawahimiza wale ambao bado hawajakamilisha zoezi hili wakazane tusonge mbele kwa pamoja. Aidha natuma salamu kwa vijana wanaoshiriki katika mashindano ya kandanda ya Kombe la Anna Tibaijuka Cup. Ninawapongeza wale ambao wameshinda mashindano ya kata na ninaamini mwisho wa mwaka tutakapocheza fainali washindi wataweza kutoa vijana wa Muleba kujiunga na Taifa Stars. Nimefurahi kusikia kwamba na wasichana hawakubaki nyuma wameitikia wito wangu na kushiriki michezo ya riadha inayotangulia mashindano ya mpira. Vijana michezo ni maendeleo. Kwa wenye vipaji, Muleba tusikubali vijana wetu kubaki nyuma kwa kuwa tu tuko mbali na majiji makubwa nchini hususan Dar es Salaam. Kwa kupitia ligi yetu, wenye uwezo wataibuka na kung’ara na kusonga mbele. Mwisho ninatuma salamu kwa mama yangu mzazi Ma Aulelia Kajumulo hapo Muleba. Sala zake za kila siku anapokuwa na nguvu zinasikika maana huku mie ni mzima wa afya.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru kwa dhati viongozi wote wa Chama cha Mapinduzi (CCM), viongozi na watendaji wa Serikali kwa kuniwezesha kutekeleza majukumu ya Wizara yangu. Kwa namna ya kipekee natoa shukurani zangu za dhati kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa James Daudi Lembeli (Mbunge wa Kahama), kwa ushirikiano mkubwa na ushauri wao ambao umeiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi. Natoa shukurani za pekee kwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Goodluck Joseph Ole-Medeye (Mbunge wa Arumeru Magharibi) kwa ushirikiano na umoja tuliojenga kutekeleza majukumu yetu na pia nampongeza kwa Mhe. Rais kuamua aendelee na wadhifa wake huo. Nawashukuru pia Katibu Mkuu Bw. Patrick Rutabanzibwa; Naibu Katibu Mkuu, Bibi Maria Bilia; na watendaji wote wa Wizara na Taasisi za Wizara. Watanzania wengi wanatambua changamoto kubwa zinazoikabili sekta yetu lakini hakuna kinachoshinda umoja, maana ni nguvu ya pekee.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2011/12 NA MALENGO YA MWAKA 2012/13
Ukusanyaji wa Mapato
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara ilikuwa na lengo la kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 23.6 kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato katika sekta ya ardhi. Hadi Juni, 2012 jumla ya Shilingi bilioni 17.1 ambazo ni sawa na asilimia 72.5 ya lengo zilikusanywa.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13 Wizara imeweka lengo la kukusanya Shilingi bilioni 99.8. Maduhuli haya yatakusanywa kwa kutumia mikakati ifuatayo: kuongeza kodi ya ardhi na tozo kama ilivyoagizwa na kamati ya Ardhi; kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu za ardhi; kupanga, kupima na kumilikisha maeneo mapya; kukamilisha upimaji na umilikishaji wa viwanja kwenye maeneo ambayo upimaji wake haujakamilika; kuhamasisha wananchi kulipa kodi ya ardhi; na kuwachukulia hatua za kisheria wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi. Naomba nitumie fursa hii kuhimiza wananchi kulipa kodi ya pango la ardhi na tozo nyingine kwa mujibu wa sheria za nchi ili kuepuka usumbufu wa kushitakiwa mahakamani, kunyang’anywa ardhi na maendelezo juu yake au kulipa faini. Nasisitiza kwamba muda wa kuvumiliana na wa visingizio umekwisha.
Matumizi
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara iliidhinishiwa jumla ya Shilingi bilioni 50.89. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 9.3 sawa na asilimia 18 ya fedha zilizoidhinishwa zilitengwa kwa ajili ya mishahara, Shilingi 19.6 sawa na asilimia 39 zilitengwa kwa ajili ya matumizi mengineyo na Shilingi bilioni 21.9 sawa na asilimia 43 zilitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Hadi Juni, 2012 jumla ya fedha zilizopatikana ni Shilingi bilioni 34.65 sawa na asilimia 68.1 ya fedha zilizoidhinishwa, na jumla ya Shilingi bilioni 34.45 zilitumika. Kiasi kilichotumika ni sawa na asilimia 99.4 ya fedha zilizopatikana. Kati ya fedha zilizotumika Shilingi bilioni 8.96 zilitumika kwa ajili ya mishahara, Shilingi bilioni 19.49 kwa ajili ya matumizi mengineyo, na Shilingi bilioni 6.0 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Fedha za maendeleo zilizopatikana zilikuwa sawa na asilimia 28 tu ya bajeti ya miradi ya maendeleo
UTAWALA WA ARDHI
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria za Ardhi, mamlaka za ugawaji wa ardhi ziko katika ngazi tatu za vijiji; Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji; na Taifa. Majukumu ya mamlaka hizi yameainishwa katika Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999, Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999 na Kanuni za sheria hizo. Kwa mujibu wa Kanuni ya 76 ya Kanuni za Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Halmashauri ya Kijiji ina uwezo wa kugawa ardhi kwa mwanakijiji au mtu yeyote ilimradi awe ni raia wa Tanzania na ardhi iwe na ukubwa usiozidi hekta 21. Halmashauri ya Wilaya, kupitia kamati yake ya kugawa ardhi, ina mamlaka ya kugawa ardhi ya Kijiji yenye ukubwa wa kati ya hekta 21 na 50. Ardhi ya Kijiji yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 50 inagawiwa kwa ridhaa ya Kamishna wa Ardhi. Kwa upande wa ardhi ya kawaida Halmashauri ya Kijiji inaruhusiwa kugawa ardhi yenye ukubwa usiozidi hekta 21. Halmashauri ya Wilaya inaruhusiwa kugawa ardhi yenye ukubwa wa kati ya hekta 21 na hekta 202. Mapendekezo ya kugawa ardhi katika fukwe, visiwa vidogo na kwa ajili ya uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) yanatakiwa yawasilishwe kwenye Kamati ya Taifa ya Kugawa Ardhi ambayo mwenyekiti wake ni Kamishna wa Ardhi. Wajumbe wa Kamati hiyo wanatoka Wizara za Ulinzi, Kilimo, Mifugo na Viwanda, na Tume ya Mipango. Kamati hiyo huteuliwa na Waziri wa Ardhi. Hata hivyo, pamoja na sheria kuonesha bayana majukumu ya mamlaka husika, kumekuwepo tabia ya baadhi ya mamlaka kugawa ardhi inayozidi mamlaka yake. Aidha, baadhi ya mamlaka zikiwemo za vijiji zimekuwa zikitoa ardhi kwa waombaji ambao si raia wa Tanzania, kinyume cha sheria. Tabia hii husababisha migogoro na hasara kwa waliopewa ardhi bila kufuata utaratibu. Kupitia Bunge lako Tukufu naziagiza mamlaka za vijiji na Halmashauri kufuata sheria, kanuni na taratibu za kugawa ardhi ili kuepusha malalamiko na migogoro isiyo ya lazima. Nasisitiza kuwa ardhi kwa ajili ya wawekezaji hutolewa na Kamishna wa Ardhi kwa mamlaka ambayo yako chini ya Rais. Hakuna tena njia nyingine ya kugawa ardhi nje ya utaratibu huu. Ukiwa na ardhi yako ukaamua kumpa mtu mwingine huna budi kuirudisha kwa Kamishna (surrender) ili igawiwe upya kwa mtu mwingine. Makubaliano yanayofanyika kati ya Halmashauri na Wawekezaji au Wamiliki wengine na wawekezaji nje ya utaratibu huu ni batili, sharti yapate baraka za Kamati ya Kugawa Ardhi ya Taifa kabla hatimiliki mpya hazijatolewa.
Utoaji Milki
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara ilikuwa na lengo la kutoa hatimilki 21,000. Hadi kufikia Juni, 2012 Wizara ilitoa hati milki 23,610 sawa na asilimia 112.4 ya lengo. Kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu inatarajia kutayarisha na kutoa hatimiliki 40,000. Natoa wito kwa Halmashauri za wilaya na miji nchini kuhakikisha kuwa zinamilikisha viwanja vyote vilivyopimwa na kuandaa hati ili wananchi waweze kuwa na milki salama.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara yangu iliahidi kufungua Ofisi ya Ardhi ya Kanda ya Magharibi mjini Tabora Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, la Ofisi limepatikana mjini Tabora na ofisi hiyo itaanza kutoa huduma mwaka huu wa fedha.
Utwaaji, Ubatilishaji na Uhamisho wa Milki
Katika mwaka 2011/12, ilani za ubatilisho zilizotumwa ni 792 na jumla ya milki72 zilibatilishwa na kutwaliwa na milki 1,512 zilihamishwa. Kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu itaendelea kutwaa ardhi na kubatilisha milki kwa mujibu wa sheria na inatarajia kushughulikia maombi 1,700 ya uhamisho wa milki. Ili kuhakikisha kuwa ardhi inatumika kwa ufanisi natoa agizo kwa Halmashauri zote nchini kuwasilisha Wizarani taarifa za viwanja na mashamba yaliyotelekezwa au kutumika kinyume na masharti ya milki ili taratibu za kubatilisha milki ziweze kuchukuliwa.
Utekelezaji wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara yangu iliweka lengo la kutoa Vyeti 3,732 vya Ardhi ya Kijiji. Hadi Juni 2012 ilitoa Vyeti vya Ardhi ya Kijiji 1,950. Idadi hii inafanya jumla ya Vyeti vya Ardhi ya Kijiji vilivyotolewa nchini kufikia 9,460 kati ya vijiji 11,817 vilivyosajiliwa nchini. Pia, Wizara iliandaa, kusajili na kutoa Hati za Hakimilki ya Kimila 21,169 kati ya lengo la hati 45,000. Natoa pongezi kwa Halmashauri zote zinazoendelea na utekelezaji wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999 kwa kutenga fedha kwa ajili ya uhakiki na upimaji wa mashamba pamoja na utoaji wa hatimilki za kimila kwa wananchi. Natoa wito kwa Halmashauri za Wilaya zote nchini kuiga mfano huu kwa kutenga fedha kwa ajili ya kupima na kuhakiki mashamba ya wananchi na kuwamilikisha. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge kwa nafasi zao kama wajumbe wa Baraza la Madiwani kuhamasisha wananchi kudai kumilikishwa ardhi yao na kuhimiza Halmashauri za Wilaya zao kutoa huduma za upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi kwa wananchi. Napenda kuwahakikishia ushirikiano kutoka Wizara yangu mtakapohitaji.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13, Wizara yangu itakamilisha utayarishaji na utoaji wa Vyeti vya Ardhi ya Vijiji kwa vijiji 2007 vilivyopimwa. Pia, Wizara yangu kwa kushirikiana na MKURABITA, Halmashauri za Wilaya, na wadau wengine itaendelea kuratibu utayarishaji na utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila 50,000 .
Usajili wa Hati na Nyaraka za Kisheria
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ilipanga kusajili nyaraka za kisheria 60,000 katika mwaka 2011/12. Hadi kufikia mwezi Juni 2012, nyaraka za kisheria 64,632 zilisajiliwa. Kati ya nyaraka zilizosajiliwa, 27,452 ni hatimiliki na 28,990 ni nyaraka nyingine zilizosajiliwa chini ya Sheria ya Usajili wa Ardhi Vilevile, nyaraka 7,280 zilisajiliwa chini ya Sheria ya Usajili wa Nyaraka na nyaraka 910 zilisajiliwa chini ya Sheria ya Usajili wa Rehani ya Mali Zinazohamishika. Kwa mwaka 2012/13, Wizara inakusudia kusajili hatimiliki na nyaraka za kisheria 75,000. Kati ya hatimiliki na nyaraka hizo, 35,000 zinatarajiwa kuwa hatimiliki na 40,000 ni nyaraka nyingine za kisheria.
Uthamini wa Mali
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2011/12 Wizara yangu ililenga kufanya na kuidhinisha taarifa za uthamini wa Jumla wa mali zipatazo 13,000. Hadi Juni 2012 wizara iliidhinisha taarifa za uthamini 11,445 ambazo kati yake taarifa 1,507 ziliandaliwa na Wizara na 9,938 zilipokelewa kutoka kampuni binafsi za uthamini na Halmashauri za Miji na Wilaya. Kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu imelenga kuthamini na kuidhinisha taarifa za uthamini wa mali zipatazo 14,000 kwa madhumuni mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu pia inaandaa na kuidhinisha taarifa za uthamini, hususan uthamini kwa ajili ya ulipaji fidia kwa wananchi wanaoguswa na utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa umma. Katika mwaka wa fedha 2011/12, Wizara imeidhinisha taarifa za uthamini wa mali 11,256 ikilinganishwa na lengo la 9,000 kwenye maeneo ya migodi katika vijiji vya Katoma na Nyamalembo Wilayani Geita, Nyamongo North Mara na Nyalanguru Wilayani Tarime; uwekezaji kwenye eneo la mtambo wa gesi asilia huko Mnazi Bay na njia ya bomba la gesi eneo la Somanga-Kilwa. Pia, uthamini ulifanyika kwenye eneo linalotarajiwa kumilikishwa kwa Kampuni ya Ecoenergy kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari lililoko kijiji cha Makurunge Wilayani Bagamoyo. Vilevile, maeneo ya barabara chini ya TANROADS yalifanyiwa uthamini. Kwa mwaka 2012/13 Wizara imelenga kufanya uthamini wa fidia kwa mali zipatazo 15,000 kutokana na miradi mbalimbali itakayokuwa inatekelezwa nchini ikiwepo mradi wa kuendeleza eneo la Kigamboni na mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Biashara Kurasini, Jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea na jukumu la kujenga Hazina ya Takwimu za Uthamini (Valuation Database) kwa lengo la kuwa na takwimu madhubuti za ukokotoaji wa thamani ya ardhi, majengo, mazao na mimea kwa kiwango cha soko. Katika mwaka 2011/12, Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri iliandaa viwango elekezi vya thamani ya ardhi katika Miji 10 ambayo ni Jiji la Dar es Salaam, Mbeya, Tanga na Arusha; Manispaa ya Morogoro, Iringa, Sumbawanga, Lindi na Bukoba na Halmashauri ya Mji wa Kibaha.Wizara iliendesha mafunzo kwa wathamini katika Kanda za Mashariki (Dar es Salaam), Kaskazini, (Moshi), Ziwa (Mwanza) na Kusini Magharibi (Mbeya).
Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka 2012/13, Wizara yangu itaendelea kuandaa viwango elekezi kwa miji ya mikoa 11 sambamba na uchambuzi wa kina wa takwimu kwenye miji yenye viwango elekezi. kuandaa mfumo wa uthamini wenye uwezo wa kutunza, kuchambua na kutoa taarifa ya takwimu hizo kwa wadau mbalimbali wa huduma za uthamini na kuhuisha viwango hivyo kwa kuzingatia mwenendo wa soko la mali.
Kuanzishwa kwa Hazina ya Ardhi (Land Bank)
Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka 2011/12 Wizara iliahidi kuanzisha chombo kwa ajili ya kusimamia Hazina ya Ardhi na kuanzisha Mfuko wa Fidia ya Ardhi. Kazi hiyo imeanza, na kwa mwaka 2012/13 Wizara inatarajia kukamilisha uanzishaji wa chombo hicho na Mfuko wa Fidia ya Ardhi. Chombo hicho kitasimamia utoaji wa ardhi kwa wawekezaji wa ndani na nje kwa misingi ya kuingia ubia wa kumiliki pamoja hisa kati ya wananchi na wawekezaji hao (land for equity), ambapo hisa zitatolewa kwa uwiano na thamani ya mtaji wa mwekezaji (Invested value method of land valuation). Lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika zaidi na ardhi katika maeneo yao, na kuongeza usalama wa miradi ya wawekezaji (Sustainability of extensive land-based investments). Kiwango cha chini cha hisa za Serikali katika ubia huo kitakuwa asilimia 25, na kati ya hizo mapendekezo ni kwamba angalau asilimia 5 zitagawiwa kwa Halmashauri yenye eneo hilo, asilimia 5 zitauzwa kwa bei ya soko kwa wananchi watakaotaka kushiriki katika miradi husika. Natoa wito kwa Bunge lako Tukufu kuunga mkono utaratibu mpya wa kutoa ardhi kwa wawekezaji kwa msingi wa kugawana hisa utakaofuta taratibu zinazotumiwa na Halmashauri na Vijiji kwa sasa za kupewa gawio lisilozingatia msingi ya kiuchumi, kwa mfano wawekezaji kutoa zawadi ndogondogo kama visima vya maji, madarasa na kadhalika. Taratibu zitakapokamilika tutawasilisha muswada wa sheria ya kuanzisha rasmi chombo hicho.
KUMBUKUMBU ZA ARDHI NA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO
Mheshimiwa Spika, katika Hotuba yangu ya mwaka 2011/12 niliahidi kuendelea na zoezi la kuweka mfumo wa kompyuta kwa ajili ya kukusanya kutunza na kukadiria kodi ya pango la ardhi kwenye Halmashauri kumi, pamoja na kuunganisha Ofisi za Ardhi za Kanda za Kaskazini na Ziwa kwenye mtandao wa kompyuta wa Wizara na kuweka mfumo mmoja wa ki-elektroniki. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba hadi kufikia Juni 2012, Wizara yangu ilikuwa imekamilisha kuweka mfumo ya kompyuta wa Land Rent Management System - LRMS katika Ofisi za Ardhi za Halmashauri kumi na moja (11) za Hanang, Njombe, Makambaku, Same, Hai, Mbeya (W), Muheza, Kilosa, Masasi, Mpanda na Manispaa ya Dodoma na kutoa mafunzo kwa watumiaji wa mfumo huo. Sambamba na hilo mfumo wa kompyuta wa Land Rent Management System wa vituo 17 kati ya 29 iliboreshwa. Vituo hivyo ni pamoja na Jiji la Mbeya, Mwanza, Tanga, Arusha Manispaa za Bukoba, Sumbawanga, Kigoma, Singida, Songea, Moshi, Shinyanga, Mji wa Babati, Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Kilombero, Kahama, Bagamoyo na Kibaha. Aidha, Wizara imesaini mkataba na mtaalam mshauri atakayesanifu na kusimika mfumo unganishi wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi Integrated Land Management Information System - ILMIS. Mtaalam huyo anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo katika kipindi cha miezi 24.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara itaendelea na kazi ya kujenga mfumo wa ILMIS. na kuhuisha mfumo wa kutunza kumbukumbu wa LRMS katika Ofisi za Ardhi za Halmashauri 30. Mpango huu utafanikiwa tu ikiwa Halmashauri zote nchini zitaandaa na kutekeleza mpango endelevu wa kuweka na kutunza kumbukumbu sahihi za mashamba na viwanja vilivyopimwa na kumilikishwa.
MABARAZA YA ARDHI NA NYUMBA YA WILAYA
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2011/2012, Wizara ilikamilisha taratibu za kuunda Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya katika Wilaya tatu (3) za Nzega, Kilosa na Manyoni kama nilivyoahidi na yataanza kutoa huduma katika mwaka huu 2012/13. Vilevile tutaimarisha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya za Kinondoni na Ilala kwa kuyapatia majengo yenye kukidhi mahitaji. Kutokana na kuanzishwa kwa Mabaraza mapya matatu (3), kwa sasa nchi nzima inayo Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya 42. Pia, Wizara yangu inakusudia kukamilisha uundaji wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya 6 za Ngorongoro, Tunduru, Mpanda, Muleba, Karagwe na Kyela.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya iliendelea kushughulikia migogoro 15,754 ya ardhi na nyumba iliyokuwepo mwezi Juni, 2011 na mingine 10,428 iliyopokelewa hadi Juni, 2012. Mwaka 2011/12 mashauri 8,528 yaliamuliwa, na mashauri 17,654 yanaendelea kusikilizwa. Kwa mwaka 2012/13, Wizara itaendelea kuimarisha Mabaraza yaliyopo kiutendaji ili kupunguza mlundikano wa mashauri katika Mabaraza hayo. Pia, itasikiliza na kutolea maamuzi mashauri 17,654 yaliyopo. Pia, nichukue nafasi hii kuhimiza Wenyeviti wa Mabaraza haya kutambua kwamba wananchi wamekuwa wakiilalamikia Wizara kuhusu uadilifu na utendaji usioridhisha wa baadhi yao. Bila kupenda kuingilia uhuru wa Mabaraza, nimelazimika kuunda Tume ya kuchunguza baadhi ya malalamiko. Wale watakaobaininika wana makosa watachukuliwa hatua stahiki. Mantiki ya Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ni kusogeza huduma ya utoaji haki karibu na wananchi. Kwa kuwa hadi sasa hatuna uwezo kuanzisha Mabaraza kila Wilaya, Mabaraza mengi yanafanya kazi kimkoa na hii imekuwa ni usumbufu kwa wananchi. Tunawasiliana na Wizara ya Katiba na Sheria kuangalia utaratibu wa kutumia Mahakimu Wakazi wa Wilaya kwa wakati huu ambapo mtandao wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya bado haujafikia Wilaya nyingi. Migogoro ya ardhi ni mingi sana, na wanaopendekeza kwamba Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya yafutwe wasisahau kwa nini yaliundwa.
HUDUMA ZA UPIMAJI NA RAMANI
Utayarishaji Ramani
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2011/12, Wizara yangu iliahidi kufunga mtambo mpya wa kisasa wa kuchapisha ramani kwa mahitaji mbalimbali nchini, na kujenga kituo cha kupokelea picha za satellite (Satellite Image Receiving Station) ili kupata takwimu mbalimbali za ardhi kwa ajili ya kuhuisha na kutengeneza ramani mpya za nchi. Mchakato wa kutafuta fedha za utekelezaji wa mpango wa kujenga kituo cha kupokelea picha za satellite unaendelea.
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikiainisha mipaka ya mikoa, wilaya, vijiji na hifadhi za Taifa. Uwekaji wa mipaka hiyo umekuwa ukifanyika kwa kufuata Matangazo ya Serikali ambayo hutoa maelezo yanayozingatia alama mbalimbali za asili kama vile mito, maziwa, mabonde, milima na kadhalika. Kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, baadhi ya alama hizo wakati mwingine hubadilika au kutoweka na kusababisha migogoro ya kiutawala katika maeneo husika. Katika mwaka 2012/13 Wizara yangu itajenga na kuimarisha taarifa za kijiografia (geo-database). Taarifa hizo zitatumika kutafsiri Matangazo ya Serikali yanayoainisha mipaka ya kiutawala ndani ya nchi ili mipaka hiyo iweze kueleweka kwa wahusika wote. Kazi hii itaanza kwa mikoa na wilaya mpya zilizoanzishwa hivi karibuni.
Mipaka ya Kimataifa
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2011/12 Wizara iliahidi kufanya mazungumzo na nchi jirani katika juhudi za kukamilisha makubaliano juu ya mipaka yetu. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa majadiliano na nchi za Comoro na Msumbiji yalikamilika. Mkataba wa kwanza kati ya Tanzania, Msumbiji na Comoro kwenye alama ya utatu baharini inayotenganisha nchi hizi tatu ulikamilika na kutiwa saini tarehe 5 Desemba 2011. Mkataba wa pili kati ya Tanzania, Shelisheli na Comoro ulitiwa saini tarehe 17 Februari 2012. Kwa mantiki hiyo Tanzania imekamilisha upimaji wa mipaka katika Bahari ya Hindi na itatangaza eneo lake lote la ukanda wa kiuchumi baharini (Exclusive Economic Zone) bila ya pingamizi kutoka kwa nchi jirani.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanya mazungumzo na nchi za Burundi na Kenya juu ya uimarishaji wa alama za mipaka. Tanzania na Kenya zimekubaliana kuanza kazi ya uimarishaji wa alama kuanzia Jasini katika mkoa wa Tanga hadi Mkomazi katika mkoa wa Kilimanjaro. Sehemu hiyo ina urefu wa kilometa 100 na alama nyingi zimeharibiwa na ujenzi wa nyumba kwa pande zote za mpaka. Kazi hii itafanyika mwaka 2012/13. Ukaguzi na uimarishaji wa mpaka kati ya Tanzania na Burundi vilevile utafanyika mwaka wa fedha 2012/13.
Upimaji Ardhi chini ya Maji
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2011/12 watumishi watatu walihudhuria mafunzo ya muda mfupi nje ya nchi yaliyohusu upimaji ardhi katika maji yenye kina kifupi baharini. Katika mwaka 2012/13 Wizara yangu inatarajia kununua kifaa cha kupimia vina vya maji (echo sounder). Aidha, Wizara itaendelea kuwapatia mafunzo wataalam katika fani hii ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Kuongeza eneo Nje ya Ukanda wa Kiuchumi Baharini
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2011/12 Wizara yangu iliahidi kukamilisha na kuwasilisha Umoja wa Mataifa Andiko la kudai eneo la nyongeza nje ya maili 200 za ukanda wa kiuchumi baharini. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa niliongoza ujumbe wa Tanzania kuwasilisha Andiko hilo tarehe 18 Januari 2012. Hivi sasa Tume ya Mipaka ya Baharini ya Umoja wa Mataifa inapitia andiko hilo. Serikali ya Tanzania inatakiwa kwenda tena Umoja wa Mataifa kutetea hoja ya kudai eneo hilo tarehe 7 Agosti, 2012. Ninatarajia kuongoza tena ujumbe wa Tanzania kwenye utetezi wa hoja hiyo. Napenda kuchukua fursa hii kuwatambua na kuwashukuru kwa dhati wajumbe wa Kamati ya Uongozi, Kamati ya Ufundi na Kikosi kazi cha Mradi huu. Kwanza ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge walioshiriki katika ziara yangu kuwasilisha andiko letu Umoja wa Mataifa, Mhe. Abdulkarim Esmail Hassan Shah, Mbunge wa Mafia na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na Mhe. Zakia Hamdani Meghji, Mbunge wa Kuteuliwa. Pili nimtambue mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi iliyoongozwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi Ndugu Haji Adam Haji aliyekuwa Mkurugenzi wa Upimaji na Mipangomiji Zanzibar na Dkt. Sellasie David Mayunga, Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza kwa dhati Mwenyekiti wa Kikosi Kazi kilichoandaa Andiko, Profesa Evelyne I. Mbede wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sayansi na Teknolojia katika Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia; Katibu wake Bw. Justo Lyamuya kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na Wajumbe ambao ni Bw. John A. Msemwa wa Wizara ya Ardhi, Bw. Abdon D. Makishe, Bw. Omary J. Mtunguja na Bw. Kelvin R. Komba wote kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli. Wengine ni Prof. Desiderius C.P. Masalu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mhadhiri Bw. Issa A. Hemedi wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Bw. Adam I. Zuberi wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Donald L. Chidowuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Richard A. Maridadi Mwanasheria wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Bw. Pandu S. Makame Mwanasheria aliyekuwa Ofisi ya Makamu wa Rais, Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, Kamati hizi zimefanya kazi nzuri ambayo imewezesha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukamilisha Andiko la kudai kuongeza eneo ndani ya bahari lenye ukubwa wa kilomita za mraba 61,000. Eneo hili litakapopatikana litaiwezesha Tanzania kuvuna rasilimali mbalimbali chini ya bahari kwa manufaa ya sasa na ya vizazi vijavyo. Ni sifa kubwa kwa nchi yetu kufanikisha kazi hii kwa kutumia wataalamu wetu wazawa. Nichukue fursa hii kuwashukuru kwa dhati waajiri wa wajumbe wa Kikosi Kazi kwa kuwaruhusu watumishi hawa kufanya kazi hii, na nawaomba wasichoke kuendelea kutoa ushirikiano hadi kazi hii itakapokamilika na eneo kupatikana. Na inshallah eneo hilo litapatikana kwa manufaa ya Watanzania wote. Nitatumia uzoefu wangu katika Umoja wa Mataifa katika kutekeleza kazi hii nyeti na muhimu. Niwaombe Watanzania wote, wa bara na visiwani kutambua kwamba tunachoshughulikia sasa ni maombi ya eneo ambalo tusipofanikiwa kulipata litabaki chini ya himaya ya Umoja wa Mataifa ambapo mataifa makubwa yatalifaidi. Aidha, ninashukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kufafanua kwamba kazi hii imeshirikisha pande zote za taifa letu ipasavyo na kufuta hisia potofu zilizokuwa zimeibuka zikidai vinginevyo.
Upimaji wa Mipaka ya Vijiji.
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2011/12 Wizara yangu iliahidi kupima mipaka ya Vijiji 350 ambapo hadi kufikia Juni, 2012 jumla ya vijiji 206 vimepimwa katika wilaya za Same (12), Arumeru (28), Longido (10), Mbulu (64), Uyui (66) Manyoni (22) na Kiteto (4). Kutokana na upimaji huo, mpaka sasa jumla ya vijiji vilivyopimwa mipaka nchini ni 11,467. Kwa mwaka 2012/13, Wizara yangu itaendelea na upimaji wa mipaka ya vijiji 200.
Upimaji Milki
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara yangu imeratibu na kuidhinisha upimaji wa viwanja 34,049 na mashamba 2,169 kati ya lengo la viwanja 35,000 na mashamba 800 Katika utunzaji wa kumbukumbu jumla ya plani za viwanja 15,116 zimeingizwa hivyo kufanya jumla ya viwanja vilivyoingizwa katika mfumo wa kielektroniki kuwa 30,304. Vilevile, plani za hati (deed plans) 1,685 kwa viwanja vilivyopimwa nchini zilitayarishwa. Kwa sasa utoaji wa plani za hati unafanyika haraka zaidi kutokana na matumizi ya teknolojia ya digitali.
38. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu inatarajia kuidhinisha upimaji wa viwanja 40,000 na mashamba 1,000 kutoka katika miji na vijiji mbalimbali nchini. Pia Wizara itajenga alama 300 za vianzio vya upimaji (Control points densification) katika miji 50 ili kurahisisha upimaji ardhi nchini. Vilevile, Wizara yangu itaendesha mafunzo ya utumiaji wa mtandao mpya wa upimaji ardhi nchini kwa wapima ardhi. Ili kuharakisha upangaji na upimaji wa ardhi Halmashauri za Wilaya na miji nchini zinashauriwa kununua vifaa vya kisasa vya Upimaji ardhi. Ni jambo la kusikitisha kwamba katika Halmashauri kadhaa wapima hawana hata darubini ya kawaida, nisipozungumzia vifaa vya kisasa kama GPS (Global Positioning System) na Total Station. Hii si kwa sababu ya umaskini bali kutoelewa kwamba fani hii haiwezekana bila kuwa na vifaa vya msingi.
Mfuko wa Kupima Viwanja
39. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kusimamia mfuko wa mzunguko wa kupima viwanja (Plot Development Revolving Fund – PDRF) unaozipatia mikopo Halmashauri kwa ajili ya kutayarisha michoro ya mipango miji, kulipa fidia, kupima viwanja na kumilikisha. Hadi Juni 2012 mfuko wa PDRF ulikuwa na jumla ya Shilingi milioni 606. Aidha, Halmashauri 29 hazijarejesha jumla ya Shilingi milioni 466.6. Wizara imepokea maombi kutoka Halmashauri 8 ya jumla ya Shilingi milioni 5,050 Kwa sasa Wizara inachambua maombi hayo na kutayarisha utaratibu mpya utakaowezesha kukopesha na kurejesha kwa wakati. Napenda kurudia maelekezo yangu kwa Halmashauri zilizokopeshwa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuziwezesha Halmashauri nyingine kukopa kwa ajili ya kutwaa maeneo na kupima na kumilikisha ardhi.
40. Mheshimiwa Spika, kupitia mradi wa viwanja 20,000 Wizara yangu ilizikopesha Halmashauri nne jumla ya Shilingi bilioni 1.87. Fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya kuandaa ramani za mipango miji, kulipa fidia, kupima na kumilikisha viwanja. Hadi Juni 2012 jumla ya Shilingi milioni 650 zimerejeshwa na Shilingi bilioni 1.22 hazijarejeshwa. Halmashauri ambazo bado hazijarejesha ni za Manispaa ya Morogoro (Shilingi milioni 50); Mji wa Kibaha (Shilingi milioni 270.4); Manispaa ya Kinondoni (Shilingi milioni 500) na Manispaa ya Ilala (Shilingi milioni 400) Kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) zitaweka utaratibu utakaozilazimisha Halmashauri zilizokopeshwa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati. Ninachukua pia fursa hii kutangaza kuwa nimeagiza kwamba katika asilimia 30 ya makusanyo ya kodi za ardhi yatakayofanyika na ambayo yatarejeshwa kwenye Halmashauri, Wizara yangu itakata madeni ya wadaiwa hawa sugu kabla ya kuwalipa shea yao hiyo. Sina budi kuzipongeza Halmashauri za Bagamoyo na Temeke, kwa kumaliza kulipa deni lao. Jambo hili nalo si umaskini bali ukosefu wa nidhamu ya kifedha (financial indiscpline)
MIPANGO MIJI NA VIJIJI
Uandaaji na Utekelezaji wa Mipango ya Uendelezaji Miji
41. Mheshimiwa Spika, katika upangaji wa miji, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri huandaa mipango ya muda mrefu na ya muda mfupi. Katika mwaka 2011/12, Wizara yangu ilikamilisha uandaaji wa Mpango wa muda mfupi wa mji mdogo wa Kyaka - Bunazi. Aidha, ilikamilisha uandaaji wa Mpango kabambe wa Jiji la Tanga na iliendelea na maandalizi ya Mpango Kabambe wa Mji wa Bagamoyo. Pia, Mtaalam mshauri anayeandaa Mpango Kabambe wa Jiji la Dar es Salaam aliwasilisha rasimu ya awali ya mpango huo ambao ataukamilisha mwaka 2012/13.
42. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri itakamilisha Mpango Kabambe wa mji mdogo wa Bagamoyo na katika Jiji la Mbeya itaandaa Mpango Kabambe wa Jiji hilo. Vilevile, itaendelea kuandaa mpango wa mji mdogo wa Makambako, na Mji mdogo wa Mafia.
43. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni iliendelea kuandaa mpango wa uendelezaji upya eneo la Manzese na ilikamilisha maandalizi ya mpango wa Makongo Juu na kuanza maandalizi ya kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mpango. Pia, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Njombe, ilianza uandaaji wa mpango wa uendelezaji upya wa eneo la kati la mji huo. Kwa mwaka 2012/13 Wizara itaendelea kushirikiana na Halmashauri hizo kukamilisha na kutekeleza mipango hiyo. Natoa wito kwa Mamlaka zote za Miji na Wilaya nchini kutenga fedha za kuandaa na kutekeleza mipango hiyo ambayo ni msingi wa usimamizi wa uendelezaji wa miji.
44. Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea na utekelezaji wa mradi wa uendelezaji upya eneo la Kurasini ulioanza mwaka 2006, kwa lengo la kuwezesha eneo hilo kutumika kikamilifu kwa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuifanya iwe lango kuu la biashara kitaifa na kimataifa. Katika mwaka 2011/12 Wizara ililipa fidia ya jumla ya Shilingi milioni 550 kwa wakazi wa Mtaa wa Kurasini waliopo jirani na mabwawa ya majitaka. Pia, kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi imetayarisha michoro inayoonesha ukanda wa barabara inayounganisha barabara ya Mandela na daraja la Kigamboni kwa upande wa Kurasini na kutambua ardhi na mali zilizopo katika ukanda huo wa barabara. Kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu itaendelea kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kufanya maandalizi ya eneo la ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Biashara kwenye eneo lililotengwa kwa ajili ya upanuzi wa Bandari Kurasini. Aidha napenda kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa Serikali imetenga fedha kwenye bajeti ya mwaka 2012/13 chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kulipa fidia kwa wananchi watakaopisha mradi huo katika eneo la Kurasini na Shimo la Udongo.
Urasimishaji Makazi Holela
45. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2011/12, Wizara yangu ilikamilisha uandaaji wa Programu ya Taifa ya kuzuia na kurasimisha Makazi Holela na iko katika hatua ya utekelezaji. Pia, kwa kushirikiana na Jiji la Mwanza ilirasimisha makazi 2,810. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni ilihakiki mipango ya urasimishaji 16. Kwa mwaka 2012/13, Wizara itachapisha, kusambaza na kuanza utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kuzuia na Kurasimisha Makazi Holela mijini kwa kushirikiana na MKURABITA, Halmashauri za Miji na Wilaya na wadau wote. Pia itarasimisha makazi 4,000 katika Jiji la Mwanza. Halmashauri zote nchini zinaagizwa zihakikishe kuwa zinapima viwanja na kuvigawa kwa wananchi ili kuepusha ujenzi holela. Wananchi wanaokaidi mipangomiji na kujenga kiholela, kuvamia maeneo ya wazi na kujenga katika maeneo yanayolindwa kisheria hususan fukwe na maeneo hatarishi, wasitegemee kupewa fidia wakati wa kuhamishwa. Tuko tayari kupokea maombi yenu kupewa viwanja au nyumba kuliko kupoteza akiba yenu kujenga visivyo.
Uendelezaji Miji Mipya na Vituo vya Huduma
46. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka 2011/12, Wizara yangu iliendelea kushirikiana na Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam katika kutekeleza mkakati wa kuanzisha vituo vya Huduma kwenye maeneo ya pembezoni mwa miji kwa kushirikisha sekta binafsi. Kwa upande wa Kituo cha Huduma cha Luguruni, Wizara imekamilisha mchakato wa kupata mwendelezaji mwenza (Co - Master Developer) ambaye ni kampuni binafsi itakayoshirikiana na Serikali katika uendelezaji wa kituo hicho. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imeainisha eneo jipya la Mikwambe kwa ajili ya kujenga kituo cha huduma katika Manispaa hiyo badala ya Kongowe. Kwa mwaka 2012/13 itaanza utekelezaji wa ujenzi wa Kituo cha Huduma cha Luguruni kwa ushirika kati ya Sekta binafsi na Serikali.
47. Mheshimiwa Spika Katika mwaka 2011/12 Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, ilikamilisha maandalizi ya msingi ya kuwezesha kutekeleza Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni. Kwa mwaka 2012/13 Wizara itasimamia uundwaji wa Wakala; Kuidhinisha mpango na kuanza utekelezaji; Kufanya uthamini wa mali zilizomo katika maeneo ya miundombinu, huduma za jamii na eneo la makazi mbadala (resettlement area); Kulipa fidia kwa mali zilizomo katika maeneo yaliyofanyiwa uthamini; Kuandaa michoro ya kina; kupima na kuandaa ramani za ujenzi zilizomo katika eneo la makazi mbadala; Kupima maeneo nje ya maeneo ya miundombinu kwa awamu na kuendelea na utekelezaji kwa awamu. Awamu ya kwanza ni kati ya 2012-2022, awamu ya pili ni kati ya 2022- 2027 na awamu ya tatu ni 2027-32. Gharama ya mradi inakisiwa kufikia Shiling trillion 11.6. Pamoja na kwamba asilimia 59% ya bajeti ya Wizara, takriban bilioni 60, zimetengwa kwa ajili ya Mradi wa Kigamboni, kiasi hiki ni asilimia 10 tu ya pesa tunazohitajika mwaka huu. Kwa hiyo tutatumia mbinu za kisasa kutafuta pesa nyingine, takribani bilioni 605 nje ya bajeti kutekeleza mradi huu bila kuchelewa zaidi. Mradi utahitaji kiasi hicho cha fedha kwa miaka 3 ya kwanza. Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wananchi wa Kigamboni kwa uvumilivu wao na ushirikiano wanaotuonesha na ninawahakikishia kuwa Serikali sasa imetenga bajeti ya kuhakikisha utekelezaji wa mpango huu unaanza na kushamiri. Nitasimamia mradi huu kwa karibu kwa kasi, ari na nguvu mpya. Ninataka kuanza na ziara za mafunzo (study tours) kwa wawakilishi kutoka Kigamboni kutembelea miji mipya ili tuwe na uelewa wa pamoja juu ya kazi iliyombele yetu. Aidha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi watapewa maeneo ya kuanza kujenga makazi ambayo yatatumika kuwahamisha wananchi watakaopenda kubaki Kigamboni. Tunashauri ikiwezekana wote wachague kubaki maana hivi sasa kuna wananchi takribani 82,000 wakati tunajenga mji mpya wenye uwezo wa wakazi 400,000. Hakuna sababu ya wananchi kuhama eneo hili ila makazi yao yatapangwa upya na kuboreshwa. Serikali imeamua kuunda wakala mpya, Kigamboni Development Agency (KDA) kusimamia mradi huu wa kipekee katika historia ya Taifa letu. Wananchi ambao hawajakiuka maagizo ya mradi kwa kufanya maendelezo haramu, wasiwe na wasiwasi kuhusu fidia kwa sababu mradi utazingatia haki zao na ni endelevu. Fidia itatolewa kwa mujibu wa sheria, kwa tathmini ya kiujumla ambayo itakokotolewa kutokana na viwango vya soko na kuhuishwa ili iwe sahihi (land values under mass valuation).
Usimamizi wa Uendelezaji Miji
48. Mheshimiwa Spika, eneo la mto Msimbazi ni eneo ambalo lilibainishwa kuwa wazi katika mpango kabambe wa Jiji la Dar Es Salaam wa mwaka 1979. Hata hivyo eneo hilo limeendelezwa kwa matumizi mbalimbali ambayo yanakinzana na mpango huo. Kutokana na uvamizi huo, madhara makubwa hutokea katika eneo hilo. Mfano mwezi Desemba mwaka 2011 watu walipoteza maisha na mali kutokana na mafuriko katika eneo hilo. Hali hii iliigharimu Serikali fedha nyingi katika kuwaokoa, kuwahifadhi na kuwatafutia makazi wahanga wa mafuriko. Natoa pole kwa waathirika wa mafuriko hayo pamoja na Waheshimiwa Wabunge wao.
49. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri za Manispaa za Ilala na Kinondoni ilianza maandalizi ya mpango wa kuhifadhi Bonde la Mto Msimbazi kuwa eneo la kijani. Eneo hilo linaanzia milima ya Pugu hadi Daraja la Salenda lina hekta 1,924. Mchakato wa kuhifadhi bonde hilo utafanyika kwa awamu mbili, awamu ya kwanza itaanzia kwenye Daraja la Salenda Upanga hadi Vingunguti lenye ukubwa wa hekta 1,121. Awamu ya pili itaanzia Vingunguti hadi milima ya Pugu. Hadi sasa Wizara imebainisha mipaka na kuandaa mchoro wa eneo la mpango na kutangaza kwenye Gazeti la Serikali (GN Na. 227) la tarehe 5 Aprili, 2011. Kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala na Kinondoni zitaendelea na uandaaji wa mpango huo.
50. Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza tena kuwa eneo la Bonde la Mto Msimbazi ni eneo hatarishi kwa makazi ya binadamu, hivyo mamlaka za upangaji zichukue hatua za haraka kuondoa makazi na maendelezo yote yaliyofanyika humo kwani hayana mustakabali. Ni dhahiri kwamba maafa ya mara kwa mara katika eneo hilo hayaepukiki hasa ukizingatia mabadiliko ya tabianchi. Vilevile, naagiza Halmashauri zote kuainisha maeneo yote hatarishi hususan mabonde na milimani na kuyawasilisha kwangu kwa ajili ya kuyatangaza kwenye Gazeti la Serikali. Natoa wito kwa wadau wote, kutoa ushirikiano unaostahili ili kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanyika kwa manufaa ya wakazi wote wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine.
MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI
51. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara yangu kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, ilitoa mafunzo kuhusu sheria za ardhi, matumizi ya teknolojia ya utunzaji wa kumbukumbu (Geographical Information System) na mbinu shirikishi za utayarishaji wa mipango ya matumizi ya ardhi. Katika kipindi hicho, jumla ya watendaji 51 kutoka Halmashauri za Wilaya 14 za ukanda wa Pwani walipatiwa mafunzo hayo. Vilevile, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ilifanya tathmini ya uwezo wa rasilimali za ardhi ngazi ya kijiji katika vijiji 18 vya Wilaya za Pangani, Muheza, Mkinga, Rufiji na Mafia kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.
Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya na Vijiji
52. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi iliendelea kushirikiana na Halmashauri za Wilaya na wadau mbalimbali katika kuandaa na kutekeleza mipango ya matumizi ya ardhi katika ngazi za vijiji na wilaya. Katika kipindi hicho mipango ya matumizi ya ardhi iliandaliwa katika vijiji 82 kwenye Wilaya 26. Kwa mwaka 2012/13, Wizara yangu itaandaa taarifa mbalimbali za vijiji nchini ili kuwa na kumbukumbu sahihi zitakazosaidia katika uandaaji wa mipango ya makazi vijijini.
53. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13, Wizara kupitia Tume itatekeleza Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi kwa kutayarisha mipango ya matumizi ya ardhi kwa ushirikishwaji katika vijiji 150. Mipango hiyo itaandaliwa katika wilaya za Kilombero, Ulanga na Rufiji ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya Southern Agriculture Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT). Aidha, vijiji vingine vya mipakani katika wilaya 16 za Tarime, Rorya, Same, Kibondo, Ngara, Misenyi, Longido, Ngorongoro, Rombo, Mwanga, Hai, Momba, Kyerwa, Karagwe, Karambo na Kakonko vitaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi. Vilevile, itaandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya Wilaya 4 za Mpanda, Chunya, Kilombero na Ulanga na kutoa mafunzo kwa watendaji katika Wilaya hizo kuhusu matakwa ya sheria za ardhi na mbinu shirikishi za utayarishaji wa mipango hiyo.
54. Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuzipongeza Halmashauri za Wilaya zilizokuwa zimetenga fedha katika mwaka 2011/12 kwa ajili ya kutayarisha mipango ya matumizi ya ardhi katika ngazi za vijiji ambazo ni Tandahimba, Korogwe, Monduli na Songea Vijijini. Napenda kuendelea kusisisitiza umuhimu wa Halmashauri za Wilaya kutenga bajeti kwa ajili ya kupanga mipango ya matumizi ya ardhi ngazi ya vijiji.
MAENDELEO YA NYUMBA
55. Mheshimiwa Spika, Sekta ya nyumba inatoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi, mapato ya Serikali, kuongeza nafasi za ajira na kupunguza umaskini. Katika mwaka wa fedha 2011/12 tayari baadhi ya Halmashauri zimeanza kuomba mikopo kutoka mabenki kwa ajili ya uendelezaji wa ardhi na kuweka miundombinu. Halmashauri hizo ni pamoja na Temeke na Kinondoni.
56. Mheshimiwa Spika, kuhusu upatikanaji wa mtaji wa kukopesha kwa muda mrefu, Serikali ilianzisha Tanzania Mortgage Refinancing Company (TMRC) mwaka 2010, ambayo imeendelea kuvutia uwekezaji wa mabenki zaidi. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa baadhi ya mabenki na vyombo vya fedha vimekubali kutoa mikopo kwa wananchi ili kuwawezesha kununua nyumba kwa kutumia mikopo ya muda mrefu hadi kufikia miaka 25. Nachukua fursa hii kuyapongeza mabenki yaliyojitokeza kutoa mikopo kwa ajili ya kuendeleza nyumba. Kwa upande wetu Wizara itaendelea kuboresha mazingira kwa mabenki kutoa mikopo ya kujenga na pia kununua nyumba kwa kuhimiza Wizara ya Fedha na Benki kuu kuunda chombo cha kutoa bima ya mikopo ya nyumba (housing loans insurance mechanism).
57. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2011/12 Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ilikamilisha kuandaa mwongozo wa kuunda na kuendesha vyama vya ushirika wa nyumba. Mwongozo huo utatumika wakati wa uhamasishaji wa wananchi kuunda vyama vya ushirika wa nyumba. Kwa wananchi wanaofanya kazi za kujiajiri wanashauriwa waanzishe vikundi vya ushirika wa nyumba katika maeneo yao. Chama cha ushirika wa nyumba kinaweza kusajiliwa ikiwa idadi ya wanachama waanzilishi inatimia watu kumi (10) au zaidi. Natoa wito kwa waajiri kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika wa nyumba kwenye sehemu za kazi.
58. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara yangu ilikusanya takwimu za hali ya nyumba katika miji ya Shinyanga, Musoma, Bukoba, Tabora, Singida, Mtwara, Songea, Lindi, Njombe, Kigoma, Manyara, Rukwa, Bagamoyo na Kibaha. Taarifa zilizopatikana zitaiwezesha Serikali na wadau wengine wakiwemo waendelezaji milki na benki kufanya maamuzi yanayohusu nyumba kwa kuzingatia takwimu za uhakika. Pia, taarifa hizo zitawezesha nchi yetu kupima mafanikio yake Kikanda na Kimataifa katika sekta ya nyumba.
59. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imekamilisha maandalizi ya rasimu ya Sera ya Taifa ya Nyumba. Sera hiyo inaweka msingi wa kuongoza na kusimamia uendelezaji wa nyumba. Kwa mwaka 2012/13, Wizara yangu itaratibu ukamilishaji wa Sera ya Nyumba na kutayarisha mpango mkakati na programu ya utekelezaji wake. Pia, itaanza mchakato wa kutunga Sheria ya Nyumba.
Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba na Vifaa vya Ujenzi
60. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara yangu kupitia Wakala iliendelea kufanya utafiti na kubuni mbinu za kujenga nyumba kwa gharama nafuu kwa kutumia malighafi zinazopatikana hapa nchini. Utafiti ulifanyika ndani na nje ya maabara. Vilevile, kazi za ushauri zilifanyika kwa wateja mbalimbali zikiwemo Ofisi za Serikali na watu binafsi.
61. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 mafunzo ya vitendo yalifanyika kwa vijana 380 kutoka katika Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Pwani. Mafunzo hayo yaliwezesha kuanzishwa kwa vikundi 38 vya ujenzi wa nyumba na uzalishaji wa vifaa vya ujenzi na vilipatiwa mashine 114 za kufyatulia matofali yanayofungamana na mashine 28 za kutengenezea vigae vya kuezekea pamoja na kalibu za vigae 1,400. Pia, mashine za uzalishaji wa vifaa vya ujenzi zilisambazwa katika maeneo mbalimbali nchini Lengo ni kuhakikisha kuwa teknolojia ya ujenzi wa nyumba bora na za gharama nafuu inawafikia wananchi walio wengi.
62. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13 semina za uhamasishaji na kueneza teknolojia za ujenzi wa nyumba bora na za gharama nafuu zitafanyika katika Wilaya za Arusha Vijijini, Nkasi, Kishapu, Chunya, Tandahimba na Muleba.
SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA
Kuimarisha Utendaji kazi wa Shirika
63. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Shirika la Nyumba la Taifa liliendelea na utekelezaji wa mpango mkakati wa kipindi cha miaka mitano (2010/11-2014/15). Kulingana na malengo ya mpango huu, Wizara kupitia Shirika la Nyumba la Taifa, iliimarisha ufanisi wa utendaji kazi kwa kuweka mfumo wa tathmini na ufuatiliaji na kuboresha utendaji wao; kuwapatia mafunzo wafanyakazi 535 kati ya 546 kuhusu mbinu za utendaji wa kisasa na kuingia mikataba ya kiutendaji; kufuta mikataba ya ubia 59 isiyokuwa na tija kwa Shirika na kurekebisha mikataba 311 kati ya Shirika na wadau wake.
Ardhi kwa Ajili ya Ujenzi wa Nyumba
64. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Shirika limeanza utekelezaji wa jukumu la kuwa Mwendelezaji Mkuu (Master Developer). Katika kutekeleza jukumu hili, Shirika lilinunua ardhi yenye ukubwa wa ekari 1,372.1 katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya ujenzi wa nyumba. Lengo la ununuzi huu, ni kuongeza hazina ya ardhi. Vilevile, ununuzi wa maeneo mengine yenye ukubwa wa ekari 26,887.9 katika Wilaya mbalimbali nchini uko katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Kwa mwaka 2012/13, Wizara kupitia Shirika la Nyumba la Taifa itaendelea na ununuzi wa vipande vya ardhi vilivyotambuliwa katika maeneo mbalimbali nchini. Natoa wito kwa Halmashauri za Miji na Wilaya kutenga ardhi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba kwa pamoja (Real estate) utakaofanywa na Shirika la Nyumba.
Ujenzi wa Nyumba za Biashara na Makazi
65. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Shirika liliendelea na matayarisho ya miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi na biashara 9,000 katika maeneo mbalimbali nchini. Kati ya nyumba hizo, ujenzi wa nyumba 1,620 ulikamilika. Miradi iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa iko katika maeneo mbalimbali nchini zikiwemo Wilaya mpya ambazo ni Mvomero, Kongwa, Longido na Ilembo – Mpanda. Kwa mwaka 2012/13, Shirika litaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa nyumba 7,380 katika Wilaya mbalimbali nchini ikiwemo makao makuu ya mikoa na Wilaya mpya.
67. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Serikali kupitia Wizara ya Fedha ililiruhusu Shirika kukopa kiasi cha Shilingi bilioni 300 kutoka kwenye vyombo vya fedha vya ndani na nje ya nchi. Kutokana na kibali hicho, benki 15 za ndani na nje ya nchi zilikubali kulikopesha Shirika kiasi hicho. Hadi Juni, 2012 Shirika liliingia mikataba na benki tisa (9) zilizokubali kutoa mikopo ya jumla ya Shilingi bilioni 165.4. Kwa mwaka 2012/13, Wizara kupitia Shirika la Nyumba la Taifa itaendelea kuzihamasisha benki nyingine kutoa mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na kuwahamasisha wananchi kununua nyumba zinazojengwa na Shirika.
68. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Shirika lilitarajia kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni 43.14 kutokana na kodi za pango la nyumba linazozimiliki. Hadi Juni, 2012, Shirika lilikusanya jumla ya Shilingi bilioni 53.17 sawa na asilimia 123 ya lengo. Pia, Shirika lilichangia jumla ya Shilingi bilioni 11.47 kwenye pato la Serikali kutokana na kulipa kodi mbalimbali kutokana na shughuli zake. Kwa mwaka 2012/13, Shirika linatarajia kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 52.97 kutokana na kodi ya pango la nyumba zake na kuchangia mapato ya Serikali jumla ya Shilingi bilioni 24.2 kwa kulipa kodi ya pango la ardhi, kodi ya ongezeko la thamani na kodi ya majengo. Nachukua fursa hii kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Shirikika la Nyumba la Taifa, Nd. Nehemia Mchechu na timu yake kwa kufanikiwa kubadilisha sura ya Shirika la nyumba kwa muda mfupi. Changamoto nyingi zimejitokeza katika kuleta mabadiliko hayo lakini ubunifu na bidii inayoshuhudiwa unaridhisha na kuashiria mageuzi makubwa zaidi hasa kama mikopo ya benki iliyochukuliwa italipwa kama ilivyopangwa na kukomesha ukata uliotishia uhai wa Shirika kabla ya mageuzi haya. Bila kuingilia manajimenti ya siku hadi siku, Wizara inasimamia kwa karibu masuala ya kisera ikiwemo kuanzisha utaratibu wa kuwasemehe kodi wale ambao kwa sababu za msingi watashindwa kulipa kodi mpya za pango ya nyumba za Shirika.
HUDUMA ZA KISHERIA
69. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13, Wizara yangu itakamilisha marejeo ya Sheria ya Mipangomiji ya mwaka 2007; Sheria ya Usajili wa Ardhi (Sura ya 334); Sheria ya Usajili wa Nyaraka (Sura ya 117); na Sheria ya Usajili wa Rehani ya Mali Zinazohamishika (Sura ya 210). Pia itakamilisha muswada wa sheria uthamini na usajili wa Wathamini na kuendelea kuzifanyia mapitio Sheria za Ardhi ili ziendane na matakwa ya wadau.
HUDUMA ZA UTAWALA NA RASILIMALI WATU
70. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2011/12 Wizara yangu iliendelea kuwawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Katika kipindi hicho jumla ya watumishi 190 walipandishwa vyeo na 5 walithibitishwa kazini. Aidha, watumishi 586 walihudhuria mafunzo mbalimbali kama ifutavyo:- Mafunzo ya muda mrefu na mfupi ndani na nje ya nchi watumishi 60, mafunzo yaliyohusu maadili katika utumishi wa umma watumishi 206, mafunzo elekezi ya awali kwa waajiriwa wapya 106, na mafunzo kuhusu utunzaji wa siri na nyaraka za serikali kwa watumishi 214. Kwa mwaka 2012/13, Wizara inatarajia kuwapatia mafunzo watumishi 400 katika fani mbalimbali.
Vyuo vya Ardhi
71. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inasimamia vyuo vya Ardhi vya Tabora na Morogoro ambavyo vinatoa mafunzo ya Stashahada (Ordinary Diploma) katika fani za urasimu ramani na upimaji ardhi, na Cheti (Certificate) katika fani za umiliki ardhi, uthamini na uchapaji ramani. Katika mwaka 2011/12 walihitimu wanafunzi 153. Kati ya hao, 92 walitoka Chuo cha Ardhi Morogoro na 61 walitoka Chuo cha Ardhi Tabora. Kati ya wahitimu hao wanawake ni 31 na wanaume ni 122. Naomba nisisitize kuwa Halmashauri ziajiri wataalam hawa ili kuziba pengo la ajira lililopo katika maeneo yao. Wataalam wanaohitimu katika vyuo hivi ndio wanaofanya kazi uwandani (field work). Sioni sababu ya baadhi ya Halmashauri kutokuwa na watumishi wakati vyuo vyetu vinatoa wataalam kila mwaka.
72. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2011/12, Wizara imekamilisha ujenzi wa bweni la wavulana katika Chuo cha Ardhi Tabora ikiwa ni hatua muhimu katika kuongeza udahili na kuboresha huduma ya malazi kwa wanafunzi. Kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa bweni hili, mwaka 2012/13 Wizara itaongeza idadi ya wanafunzi watakao dahiliwa katika chuo cha Ardhi Tabora. Pia, vyuo hivi vitaandaa na kutekeleza mpango wa mafunzo ya muda mfupi kwa wataalam wa sekta ya ardhi katika Halmashauri zote nchini kwa lengo la kuboresha utaalam wao. Mafunzo hayo yatatolewa kwa wataalam walioko katika taasisi za umma na sekta binafsi kwa kuwasilisha maombi.
SHUKRANI
73. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ina majukumu mengi na yanayogusa moja kwa moja Watanzania wote. Ni mategemeo yangu kwamba, Bunge litaendelea kuwa na mtizamo chanya na kuipa kipaumbele sekta ya ardhi kwa ujumla ili kuiwezesha kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
74. Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyofikiwa na Wizara yangu ni kutokana na kuwepo kwa ushirikiano kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo zikiwemo taasisi za fedha za kimataifa, nchi wahisani, taasisi zisizokuwa za kiserikali na mashirika ya kidini. Wadau hao ni pamoja na Benki ya Dunia, Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-HABITAT), Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GTZ); na Serikali za Denmark, Sweden, Uholanzi na Uingereza kupitia Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Business Environment Strengthening for Tanzania); na Serikali za Finland na Norway.
HITIMISHO
75. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu imeazimia kutekeleza mipango ya kuendeleza ardhi, nyumba na makazi ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye kaulimbiu ya Kilimo Kwanza na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16). Aidha, mbali na kuunda Wakala wa Kuendeleza Mji Mpya wa Kigamboni (KDA), Serikali itakamilisha uanzishaji wa chombo kitakachosimamia utoaji wa ardhi kwa wawekezaji kwa utaratibu mpya wa wananchi kutumia ardhi kama mtaji (land for equity). Vilevile, itahakikisha kuwa migogoro ya ardhi inayoendelea kujitokeza inatafutiwa ufumbuzi na kuzuia migogoro mingine isitokee.
76. Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo Wizara yangu imejipanga kutayarisha mipango ya kuendeleza miji na vijiji na kuisimamia, kupanga matumizi ya ardhi, kupima ardhi, kuhakiki milki, kusajili na kutoa hati ili kuwezesha kuwepo kwa usalama wa milki. Natoa rai kwa mamlaka na asasi mbalimbali kutoa ushirikiano unaotakiwa kuhakikisha kuwa ardhi inaziwezesha sekta zote ili kufikia malengo ya maisha bora kwa kila Mtanzania.
MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2012/13
77. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imejipanga kutekeleza majukumu yake iliyojiwekea ili kufikia malengo ya MKUKUTA II, Dira ya Taifa ya 2025, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16), Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010 na Malengo ya Milenia. Hivyo, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liidhinishe Makadirio ya Mapato na Matumizi kama ifuatavyo:-
78. Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru tena wewe na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Hotuba hii inapatikana kwenye tovuti ya Wizara www.ardhi.go.tz.
79. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
5 comments:
Have you ever considered creating an e-book or guest authoring on other blogs?
I have a blog based upon on the same topics you discuss and would love to have you share some stories/information.
I know my subscribers would value your work.
If you are even remotely interested, feel free to send me an e mail.
Also visit my blog post :: CHEAP LEAFLET PRINTING
Ӏ am reаlly enjoying thе theme/design of your weblog.
Dο you ever run into any web brοωser
compatіbilіty problems? A couple of my blog audience hаvе cоmplаined about mу blog not wοrkіng cοггectly in Explorеr but looks greаt
іn Chrome. Dο you have any advicе to helρ fix thiѕ issue?
My site: fotmax diet
What's up to every one, the contents existing at this site are in fact amazing for people experience, well, keep up the good work fellows.
Also visit my site :: ganhar massa Muscular
A person neсessarily aѕsist to make signifiсantly аrticles
I'd state. This is the very first time I frequented your web page and so far? I amazed with the research you made to make this particular post amazing. Great job!
Also visit my site : tomar creatina
Way cool! Some extremely valid points! I appreciate you penning this
post and the rest of the website is extremely good.
Post a Comment