ABIRIA WAUA WALIOTAKA KUTEKA NDEGE YAO...

Imefahamika kuwa watu wawili ambao wanadaiwa kujaribu kuteka ndege China walipata kipigo hadi kufa kutoka kwa abiria na wafanyakazi wa ndege hiyo.
Watu hao walikuwa sehemu ya kundi la watu sita lenye nguvu wenye umri kati ya miaka 20 hadi 36, ambao walijaribu kuteka ndege ya Tianjin Airlines iliyokuwa safarini Urumqi Ijumaa iliyopita.
Dakika kadhaa baada ya ndege hiyo iliyokuwa imebeba abiria 101 kuruka kutoka Uwanja wa Hetian, kusini-magharibi mwa Xinjiang, wanaume watatu mbele na watatu nyuma walisimama na kutangaza mipango yao ya kutisha abiria, kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana.
Kundi hilo, wote kutoka Jiji la Kashgar lililoko magharibi mwa Xinjiang, kisha wakavunja vifumbato vya alumini na kuwashambulia navyo abiria wakati wakijaribu kuingia kwa nguvu chumba cha marubani, msemaji wa serikali ameeleza.
Walishambuliwa na polisi na abiria ambao waliwafunga kwa mikanda kabla ndege haijageuza njia na kurejea tena uwanjani salama dakika 22 tu baadaye.
Abiria kadhaa na wafanyakazi wa ndege hiyo walijeruhiwa kwenye mapambano hayo. Watuhumiwa hao wa utekaji walipelekwa hospitali ambako wawili kati yao walifariki dunia baadaye, imeelezwa.
Imeelezwa wengine wawili walipatiwa matibabu hospitalini baada ya kujikata wenyewe, lakini hazikupatikana taarifa zaidi.
Msemaji wa serikali wa eneo hilo aliongeza watu walikuwa walikuwa na vitu vinavyohisiwa kuwa mabomu kwenye ndege hiyo. Polisi walikuwa bado wanachunguza zaidi vitu hivyo jana.
Xinjiang kuna idadi kubwa ya watu wa jamii ndogo ya Uighurs, lakini iko chini ya utawala wa jamii ya Hans ambao ndio wengi zaidi katika eneo nchini China.
Kumekuwa na misuguano kati ya mamlaka na jamii ya Uighurs katika siku za karibuni kuhusu udhibiti wa serikali dhidi ya dini na utamaduni.
Kundi la haki za ughaibuni limesema tukio hilo halikuwa utekaji nyara ila ni vurugu za kugombea viti ndani ya ndege.
Dilxat Raxit, msemaji wa Umoja wa World Uyghur Congress chenye makao yake Ujerumani ambacho kinafanya kampeni kudai haki za wa-Uighur, alisema lile halikuwa jaribio la utekaji nyara ila vurugu za kugombea viti ndani ya ndege.
Tukio la Ijumaa lilitokea siku chache tu kabla ya kumbukumbu ya ghasia za Julai 2009 mjini Urumqi ambapo karibu watu 200 waliuawa katika mapigano kati ya makabila ya Han na Uighurs nchini China.
Hofu imetanda mjini Hotan, ambako mamlaka zilishambulia shule ya kidini hivi karibuni na kuendesha msako wa nyumba hadi nyumba, kwa mujibu wa Umoja wa Uighur American wenye makao yake makuu mjini Washington.

No comments: