JE, WAJUA? HUYU NDIYE ANAMTOA UDENDA BILIONEA WA CHELSEA...

Kocha wa timu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani, Jurgen Klopp ndiye mwenye nafasi kubwa ya kuziba nafasi ya Andre Villas-Boas aliyetimuliwa kwenye klabu ya Chelsea ya England.
Kwa mujibu wa gazeti la Sportsmail inasemekana kocha huyo mwenye miaka 44 ndiye anayemvutia zaidi mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich katika orodha ndefu ya makocha wanaowania kutawazwa kuwa kocha wa tisa klabuni hapo.
Katika orodha hiyo, inasemekana makocha Pep Guardiola na Jose Mourinho nafasi yao imepungua kufuatia kushindwa kupokea simu kila walipopigiwa.
Msimu uliopita, Klopp ameiwezesha Dortmund kutwaa taji lao la kwanza la ligi ya Ujerumani maarufu kama Bundesliga tangu mwaka 2002 na kuirejesha timu hiyo kwenye ramani ya soka la Ulaya kwa kuifanya moja ya timu tishio.
Kocha huyo ameweza kukisuka kikosi cha Dortmund kwa kuibua wachezaji chipukizi kama Mario Gotze, Mats Hummels na Sven Bender, na kwa hatua hiyo ameweza kumtoa udenda Abramovich.
Wakati akionekana kama mtu sahihi nyumbani kwao kumrithi kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynckes, Klopp hivi karibuni amesaini mkataba mpya utakaomwezesha kubaki Dortmund hadi mwaka 2016. Lakini hiyo haiondoi uwezekano wa kocha huyo kukwepa vishawishi vya mamilioni ya fedha kutoka kwa Abramovich anayemsaka kwa udi na uvumba kukinoa kikosi cha Chelsea kipindi hiki cha majira ya joto.
Msaidizi wa Villas-Boas, Muitaliano Roberto Di Matteo tayari amekabidhiwa mikoba ya kukinoa kikosi cha Chelsea akiwa kama kocha wa muda.
Lakini Di Matteo aliliambia Eurosport, “Siku zote nitamheshimu Villas-Boas, lakini sitailazia damu nafasi hii niliyopata. Utawezaje kusuasua unapopata nafasi ya kuinoa moja ya klabu kubwa za soka duniani?
“Nilifanya kila ninaloweza na Andre anafahamu hilo. Sikuwahi kumhujumu na maamuzi yote tuliyofikia, tulifanya pamoja.”
Wakati huohuo, Chelsea imemtimua kiungo wake Jacob Mellis baada ya kukiri kosa la kuchoma mafataki na kusababisha hewa nzito kwenye Uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo uliopo Cobham.
Mellis alikipiga kwenye kikosi cha Chelsea kwa mara ya kwanza kwenye Michuano ya Klabu bingwa Ulaya msimu uliopita, lakini ameelezwa kuwa hahitajiki klabuni hapo katika kikao cha nidhamu kilichoketi hivi karibuni.
Mchezaji mwenzake, Billy Clifford yeye alinusurika lakini akatozwa faini baada ya kukiri kupeleka mafataki hayo kwenye uwanja wa mazoezi.

No comments: