Kampuni ya Food Safety and Quality Consultancy imeandaa
makongamano kwa ajili ya kuwajengea uwezo wajasiriamali wadogo na wa kati
waweze kuyafikia masoko bora ya kimataifa.
Ofisa Mtendaji wa kampuni hiyo, Paul Seni alisema hayo
jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa.
Alisema makongamano hayo yatafanyika Mwanza, Agosti 25 na
26 na jijini Dar es Salaam Agosti 28 na 29 mwaka huu.
Alisema kampuni hiyo iliyosajiliwa na Serikali mwaka
2013, ilianzishwa kwa lengo la kuwashirikisha wajasiriamali wa Tanzania waweze kuzalisha bidhaa bora kuhimili
ushindani wa masoko na kuongeza kipato chao kwa kutumia fursa zinazowazunguka
ndani na nje ya nchi.
Seni alisema mafunzo hayo yatahimiza ubora wa vyakula
kuanzia utayarishaji shamba, matumizi mazuri ya virutubishi bora kama mbolea,
viuagugu, viuatilifu, viua dudu na namna ya kuondoa visumbufu vinavyoharibu
ubora wa mazao shambani, ghalani, katika usindikaji na uhifadhi bora wa mazao.
Pia kampuni hii inajenga uwezo kwa wajasiriamali
wanaomiliki biashara ya vyakula kwa wenye mahoteli, migahawa au wasindikaji
hafifu wa vyakula kuongeza ubora na kuondoa magonjwa yanayoletwa na
utayarishaji hafifu wa vyakula.
No comments:
Post a Comment