UKAWA WATAKA CAG KUKAGUA MATUMIZI BUNGE MAALUMU LA KATIBA

Wajumbe wa Bunge Maalamu la Katiba, kutoka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), limemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalumu kwenye matumizi ya fedha za bunge hilo, ili kubaini ufujaji wa fedha usio halali.
Tamko hilo lilitolewa jijini Dar es Salaam jana na viongozi wa Ukawa wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu nia yao, ikiwa ni mkakati wao wa kutaka pia Rais Jakaya Kikwete asitishe shughuli za bunge hilo, kwa madai linavuruga mchakato wa kupata Katiba mpya.
Viongozi hao ni pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba, Mwenyekiti wa Nccr-Mageuzi, James Mbatia na Katibu Mkuu wa Chadema, Wilbrod Slaa.
Akizungumzia hilo, Mbatia alisema sio sahihi bunge hilo kuendelea na vikao vyake mjini Dodoma ili hali kundi jingine liko nje kutokana na hitilafu ya mchakato mzima wa rasimu ya Katiba, na kwamba kufanya hivyo ni kuendelea kutumia fedha za umma pasipo manufaa mwishowe.
“Tumeshangazwa na kitendo cha CCM kuendelea kulazimisha bunge maalamu Katiba, tena kwa mtindo wa kupuuza maoni ya wananchi yaliyomo kwenye Rasimu ya pili ya Katiba, tunataka, rais asitishe bunge hilo na CAG, afanye uchunguzi wa matumizi ya fedha”, alisema Mbatia.
Alisema pamoja na mkaguzi huyo kufanya ukaguzi wa fedha kuanzia bunge hilo lililopita, pia wanamtaka rais asitishe shughuli za bunge hilo,ili lisiendelee kufuja fedha za Watanzania.
Alisema ikiwa rais hatafanya hivyo, watawaongoza wananchi kufanya maandamano na mikutano ya hadara nchi nzima kupinga jambo hilo, kwa madai kuwa halitekelezi matakwa ya wananchi wengi.
“Iwapo rais atashindwa kutumia mamlaka yake kusitisha bunge hilo, tutafanya maandamano nchi nzima kuwaongoza watanzania kupaza sauti zao kupinga jambo hilo,” alisema Mbatia.
Kwa upande wake, Lipumba alisema hawako tayari kuona ubadhirifu ukiendelea ndani ya bunge hilo ambalo, hali sio shwari kutokana na kutokuwepo na maridhiano baina ya Ukawa na wajumbe wengine, hali inayofanya mchakato mzima wa katiba kukosa uwakilishi sawa wa wananchi.
Awali, Ukawa walitoka nje ya Bunge Aprili 16, mwaka huu wakati bunge hilo likiendelea kujadili maoni ya rasimu ya katiba, kwa madai kuwa rasimu inayojadiliwa siyo iliyopendekezwa na Tume.

No comments: