MTENDAJI KORTINI KWA UJANGILI

Watu wawili wanaosadikiwa kuwa ni majangili,  akiwemo mtendaji wa Kijiji cha Kikwazo kilichopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kujibu mashitaka mawili ya uhujumu uchumi.
Watuhumiwa hao walikutwa na ngozi 10 za  chui na mbili za mnyama aina ya mondo zote zikiwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 59.
Waliofikishwa mahakamani  ni pamoja na Mtendaji wa Kijiji, Juma Salimu(41) na Juma Bakari Ramadhani (25), wote wakazi wa kijiji hicho kilichopo wilayani Bagamoyo katika Mkoa wa Pwani.
Akiwasomea mashitaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Arusha mbele ya Hakimu Dovote Msofe, Mwendesha Mashitaka wa Kikosi cha Kuzuia Ujangili nchini(KDU), Michael Msokwa ilidai katika mashitaka ya kwanza ni kupatikana na nyara za Serikali kinyume na sheria namba 86(11) b na c ya mwaka 2009 na kufanyiwa marekebisho katika kifungu namba 14 (d) cha mwaka 2002.
Msokwa alisoma mashitaka ya pili kuwa ni kujishughulisha na kufanya biashara ya nyara ya serikali kinyume na sheria namba 84 kifungu kidogo namba 1(2) na (5) cha mwaka 2009.
Mwendesha mashitaka huyo alidai mahakamani hapo kuwa wote kwa pamoja Julai 31 mwaka huu katika mji wa Mbwewe mkoani Tanga walikutwa na ngozi za chui 10 zenye thamani ya dola za Marekani 35,000 (Sh milioni 58) na mbili za mnyama aina ya mondo zenye thamani ya dola za Marekani 600 (Sh 997,512).
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, Hakimu Msofe aliwaambia washitakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na walienda rumande hadi Agosti 21 mwaka huu, kesi yao itakapotajwa tena.

No comments: