MBUNGE WA CHADEMA 'AMCHANACHANA' TUNDU LISSU

Siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza uwezekano wa kuwachukulia hatua wabunge wa chama hicho wanaokiuka msimamo wao wa kususa vikao vinavyoendelea vya Bunge Maalumu la Katiba, Mbunge wa Mpanda Kati, Said Arfi (Chadema) amehoji uhalali wa Chadema kuendelea kumbana.
Amemtaka Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kuacha kuwadanganya Watanzania juu ya mchakato huo na kwamba, kama angekuwa na nia njema angeshauri waende mahakamani kusimamisha Bunge ili kupata tafsiri ya sheria na si kutoka nje.
Kauli ya Arfi aliyoitoa jana, imekuja baada ya Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki kukaririwa na vyombo vya habari akisema wasaliti wa Ukawa wajiandae kuwa wabunge wa mahakama, akimaanisha kutengwa na chama hicho.
Arfi aliyeachia ngazi nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Taifa mwishoni mwa mwaka jana, alisema ameshangazwa na kauli ya Lissu na kuhoji uhalali alionao katika kumbana.
“Napenda kumkumbusha Lissu kama anapenda kusema, akili yake isiwe ya kusahau. Ni hatari kwa kiongozi na wala hataepuka kuitwa mropokaji …naomba arejee kauli yake iliyoandikwa pia na gazeti la (analitaja) la tarehe 27.06.2014, nanukuu  "...kutoruhusiwa kushiriki shughuli za kambi hiyo..."
“Sasa Lissu anapata wapi uhalali wa kuhoji matendo na maamuzi yangu wakati wamenitenga kinyume na kanuni za kambi rasmi? Hivi Lissu ni nani..? Angewaachia wengine walisemee, si Lissu,” alihoji Arfi.
Aliongeza kuwa, kukaa kwake kimya si ujinga bali ni busara, lakini si kwa kila jambo na kwamba Lissu anapolazimisha kutoshiriki kwenye bunge hilo hadi hapo uongozi wa bunge hilo utoe ufafanuzi wa kifungu cha 25, cha sheria ya mchakato wa Katiba sura ya 83, anajidanganya na kuwadanganya Watanzania.
Alisisitiza kuwa kazi ya Bunge ni kutunga Sheria na chombo cha Kikatiba cha kutafsiri sheria ni Mahakama na kwamba angemuelewa  Lissu kama Mwanasheria, angewashauri kwenda mahakamani kusimamisha Bunge hilo, ili  kupata tafsiri ya sheria na sio kushawishi kutoka nje ya bunge.
Wajumbe wa Ukawa wanaotokana na vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, wameendelea kuwa nje ya Bunge Maalumu la Katiba lililoanza awamu ya pili ya vikao vyake hivi karibuni, vikishikilia msimamo uliowatoa bungeni Aprili 16 mwaka huu, kwa madai ya hoja za wajumbe wa upinzani `kutopewa’ uzito na kudharauliwa.
Awali mwishoni mwa wiki hii, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Slaam na kusema hatua kali zitachukuliwa na chama hicho, ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kwenye chama wasaliti wote wa Ukawa.
Alisema kamati hiyo haitachezewa na wala haipendi wakaidi, hivyo muda utakapofika watafanya uamuzi dhidi ya wasaliti hao.
Wabunge watatu wa Chadema, John Shibuda,  Mbunge wa Viti Maalumu Leticia Nyerere na Arfi wanadaiwa kukisaliti chama hicho kwa kujisajili na kusaini posho zao kwenye Bunge la Katiba linaloendelea hivi sasa mjini Dodoma, wakati makubaliano ya Ukawa ni kutorejea bungeni  hadi madai yao yatakapotekelezwa.
Akizungumza na wanahabari juzi, Lissu alisema ,”Hatutarajii kumuogopa yeyote awe Shibuda, Nyerere au Arfi, tunajua hawa wote wako Dodoma na wamesaini posho, hivyo watatueleza wakati utakapofika, ni bora wawe wabunge wa mahakama kuliko kuendeleza usaliti ndani ya chama,” alisema Lissu.

No comments: