MAOFISA HABARI WATAKIWA KUTOA ELIMU KUHUSU DART



Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) umetaka maofisa habari na  mawasiliano wa taasisi zinazoguswa moja kwa moja na mradi huo, kusaidia kutoa elimu na taarifa sahihi kwa wananchi juu ya uendeshaji na usimamizi wake. 
Mkurugenzi wa Utawala, Rasilimali Watu na Mawasiliano wa Dart,  Evodius  Katare, alisema  maofisa habari na mawasiliano ni nguzo muhimu katika utoaji wa taarifa za mradi wananchi waweze kuuelewa.
“Sisi kama Dart tunaamini kuwa maofisa habari na mawasiliano wa taasisi zote zinazoguswa na mradi huu wakiuelewa vizuri na kubadilishana taarifa itasaidia sana kuelimisha wananchi na kuwajengea uelewa mkubwa,” alisisitiza Katare.
Alikuwa akizungumza na maofisa wa habari na mawasiliano kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Usafirishaji wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), Wakala wa Barabara  nchini (Tanroads) na wa Wizara ya Ujenzi.
Maofisa wengine ni kutoka Kampuni ya Strabag, SMEC, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na  Manispaa za Ilala, Kinondoni na Temeke.
Mkurugenzi huyo alitaka maofisa hao kuwa kitu kimoja na kukutana kila wakati kuzungumzia maendeleo ya mradi.
“Ninyi ni wadau wakubwa wa mradi na hivyo mnapaswa kujua kila hatua ya maendeleo ya mradi ili muweze kuwafahamisha wananchi na kwa maana hiyo ni vyema mkaandaa utaratibu ambao utawawezesha kukutana mara nyingi,” alisisitiza. 
Meneja wa Mawasiliano wa Sumatra, David Mziray alisema, “Mkutano huu na kukutana kwetu mara kwa mara ni muhimu sana kwetu, kwani itatujengea uwezo na kuuelewa mradi.
Kwa upande wake, msemaji kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam,  Gaston Makwembe  alipongeza Dart kwa kuandaa mkutano na maofisa habari na mawasiliano hao na kuweka utaratibu wa kukutana mara kwa mara na kujengea uwezo wa kuuelewa mradi. 

No comments: