MAKANISA YAOMBA KUIOMBEA NCHI AMANI

Makanisa nchini yametakiwa kuendeleza amani iliyopo kwa kufanya maombi ya kuliombea Taifa ,ili amani iliyopo isivurugwe na baadhi ya watu wachache wasioitakia mema nchi hii.
Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na Ofisa Tarafa ya Kibaha, Anatory Mhango, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza, wakati wa kuhitimisha siku 40 za kufunga kwa ajili ya kuliombea Taifa zilizoandaliwa na Baraza la Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste mkoani Pwani.
Mhango alisema kuwa madhehebu ya dini ni moja ya sehemu muhimu za kudumisha amani ya nchi kwa taifa lolote, kwani wao ndiyo wanaowaelekeza waumini kumheshimu Mungu pamoja na mamlaka zilizopo.
“Madhehebu ya dini ndiyo sehemu ya kuwafanya watu waweze kudumisha amani, kwa kuepuka maovu yanayokatazwa ndani ya jamii ambayo mengi yamekuwa yakipelekea kuvunjika kwa amani,” alisema Mhango.
Alisema amani ndiyo msingi imara unaowaunganisha Watanzania pamoja na nchi jirani, Afrika na dunia nzima ambapo imekuwa ni mfano wa kuigwa na mataifa mengine.
“Nawapongezeni kwa kuweza kufunga siku 40 kwa ajili ya kuliombea Taifa ili liendelee kudumisha amani iliyopo, mmeonesha mfano mzuri ambao unapaswa kuigwa na madhehebu mengine hapa nchini na Watanzania wote hata mmoja mmoja kwa imani yake,” alisema Mhango.
Aidha aliwaomba Watanzania wote waendelee kufanya maombi kama hayo ili nchi iendelee kuwa na amani ambayo imedumu kwa kipindi kirefu tangu nchi ilipopata uhuru zaidi ya miaka 50 iliyopita.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa baraza hilo, Askofu Nasania Amos alisema kuwa lengo la kuwa na baraza hilo ni kuyaunganisha makanisa hayo ili kuwa na ushirikiano kwa ajili ya kutoa huduma za kiroho na kijamii.
Alisema waliamua kufunga ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kudumisha amani na kumfanya shetani asiwe na nguvu ya kupandikiza roho ya uvunjifu wa amani.

No comments: