WANASIASA WANAOGEUZA SUALA LA GESI KUWA MTAJI WAONYWA...

Wakazi wa Msimbati, Mtwara wakishiriki maandamano hivi karibuni kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam.
Kilio cha gesi kubaki mkoani hapa kimezidi kuibua maoni, safari hii Mwenyekiti wa zamani wa CCM wa Mkoa, Alhaji Dadi Mbulu akionya wanaoigeuza gesi kuwa suala la kisiasa kuacha kuchonganisha wana Mtwara na Rais Jakaya Kikwete.
Alisema mengi yanayozungumzwa yanapotoshwa, hivyo kuwapo mtazamo tofauti, kwamba Mtwara wamekataa gesi kusafirishwa kwenda sehemu nyingine ya nchi.
Mbulu alisema hayo juzi katika mkutano wa mashekhe na waumini wa dini ya Kiislamu kutoka wilaya zote za Mkoa wa Mtwara, waliokutana kwenye viwanja vya Mashujaa, mjini hapa kujadili suala la gesi. Mkutano huo ulitangulizwa kwa dua ya zaidi ya dakika 45 na baadaye mkutano wa zaidi ya saa tano.
Akizungumza baada ya kupata nafasi ya kuchangia hoja, Mbulu aliunga mkono wazo la kutaka gesi ghafi isisafirishwe, bali ichakatwe kwanza ndipo isafirishwe.
“Naomba mnaompelekea taarifa Rais wetu msimpotoshe jamani, maana kadri ninavyomsikia akizungumzia suala hili, haoneshi kama anajibu hoja zetu…sisi hatusemi gesi isiondoke au isinufaishe Watanzania wengine.
“Tunachosema ni kwamba ichakatwe hapa ndipo iende huko kwingine, na kama ni umeme sawa, lakini uzalishwe hapa…tueleweni jamani msimpotoshe Rais wetu…mnamgombanisha na wana Mtwara,” alisema.
Awali, akisoma tamko la Shura ya Maimamu wa Mkoa wa Mtwara, Ustaadhi Mohammed Salum alisema Waislamu wameamua kuungana na wananchi wa Mtwara, kutaka mitambo ya kuchakata na kufua umeme ifungwe Mtwara, kisha gesi na umeme isafirishwe kokote nchini. Alifafanua, kuwa ombi lao ni la kiroho zaidi badala ya kisiasa kama inavyohisiwa na wengi.
Kabla ya tamko hilo, Waislamu walifunga siku saba mfululizo tangu Ijumaa wiki jana huku wakisoma kunuti (dua maalumu) ya kumwomba Mwenyezi Mungu mafanikio katika kusudio lao la kupinga gesi kwenda Dar es Salaam, dua iliyohitimishwa uwanjani hapo.
Sheikh Jamadini Mchamwi aliitaka Serikali kufikiria upya uamuzi wake badala ya kuibua mvutano.
“Mimi sidhani Serikali itatupeleka huko wanakotaka tufike…hatutafuti mshindi hapa, ni vema Serikali ikanusuru giza lililopo mbele…ikubali hasara ya hizo Sh trilioni tatu, tumepata hasara matrilioni mangapi, sembuse hizi? “Naomba sana viongozi wetu wasimpe shetani nafasi…tuwaombee dua viongozi wetu wazidi kujazwa busara katika hili,” alisema.
Mkutano wa mashekhe na waumini wa dini ya Kiislamu, umekuja wiki moja baada ya waumini wa Kikristo wa madhehebu ya Kilutheri (KKKT) na Anglikana, Dayosisi ya Newala kutoa tamko la kupinga gesi asilia inayovunwa kijiji cha Msimbati, kupelekwa Dar es Salaam.
Askofu Mteule wa KKKT, Kanda ya Kusini Mashariki, Mchungaji Lucas Mbegule na Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Newala, Oscar Mnung’a walisisitiza umuhimu wa Serikali kusikiliza kwanza hoja za wana Mtwara kabla ya kuanza kutekeleza mradi huo.

No comments: