WANAKWAYA WALIA KUTAPELIWA FEDHA ZAO ZA HARAMBEE...

Aggrey Mwanri.
Mgogoro mwingine ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mjini Kati umeibuka mbali na wa deni la Sh bilioni 11 ambapo safari hii, waumini wanadai fedha zilizochangwa katika harambee ambazo inadaiwa hazijulikani ziliko.
Harambee hizo zilifanyika mara tatu mwaka 2008 na mbili kati ya hizo, zilisimamiwa na mawaziri Aggrey Mwanry, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Lazaro Nyalandu wakati huo akiwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara.
Katika harambee hizo zaidi ya Sh milioni 90, zilichangwa kwa ajili ya kununua basi la Kwaya ya Uinjilisti ya Vijana wa Usharika huo.
Habari kutoka kwa baadhi ya waimbaji wa kwaya hiyo, zinadai kwamba fedha hizo zilikuwa za harambee tatu zilizofanyika jijini hapa mwaka 2008.
Vyanzo vya habari vilidai kuwa kiasi hicho cha fedha kilipatikana lakini katika hali ya kushangaza, hakikuwekwa katika akaunti ya kwaya kama lengo lilivyokusudiwa na haijulikani sehemu ya fedha hizo ziliko hata sasa.
Baada ya kutokea kwa hali hiyo, baadhi ya waimbaji walifanya mgomo wa wazi na kufikia hatua ya kususa kuimba katika moja ya ibada mpaka fedha zao zitakapojulikana ziliko.
Mtoa habari kutoka kwaya hiyo, alieleza kuwa baada ya shinikizo kuzidi, uongozi wa Usharika huo ulidai umenunua basi aina ya Isuzu Journey kwa Sh milioni 60 badala ya uongozi wa kwaya hiyo kufanya hivyo.
Hata hivyo, pamoja na basi hilo namba T 416 BUZ kudaiwa kununuliwa kwa fedha hizo, lilipowasili lilionekana dhahiri kuwa ni bovu, chakavu na lisilo na thamani ya fedha hizo.
“Sisi si watoto wa kudanganyiwa peremende. Ni watu wazima tunaoelewa kitu kipya na chakavu. Hata asiyeona anaweza kutambua kuwa lile basi ni chakavu na ndiyo maana tuligoma kulipokea,” alisema mmoja wa wanakwaya ambaye hakutaka jina lake litajwe. 
Basi hilo inadaiwa lilifikishwa katika Kanisa hilo bila ya shamrashamra kama ilivyozoeleka kwa vifaa vingine vya Kanisa ambavyo kwa kawaida,  hupokewa kwa mbwembwe nyingi zinazoambatana na ibada ya kuvibariki.
"Mwenyekiti wetu aliitwa asubuhi na kuambiwa atafute dereva ili aendeshe hilo basi likaoshwe, lakini cha kushangaza halikuwaka!
"Hivi basi jipya kutoka Japan linaweza kukataa kuwaka? Kwa nini lije usiku wa manane, hapa tumeuziwa mbuzi kwenye gunia, huu ni ufisadi wa fedha za wanakwaya,’’ alisema mtoa habari huyo.
Kutokana na utata huo ambao viongozi wa Usharika wamegoma kuutolea ufafanuzi, kwaya hiyo ya vijana ilikataa kupokea basi hilo na hadi sasa limeegeshwa eneo la Kanisa la Mjini Kati likiendelea kuchakaa kwa mwaka sasa.
Mwenyekiti wa Kwaya hiyo, Felix Mweta alipoulizwa juu ya suala hilo, alishindwa kukanusha wala kuthibitisha na kueleza kuwa suala la basi hilo liko uongozi wa juu wa Dayosisi.
‘’Siwezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa kwa kuwa mimi ni kiongozi, nilipeleka suala hilo kwa uongozi wa juu wa Dayosisi yetu ili lipatiwe ufumbuzi na kulizungumzia kwa sasa ni utovu wa nidhamu,’’ alisema Mweta.
Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, Israel ole Karyongi na Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Mjini Kati, Titus Laroya kwa nyakati tofauti hawakutaka kupokea simu wala kujibu ujumbe katika simu zao ili kutoa ufafanuzi wa suala hilo.
Sakata hilo ni mfululizo wa mgogoro unaoendelea ndani ya Kanisa hilo Dayosisi ya Kaskazini Kati ambako mali za Kanisa ziko hatarini kupigwa mnada kutokana na deni la Sh bilioni 11 baada ya kushindwa kurejesha mikopo ya benki.
Mkopo huo ulitumika kujenga vitega uchumi ikiwamo Hoteli ya Arusha Corridor Springs lakini sasa hivi imesababisha hali ya kifedha kuwa katika hali mbaya.

No comments: