WANAFUNZI IFM WAAMBULIA MABOMU WAKIDAI USALAMA WAO...

Baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) wakiwa wameamriwa na polisi kuchuchumaa baada ya kukamatwa kwa kosa la kuandamana bila kibali, Dar es Salaam jana.
Baadhi wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) jana waliandamana kupinga vitendo vya kuporwa, kulawitiwa na kubakwa wanavyofanyiwa wenzao wanaoishi Kigamboni.
Wanafunzi wanaodaiwa kufanyiwa vitendo hivyo ni waliokosa vyumba vya hosteli katika chuo hicho na kulazimika kutafuta hifadhi kwa kupanga vyumba Kigamboni.
Wakiwa njiani kwenda Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, wanafunzi hao walizuiwa na kutawanywa walipofika karibu na jengo la PPF Tower jijini Dar es Salaam baada ya kuelezwa kuwa maandamano yao hayakuwa halali.
Baada ya kutawanywa, wanafunzi hao walianza kuhamasishana  wajiunge pamoja kwenda Kigamboni kuwasaka watu wanaodaiwa kuwavamia na kuwafanyia uporaji na udhalilishaji na walipofika walianza kufanya vurugu wakidai kuwasaka
wanaotuhumiwa.
Kutokana na vurugu hizo,  askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walifika na kufyatua mabomu ya machozi kuwatawanya wanafunzi hao. 
Vurugu hizo zilisababisha wafanyabiashara katika eneo hilo kufunga shughuli zao wakihofia kuporwa mali zao na wahuni.
Mmoja wa wanafunzi aliyezungumza na mwandishi, Moses Ndile alidai wamechosha na  wizi na unyanyasaji unaofanywa kwa wenzao.
Ndile alidai Polisi tayari inayo taarifa  lakini hakuna hatua zilizochukuliwa huku akidai mbali na kubakwa na kulawitiwa, wamekuwa wakiporwa fedha, kompyuta za mkononi.
Hata hivyo,  Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alifika eneo la tukio na kuzungumza na   wanafunzi hao ambapo waliafikiana kuanza msako wa pamoja ili kuwatia mbaroni wote watuhumiwa wa matukio hayo.

No comments: