UONGOZI WA KKKT WAWAANGUKIA WACHUNGAJI...

Uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati umewapigia magoti wachungaji wa Dayosisi hiyo, ili washiriki kunusuru mali za Kanisa hilo zisipigwe mnada.
Mbali na kuwasihi kuokoa mali hizo, uongozi wa Dayosisi umelazimika kutumia mbinu mbalimbali kupunguza munkari wa wachungaji hao, ikiwamo kuahidi kurejeshwa kazini bila masharti kwa Mchungaji Philemon Mollel. 
Hatua hiyo ilijitokeza juzi katika kikao cha wachungaji hao kilichoitishwa mahsusi na uongozi wa Dayosisi, ili kujaribu kutuliza mgogoro unaoendelea chini kwa chini kati ya uongozi na washarika wa Kanisa hilo.
Kikao hicho kiliongozwa na Askofu Jacob ole Mameyo wa Dayosisi ya Morogoro, ambaye alitumia muda mwingi kubembeleza wachungaji hao wausaidie uongozi wa Dayosisi ya Kaskazini Kati.
Mmoja wa wachungaji waliohudhuria kikao hicho kilichofanyika Oldonyo Sambu, alimwambia mwandishi kuwa uongozi wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, ulilazimika kutumia mbinu kadhaa za  kubembeleza wachungaji.

No comments: