DK MWAKYEMBE, MAGUFULI, KAGASHEKI WATABIRIWA KUNG'ARA 2013...

KUTOKA KUSHOTO: Balozi Khamis Kagasheki, Dk John Magufuli na Dk Harrison Mwakyembe.
Mawaziri Dk Harrison Mwekyembe wa Uchukuzi, Dk John Magufuli wa Ujenzi na Balozi Khamis Kagasheki wa Maliasili na Utalii, wametabiriwa kung’ara kwa kuungwa mkono na wananchi wengi kwa mwaka 2013.
Utabiri huo umetangazwa jana na mtoto wa aliyekuwa bingwa wa Utabiri na Unajimu Afrika Mashariki na Kati, marehemu Shekhe Yahya Hussein, Hassan Hussein.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa baba yake Magomeni Dar es Salaam huku akiwa amekalia kiti alichokuwa akikalia Shekhe Yahya, Hussein alitabiri kuwa Rais Jakaya Kikwete ataungwa mkono kwa asilimia 100 na wananchi.
Akifafanua utabiri huo, Hussein alisema Rais Kikwete ataiunganisha nchi na kuwa moja yenye uimara wa utaifa kuliko watangulizi wake.
Alitabiri kuwa Rais Kikwete atashirikiana zaidi na wanasiasa na viongozi wa dini kuondoa mtikisiko wa uvunjifu wa amani uliokuwapo nchini mwaka jana.
Kuhusu akina Mwakyembe, Hussein ametabiri kwamba nyota za mawaziri hao kama zilivyong’ara mwaka uliopita, zinaonesha kuwa zitang’ara zaidi mwaka huu kutokana na utendaji wao wa kazi na kujikuta wakikubalika na wananchi wengi zaidi.
Mbali na utabiri kwa viongozi mmoja mmoja, katika masuala yanayoikabili nchi hasa sakata la baadhi ya wananchi mkoani Mtwara kupinga gesi asilia isisafirishwe kwenda mkoani Dar es Salaam, Hussein alitabiri kuwa sakata hilo litaisha kwa amani.
Alitabiri kuwa mbali na kumalizika kwa amani, pia wananchi wengi wataunga mkono matumizi ya gesi hiyo kwa faida zaidi ya taifa badala ya jimbo kwa jimbo.
Katika medani za siasa, ametabiri kwamba mwaka huu kwa kuwa ulianza siku ya Jumanne, matukio ya viongozi kutoa matamshi yenye utatanishi na kusababisha hofu kwa watu kupigana yatatokea, lakini watakaa pamoja na kukubaliana mambo baina yao na kurejesha hali ya amani.
“Matukio yote ninayotabiri yatatokea mwaka huu, utabiri unaonesha kuwa wabunge wengi wataungana katika masuala yatakayohusu utaifa bila kujali itikadi za vyama vyao, nyota zinaonesha kuna baadhi ya wabunge wataanguka bungeni wakati wa majadiliano,” alitabiri.
Pia ametabiri Rais ajaye atakuwa mwanamume na kupinga utabiri uliowahi kutolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kiislamu ya Imamu Bukhary, Shekhe Khalifa Khamis kuwa nchi itaongozwa na Rais mwanamke mara baada ya rais aliyepo madarakani kumaliza muda wake.
“Mwaka 2013 ulioanza Jumanne, umetawaliwa na sayari ya Mars yenye nyota za Punda na Ng'e ambapo nyota ya Punda ndiyo ya mwanzo ambayo ni  kichwa au nyumba ambayo maana  yake ni mwanzo wa jambo, anza jambo, tangaza jambo au kupata mafanikio.
“Pia nyota ya ng’e iliyopo nafasi ya nane kinyota, inaashiria hasira, kupotea, kuachana, kukimbiwa, maziko, vifo na wasiwasi ambapo kwa kawaida Mwaka ukianzia Jumanne unaashira mambo mengi ikiwemo vita sehemu mbalimbali duniani, maradhi na vifo,” alisema Hussein.
Kuhusu uchaguzi wa Kenya unaotarajiwa kufanyika Machi mwaka huu, mtabiri huyo ametabiri kuwa muungano unaongozwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Raila Odinga utawashinda wapinzani wake akiwemo Uhuru Kenyatta na William Ruto. Uchaguzi huo utafanyika katika hali ya amani na utulivu.

No comments: