DK MWAKYEMBE AVUNJA UKIMYA RELI YA KIGALI...

Dk Harrison Mwakyembe.
Waziri wa Uchukuzi, Dk  Harrison Mwakyembe amesema kuwa wanasubiri ripoti ya mtaalamu mwelekezi ili waanze uendelezaji na uboreshaji wa reli ya pamoja itakayounganisha nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi.
Aidha alisema kukamilika kwa ripoti hiyo ndipo kutaonesha ni kiasi gani cha fedha kinahitajika ili kufanya kazi kitaalamu na pia kuonesha maeneo gani yamependekezwa reli hiyo ipite hasa katika eneo ambalo halikuwa na reli.
Akizungumza na waandishi wa habari jana  Dar es Salaam, baada ya kufungua mkutano uliowashirikisha wataalamu na mawaziri wa Uchukuzi kutoka nchi hizo, Dk  Mwakyembe alisema kuwa reli hiyo itajengwa kutoka Dar es Salaam-Isaka na kutoka Isaka- Kigali Keza na kupita Gitega kwenda Musongati.
Alisema kwa sasa reli iliyopo ni nyembamba hivyo wataiboresha ili iwe pana na kuna maeneo mengine ambayo ni mapya reli hiyo haikupita watajenga upya ili kuunganisha nchi hizo kibiashara.
Alisema kuwa tangu mtaalamu huyo aanze kazi ni mwaka wa pili sasa na anatarajiwa kukamilisha kazi yake Machi mwaka huu ambapo kila nchi itabeba gharama zake ingawa ukopaji utakuwa wa pamoja.
Kwa upande wao Uchukuzi wa Burundi, Moise Bucumi na Waziri wa Uchukuzi wa Rwanda, Alexis Nzahabwanimana walisema kuwa kukamilika kwa reli hiyo kutasaidia kukua maendeleo ya biashara katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na nchi za jirani.

No comments: