WASOMI WAPINGA UDHIBITI WA ADA SHULE ZA BINAFSI...

Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere wakifuatilia hoja mbalimbali.
Baadhi ya wasomi wamepinga mpango wa Serikali wa kutaka kuweka udhibiti wa ada kwa shule za sekondari za binafsi, kwa maelezo kuwa kufanya hivyo ni kurudisha nyuma juhudi za sekta binafsi kusaidia utoaji wa elimu nchini.
Lakini pia baadhi ya wasomi hao, wameonya Serikali isijifariji kuwa tatizo la walimu linaweza kumalizika mwaka 2015, kwani wanafunzi wengi wanaosomea shahada ya ualimu wanafanya hivyo ili iwe rahisi kupata mkopo wa Serikali, lakini hawana mapenzi ya kwenda kufundisha.
Badala yake wasomi hao wanaoshiriki Kongamano la Uchumi na Maendeleo lililoandaliwa na Kigoda cha Mwalimu Nyerere cha Maendeleo kwa kushirikiana na Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wameshauri Serikali ifanye juhudi za kuboresha shule zake ili zitoe elimu sawa na ile inayotolewa na shule binafsi.
Walikuwa wanachangia katika mada iliyotolewa na Dk Godius Kahyarara na Dk Luke Kirama juu ya mikakati ya utoaji wa elimu inayoendana na kukua kwa ujuzi kwa kuzingatia ubora, kiwango, gharama na maendeleo kwenye sekta hiyo.
Profesa Gelase Mutahaba alisema Serikali itafanya kosa kubwa kama itaamua kuunda chombo cha kudhibiti ada katika shule binafsi, kwani mfumo huo umepitwa na wakati na sasa soko huru ndilo linafanya kazi.
Alishauri inachotakiwa Serikali ni kuunda chombo ambacho kitaweka viwango vya ufundishaji, mitaala, kiwango cha elimu cha walimu na masomo yanayofundishwa katika shule hizo na ikiwezekana wawe wanapeleka wakaguzi kwenye shule hizo binafsi kuona kama mambo hayo yanazingatiwa.
“Hili ni soko huru sio umlazimishe mtu kupanga ada, Serikali iishie kwenye kudhibiti kiwango cha elimu, suala la ada sio lao,” alisema Profesa Mutahaba na kuonya kuwa iwapo Serikali itaweka udhibiti wa ada, vitendo vya rushwa katika shule hizo itakuwa ni kubwa.
Naye Dk Johovaness Aikaeli alisema mpango wa kudhibiti ada katika shule binafsi halitasaidia uboreshaji wa elimu nchini badala yake akataka Serikali ijikite zaidi kuboresha kiwango cha elimu katika shule zake.
"Serikali ijipange iboreshe elimu katika shule zake ifanane na ile inayotolewa kwenye shule binafsi lakini sio kuja na mpango ambao utekelezaji wake pia ni mgumu," alisema Dk Aikaeli.
Katika mada iliyowasilishwa kwenye kongamano hilo, Dk Kahyarara alisema kwa Tanzania, mzazi anayesomesha mtoto sekondari ya Serikali analipa kidogo kuliko yule anayesomesha mtoto sekondari binafsi.
Alisema katika sekondari binafsi gharama halisi za uendeshaji ni dola 2000 (Sh milioni 3.6), lakini ada katika shule hizo wakati mwingine inaweza kuwa zaidi ya kiasi hicho au mara mbili ya fedha hizo.
“Hakuna uwiano unaolingana katika utozaji wa ada, kila shule inajipangia kutokana na mahitaji ya shule husika au ukubali wa wazazi ambao wako tayari kulipa kiasi hicho,” alisema Dk Kahyarara.
Kwa upande wake, Dk Josephat Kweka alipendekeza kuwa ni lazima Serikali iwe na chombo ambacho kitadhibiti upandaji wa ada katika shule hizo binafsi, kwa maelezo kuwa huwezi kuwa mchezaji mpira na papo hapo unakuwa refarii.
Kuhusu elimu ya vyuo vikuu, mada ya Dk Kahyarara ilisema Serikali imekua, vyuo binafsi vimesaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya  juu lakini akaonya kuwa utoaji wa elimu katika taasisi hizo  haujakidhi mahitaji ya waajiri.
Alisema waajiri wengi wanalalamika ujuzi wa wahitimu wengi wa vyuo vikuu uko chini kwani wanachofundishwa katika vyuo hivyo haukidhi mahitaji ya waajiri. Moja ya eneo alilolalamikia ni mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa kozi zinazofundishwa kwenye vyuo vingi hazikidhi mahitaji ya mifuko hiyo.
Hali hiyo imefanya wahitimu wengi nchini kupata ushindani mkubwa na wahitimu kutoka Marekani, Uingereza na baadhi ya shahada za Kenya, India na Afrika Kusini, lakini akashauri kuwa kuna haja ya vyuo vya nchini kufanya utafiti kubaini mahitaji ya soko na ikiwezekana kubadilisha mitaala yake.
"Baadhi ya wahitimu wa shahada ya kwanza kutoka vyuo vyetu ni wazuri ukilinganisha na hao wanaosoma nje ila tatizo linakuwa kwenye lugha, kutojiamini, kutokuwa wabunifu na kushindwa kumudu namna ya kuwa na ujuzi na kompyuta pamoja na lugha ya kibiashara," alisema msomi huyo.
Baadhi ya wachangiaji walishauri kuwa kama wahitimu hawakidhi mahitaji ya soko ni vyema mitaala ibadilishwe ili iweze kuendana na wakati. “Kama miaka mitano tunashindwa kukidhi mahitaji ya soko, tutambue kuwa tuna tatizo, tubadilishe hali hii,” alisema.
Kuhusu walimu, wachangiaji kadhaa walionya kuwa kutokana na fani ya ualimu kutopewa kipaumbele na Serikali, wanafunzi wengi wanaosomea fani hiyo, wanafanya hivyo ili iwawie rahisi kupata mkopo.
Walidai wakishamaliza wanaenda kufanya kazi nyingine au wanaenda kusoma shahada zingine za uzamili ili waachane na kazi hiyo. Hivyo walishauri Serikali iipe kipaumbele fani hiyo katika masuala ya malipo.
Lakini Aisha Mohamed ambaye anasomea ualimu alisema "napenda kupinga hoja za watu zilizotolewa hapa kuwa tunasomea ualimu ili ituwie rahisi kupata mikopo, mimi nina wito na simo kwenye kundi hilo," alisema.
Walitaka ili kuboresha elimu ya msingi na sekondari Serikali iachane na tabia ya kuwapeleka wanafunzi waliofeli kwenye vyuo vya ualimu kwani kufanya hivyo ndiko kunazidi kudidimiza elimu ya hapa nchini.
Wengine walishauri kuwa ili masomo ya sayansi yaweze kupendwa na wanafunzi ni vyema masomo hayo yakafundishwa kuanzia darasa la kwanza na yawe ni lazima kwa mwanafunzi kuyasoma.

No comments: