MADAKTARI 372 WALIOSHIRIKI MGOMO WAITWA KUHOJIWA...

Baadhi ya madaktari na wauguzi wakiwa nje ya maeneo yao ya kazi wakati wa mgomo.
Madaktari 372 waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo,  waliosimamishwa baada ya kushiriki katika mgomo wa madaktari mapema mwaka huu, wameanza kuitwa na kuhojiwa uhusika wa kila mmoja katika mgomo huo.
Taarifa zilizofikia gazeti hili wiki hii, zimeeleza kuwa madaktari hao wameitwa kuhojiwa katika Wizara ya Afya na Jamii kuanzia Desemba 6; na mahojiano yanatarajiwa kukamilika kesho.
Mtoa habari kutoka miongoni mwa madaktari hao, alisema kwamba waliitwa kwa kutumiwa ujumbe mfupi wa simu, kupigiwa simu na wengine walitumiwa barua pepe.
Kwa walio mikoani walitakiwa kuripoti Dar es Salaam kwa mahojiano hayo na asiyefika, adhabu yake kwa mujibu wa mtoa taarifa ni kujifukuzisha mwenyewe.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, jopo la wataalamu wa Serikali wanaoshiriki kuwahoji madaktari hao ni wanasheria wa Serikali  na wizara na wamekuwa wakifanya kazi mpaka mwishoni mwa wiki.
Mtoa habari huyo alibainisha kuwa baada ya mahojiano, wanasheria hao wamekuwa wakitoa adhabu papo hapo na mpaka sasa baadhi ya madaktari hao wamepewa onyo, onyo kali, kusimamishwa miezi miwili, minne au sita huku wengine wakifukuzwa kabisa na kuharibu fani yao ya udaktari.
Imeelezwa kuwa waliofukuzwa chuoni mpaka sasa ni wachache, kutokana na wengi wao kutotaka kuzungumzia suala hilo huku wengine wakichanganyikiwa, kutokana na uamuzi uliochukuliwa dhidi yao.
Pamoja na mazingira hayo, madaktari hao wamelalamikia jopo hilo la wanasheria, kwa kuwalazimisha kukubali makosa ili suala hilo liishe.
Pia wamelalamika kuwa wenzao wengi mikoani, hawakupata taarifa na hawajafika na kusababisha wawe hatarini kufukuzwa.
“Suala hili la kutuhoji limekuwa siri,” alisema mtoa habari wetu na kuhoji; “kama awali walipotusimamisha walitangaza, kwa nini sasa wamefanya siri kutuma ujumbe mfupi wa simu na siyo kutangaza kwenye vyombo vya habari?
“Lakini pia adhabu waliyotoa si haki, kama mimi wamenisimamisha miezi miwili na nimeshakaa miezi sita jumla ni miezi nane,” alihoji mmoja wa madaktari jina limehifadhiwa.
Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Donan Mmbando, alikiri madaktari hao kuhojiwa na watamaliza mwishoni mwa wiki hii.
Pia, alibainisha kuwa wiki hii wanahoji madaktari kutoka Kanda ya Dar es Salaam.
Alithibitisha pia kuwa baada ya kuwahoji madaktari hao mmoja baada ya mwingine, wametoa hukumu kulingana na kosa alilofanya. Hata hivyo, alikataa kutamka adhabu gani kwa madai kuwa hukumu ni siri.
Katika mgomo wao wa mwaka huu, madaktari walikuwa wakitaka walipwe mshahara wa kuanzia Sh milioni 3.5 na posho kadhaa.
Kwa mujibu wa madai hayo ya mshahara na posho, daktari anayeanza kazi alitakiwa kulipwa Sh milioni 7.7. Serikali ilikubali kupandisha baadhi ya posho na kukataa zingine na mshahara waliokuwa wakiudai.
Kutokana na gharama kubwa ya mshahara waliyokuwa wakihitaji, Serikali iliwataka madaktari kuacha kazi na kutafuta mwajiri mwingine mwenye uwezo huo.
Aidha, kwa madaktari waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo, Rais Jakaya Kikwete aliwaonya kuwa walikuwa wakihatarisha taaluma yao, kwa kuwa adhabu yao ni pamoja na kunyimwa kibali cha kufanya kazi hiyo waliyoisomea.
Hata hivyo, kutokana na ukaidi, uongozi wa hospitali za Muhimbili, KCMC,  Mbeya, Bugando, Amana, Temeke, St. Francis- Ifakara, Mwananyamala, Sekou Toure, Haydom na Dodoma walikokuwa wakifanya kazi, uliwaandikia barua madaktari waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo, kuwataka warudi kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Baada ya hapo, Katibu Mkuu alipeleka malalamiko Baraza la Madaktari Tanganyika, ambalo kwa kuzingatia masharti ya sheria kuhusu kupata usajili wa muda, lilisitisha usajili wao kuanzia Julai 11, mwaka huu.
Kutokana na uamuzi huo, madaktari hao walitakiwa kurejesha hati za usajili wa muda kwenye Ofisi ya Msajili wa Madaktari kabla ya Julai 17, 2012 na kurudi nyumbani mpaka walivyoanza kuitwa hivi karibuni.

No comments: