HATARI ZA WAZAZI KUWABUSU WATOTO WACHANGA ZAANIKWA...

Wataalamu wa afya nchini wametahadharisha wazazi kuwa macho na watu wanaobusu na kuwabeba watoto wao wachanga, wenye umri chini ya miaka mitano, kwa kuwa wanachangia kwa sehemu kubwa kuwaambukiza maradhi ikiwemo nimonia.
Wamehadharisha kuwa ikiwa wanataka kuwabusu na kuwabeba, basi wahakikishe wananawa mikono na uso hasa midomo kwa maji safi na sabuni, ili kupunguza vifo vya watoto 15,000 kwa mwaka vinavyotokana na ugonjwa huo nchini.
Kampeni hiyo za ‘kuzuia kubusu watoto’ imetajwa kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa nimonia na ule wa kuhara ambao chanjo zake mbili zilizinduliwa hivi karibuni na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete na zitaanza kutolewa rasmi nchi nzima Januari mwakani.
Ofisa Mfuatiliaji wa Magonjwa Yanayokingwa kwa Chanjo kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Daudi Manyanga alisema hayo jana alipotoa mada kuhusu nimonia katika semina ya waandishi wa habari.
Semina hiyo ilihusu chanjo mpya mbili; Pneumocaccal (PCV 13) ya nimonia na Rotarix ya kuzuia kuhara.
“Ugonjwa wa nimonia unasababishwa na vimelea vya Streptococcous pneumonia ambavyo huenezwa kwa njia ya hewa, lakini pia yanaambukizwa kwa njia ya kugusa sehemu zenye vimelea kama vile nguo, ngozi au kikombe. Hivyo ni hatari kwa wale wanao ‘mchumu’ mtoto,” alisema Dk Manyanga.
Alisema hatari hiyo inatokana na hali halisi kwamba ndugu, jamaa na marafiki wanapotembelea familia iliyojaliwa mtoto, humbeba na kuanza kumbusu bila kunawa mikono wala uhakika wa afya na hewa inayotoka mdomoni, hivyo ni rahisi kwa mtoto ambaye ngozi na kinga yake si kubwa sana, kuambukizwa nimonia.
Dk Manyanga akinukuu takiwmu za Shirika la Afya Duniani (WHO), hapa nchini kwamba watoto 15,206 kati ya wagonjwa 222,256 wanaougua nimonia kwa mwaka, hufa.
Alisema kisayansi, utafiti unaonesha kuwa kinga madhubuti ya nimonia pamoja na hiyo ya usafi, ni chanjo na kuwataka wazazi na walezi kupeleleka watoto kwenye chanjo Januari mwakani.
Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo, Dk Dafrossa Lyimo aliwaambia wanahabari katika semina hiyo ya siku moja kuwa pamoja na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha watoto hawafi kwa kuhara au nimonia inayoendelea, Serikali imedhamiria kupitia chanjo, kukomesha vifo na kufikia lengo namba 4 la milenia mwaka 2015.
Kwa mujibu wa Dk Lyimo, chanjo hizo mbili zitatolewa kwa awamu kulingana na aina ya chanjo ambapo ya kuzuia nimonia itatolewa mara tatu, mara ya kwanza mtoto akiwa na wiki sita, akiwa na wiki 10 na baadaye wiki 14. Ya kuhara itatolewa kwa awamu mbili, mtoto akiwa na wiki sita na baadaye wiki 10.
Nimonia ni ugonjwa wa pili hatari kwa kusababisha vifo vya watoto chini ya miaka mitano kwa asilimia 14 baada ya malaria inayoongoza kwa asilimia zaidi ya 15. Kuhara kunachangia kwa asilimia 13 ambapo asilimia kati ya 30 hadi 50 ya watoto wanaolazwa hospitali, husumbuliwa na kuhara.

No comments: