FAMILIA YAPONEA CHUPUCHUPU KUFA KWA UYOGA...

Uyoga.
Watu watatu wa familia moja katika Kijiji na Kata ya Katoro Wilaya ya Geita mkoani hapa, wamenusurika kufa baada ya kula uyoga unaosadikiwa kuwa na sumu.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 7 mchana ikiwa ni muda mfupi baada ya familia hiyo kumaliza kula chakula cha mchana.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Katoro, Aloyce Kamuli alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja watu waliokumbwa na mkasa huo kuwa ni Nusura Francis (11) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Lutozo, Rehema Francis (5) na Pili Sentole (38) ambaye ni mama wa familia hiyo.
Akielezea tukio hiyo jana, baba wa familia hiyo Francis Sentole (48) ambaye yeye alinusurika katika tukio hilo kutokana na kuwa safarini, alisema baada ya familia yake kumaliza kula chakula hicho walianza kusikia kizunguzungu na baadaye kutapika.
“Walipomaliza kula, mtoto mdogo wa miaka mitano (Rehema) alipatwa na kizunguzungu na kuanza kutapika, na wakati mama yake pamoja na majirani wakijiuliza la kufanya na mwingine naye alikumbwa na hali hiyo na kisha mama yao, walichukuliwa na kukimbizwa kwenye Kituo cha Afya cha Katoro…,’’ alisema baba wa familia hiyo.
Alisema baada ya kupata taarifa za tukio hilo alikimbia kwenye kituo cha afya ambako aliwakuta wakipatiwa matibabu, lakini katika mahojiano na mkewe alimweleza juu ya uyoga waliokuwa wamenunua na kuula mchana huo.
Alifafanua kuwa siku hiyo, alikwenda katika Soko la CCM mjini Katoro na kununua uyoga huo, alipofika nyumbani aliupika na kula yeye na familia yake, lakini baada ya muda mfupi walikumbwa na hali hiyo.
“Mara baada ya kumaliza kula chakula cha mchana walikaa takribani dakika 20 ndipo walipoanza kutapika mfululizo hali iliyosababisha miili yao kuishiwa nguvu na hata kupungukiwa maji mwilini na hivyo kulazimika kuomba msaada kwa majirani kabla ya kwenda kituo cha afya…,’’ alifafanua.
Naye Mganga Mfawidhi katika Kituo cha Afya cha Katoro, Alex Gatuku alithibitisha kuwapokea watu hao na kuwapatia huduma ya kiafya, kisha kuwaruhusu siku hiyo na kwamba hali zao kwa sasa zinaendelea vizuri.
Kwa mujibu wa mganga huyo majeruhi walipofikishwa katika kituo hicho cha afya walikuwa wakitapika na kuishiwa nguvu, hali iliyosababisha wahudumu kuanza kutoa huduma ya kwanza na kwamba hadi kufikia jana asubuhi hali zao zilikuwa zinaendelea vizuri na kwamba walikuwa wamerejeshwa nyumban
Hata hivyo, Mganga huyo  alitoa mwito kwa jamii kuwa makini na uyoga unaouzwa mitaani kwa kuwa watu wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakichuma uyoga wa aina yoyote porini na kwenda kuuza bila kujua una sumu ama la.

No comments: