MAMA ASUKA MPANGO BINTIYE ATEKWE KISHA ADAI FIDIA MABILIONI...

JUU: Jumba la Donovan ambapo Shannon alikutwa kafichwa. CHINI: Karen (kushoto), Shannon na Donovan (kulia).
Wanaharakati wanapiga kelele za kumsaka kwa udi na uvumba Karen Matthews kwenye kampeni ya kumtenga inayoendelea mitandaoni baada ya mama huyo kuachiwa kutoka gerezani wiki hii.
Tovuti zimesheheni meseji za vitisho dhidi ya mama huyo mwenye miaka 36 ambaye amebatizwa jina la ‘Mama Katili zaidi Uingereza’ baada ya kusuka mpango wa utekaji nyara binti yake Shannon ili adai fidia ya Pauni 50,000 za Uingereza.
Polisi wamekuwa wakifuatilia kwa karibu vitisho hivyo vya kutaka kulipiza kisasi kwenye tovuti kadhaa ikiwamo Twitter na Facebook dhidi ya Karen, ambaye inaaminika kuwa amejikondesha ili kubadili muonekano wake.
Ametumikia kifungo cha miaka nane tu jela.
Ujumbe mmoja kwenye Twitter umesomeka, “Nitampiga kwa furaha risasi ya kichwa kwa malipo kiduchu mno.”
Mwingine umesema, “Inasikitisha kuona watu kama Karen wanatarajia kuja kivingine – hakika wanastahili lolote baya kutoka kwa wanaharakati.”
Ujumbe mwingine ulisema, “Karen amehukumiwa miaka minane kwa kuruhusu binti yake atekwe ameachiwa baada ya miaka minne. Masihara gani haya kwa mfumo wetu wa Makosa ya Jinai.”
Kundi la watumiaji wa Facebook limeandika ujumbe unaosema, “Karen Matthews Akae Jela kwa Muda Mrefu.”
Mama huyo mwenye watoto saba aliachiwa kutoka gereza la Foston Hall, lililoko Derbyshire na kupelekwa sehemu ya mafichoni inayoaminika kuwa umbali wa maili karibu 30 kutoka nyumbani kwake Dewsbury Moor, West Yorkshire.
Karen sasa anaishi kwenye hosteli moja sehemu isiyofahamika, lakini maofisa wa polisi wanahofia kuwa inaweza kufahamika na kumfanya mama huyo kuwa katika hofu ya kushambuliwa na wanaharakati hao.
Amepunguza uzito na amekuwa akirembwa ikiwa ni pamoja na kubadili mtindo wa nywele kumwepusha asiweze kutambulika mitaani.
Vyanzo vya habari kutoka gerezani vimesema: “Amepungua uzito, hata hivyo amenyolewa nywele mtindo mwingine kiasi cha kuonekana kivingine tofauti na alivyoingia gerezani miaka mine iliyopita.”
Chanzo cha habari kimesema: “Kama maficho hayo ya Karen yatajulikana wiki chache zijazo na hatari dhidi yake kuongezeka, atalazimika kuhamishiwa sehemu nyingine.”
Karen, ambaye watoto wake wako chini ya uangalizi, ataendelea kuishi chini ya uangalizi maalumu kwa kipindi chote kilichobakia cha kifungo chake.
Katika kipindi chote hicho anatakiwa kufuata sheria kali ama atakabiliwa na adhabu ya kurudi gerezani.
Karen na mshirika wake, Michael Donovan mwenye miaka 44, waliwataka polisi kulipa Pauni milioni 3.2 wakati walipomteka Shannon kutoka nyumbani kwao.
Karen huku akilia kwenye televisheni alimwomba mtu aliyemteka binti yake amwachie huru na mamia ya wakazi wakajitolea kusaidia kumsaka binti huyo.
Shannon alipatikana siku 24 baadaye kwenye ghorofa analoishi Donovan umabli wa maili moja akiwa amelishwa madawa na kufichwa uvunguni mwa kitanda.
Donovan, ambaye pia alifungwa miaka minane jela, aliachiwa wiki iliyopita.

No comments: