MVUVI ASIMULIA ALIVYORUDI KUMUAGA RUBANI AJALI YA PRECISION AIR

Kijana mvuvi aliyeshiriki katika uokoaji wakati wa ajali ya ndege ya Precision Air  liyosababisha vifo vya watu 19 juzi mjini Bukoba, Majaliwa Jackson almaarufu  ajamnyama ameelezea namna alivyopambana kuvunja mlango wa ndege, kuokoa abiria hadi marubani.
Majaliwa ambaye katika harakati hizo naye alijeruhiwa na kupoteza fahamu na kuishia hospitali, alisema yeye ndiye aliyeona kwa mara ya kwanza na kushuhudia ndege hiyo ikizunguka mpaka ikitua kwenye maji.
Alisema wakati ajali inatokea alikuwa kwenye kazi yake ya kuvua dagaa na aliona ndege
ikizunguka lakini kilichomshtua ni ndege kutokea upande wa Kyaka wilayani Missenyi, wakati si kawaida.
“Na ilipokuja ikaenda moja kwa moja kama inataka kutua kisiwani Msila…nikasimama kuangalia hii show ikoje, nikaona inageuza kama inaenda bandarini, lakini nako ikageuza kwa mwendo wa taratibu ndipo rubani akaiweka ndani ya maji,” alieleza Majaliwa.
Alisema wakati tukio hilo linatokea kulikuwa na wavuvi wanatoka kuvua sato wakiwa na
mtumbwi mdogo na kuwashtua kuwa kuna ajali na wakiwa watatu wakasukuma mitumbwi yao hadi eneo la tukio.
“Tulipofika tukaona watu ndani ya ndege wanahangaika kufungua mlango. Mlango ulikuwa kama umejifunga… nikatumia kasia langu na kuuvunja kwa nguvu ukafunguka na watu wakaanza kutoka.
Mimi nikahamia upande wa pili wa rubani nikazama hadi nikamuona rubani akanielekeza nipasue kioo,” alisema mvuvi huyo.
Aliongeza: “Nikatoka nje ya maji nikaomba walinzi wa uwanja wa ndege waniletee kifaa cha kuvunjia wakaniletea vishoka, wakati naondoka mwanaume mmoja aliyekuwa na kipaza sauti akanikataza kuvunja kioo kwa sababu rubani anawasiliana nao kwenye simu na
maji aliko hayapo mengi.”
Alisema ikabidi arejee tena kuzamia hadi kwa rubani na kumpungia mkono wa ‘kwaheri’,
lakini alimwonesha mlango wa dharura akachukua kamba akiwa na wavuvi wenzake na kuifunga kwenye mlango huo ili wauvunje na kuokoa abiria.
Alisema kamba waliyotumia ilikuwa inavutika na walipoifunga wakati anamalizia ili wauvute mlango huo, bahati mbaya kamba ikavutika ikampiga usoni akapoteza fahamu na alipoamka alijikuta hospitalini.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamika, kutokana na tukio hilo kijana huyo alikimbizwa hospitalini na kuchanganywa na abiria waliopelekwa hospitalini hapo.
Tayari kijana huyo amepongezwa kwa ushujaa wake huo ikiwamo kupatiwa fedha na Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amtafutie nafasi kwenye Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili apate mafunzo zaidi ya uokoaji.

No comments: