MUFTI SIMBA KUZIKWA LEO JUMANNE SHINYANGA

Wakati mwili wa  Mufti na Shehe  Mkuu wa Tanzania, Issa Bin Shaaban Simba (78) aliyefariki dunia jana asubuhi ukitarajiwa kuzikwa leo jioni mkoani Shinyanga, Rais Jakaya Kikwete ameungana na Waislamu wote nchini na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania  (BAKWATA) kuomboleza kifo cha kiongozi huyo wa juu wa kiroho nchini.

Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya familia, Mufti aliyefikwa na mauti akiwa katika Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa sukari na shinikizo la damu, atazikwa leo kutokana  na wosia aliokuwa ameuacha kuwa, akiaga dunia mwili wake usiachwe muda mrefu bila kuzikwa.
Hata hivyo, taarifa kutoka Bakwata zinasema kwa upande wao wanatarajiwa kuuhifadhi mwili wa  Mufti kesho au keshokutwa, kwani alikuwa mtu wa watu hivyo kuna umuhimu wa kutoa fursa kwa wengi kutoa salamu zao za mwisho kwa mpendwa wao.
Mmoja wa watoto wa marehemu, Selemani Simba alisema mwili  utasafirishwa kwa ndege leo saa 3:00 asubuhi  kuelekea mkoani Shinyanga, ambako atazikwa katika eneo la Majengo.
“Hali yake ilibadilika siku ya Ijumaa ambapo tulimkimbiza Hospitali ya TMJ ambako baada ya kufanyiwa vipimo ikabainika mapafu yalikuwa yamejaa maji hivyo ilitakiwa afanyiwe upasuaji,” alisema.
Alisema baada ya kufanyiwa upasuaji huo juzi, madaktari waliagiza mgonjwa apewe muda wa kupumzika na asisumbuliwe, hivyo hakuweza kuzungumza na mtu yeyote hadi umauti ulipomfika jana saa 3:45 asubuhi.
Katika salamu zake za rambirambi, Rais Kikwete alisema; "Kifo kinaleta huzuni, hata hivyo kifo hakizuiliki, hatuna budi kukikubali na ni wajibu wetu kumuombea Shehe Mkuu kwa Mola wetu ampe mapumziko ya milele".
Rais Kikwete ametuma salamu hizo za rambirambi kupitia kwa Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum.
"Nawaombea subra wana familia, ndugu, jamaa, Waislamu wote na wana jamii kwani Mufti alikuwa kiongozi katika jamii yetu,” Rais alisema na kueleza kuwa, "Kamwe mchango wake hautasahaulika katika jamii yote kwa ujumla na hakika sote tutamkumbuka."
Mufti Simba alijiunga na BAKWATA mwaka 1968 na amekuwa mwalimu wa chuo katika mikoa mbalimbali ya Mwanza, Bukoba na mwaka 1970 alikuwa Shehe wa Mkoa wa Shinyanga.
Rais alimwelezea Mufti kama mwalimu katika jamii ambaye alikuwa na uzoefu wa hali ya juu na mwenye kupenda dini yake na kuitumia kwa manufaa ya jamii iliyomzunguka.
"Amekuwa mwalimu imara na mtu wa kutumainiwa na kutegemewa katika Uislamu na jamii kwa ujumla, hakika tutamkumbuka siku zote.”
Shehe Issa Bin Shaaban Simba alikuwa na uzoefu  mkubwa ndani ya Bakwata na  aliwahi kukaimu nafasi ya Mufti kwa siku 90, baada ya kifo cha Mufti Hemed mwaka 2002.
Baada ya hapo akasimamia mchakato wa uchaguzi wa Mufti Mkuu na baadaye 2003 akachaguliwa kuwa Mufti Mkuu wa Tanzania.
Kama ilivyokuwa kwa Rais Kikwete, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara naye ametuma salamu za rambirambi  Bakwata na kwa Waislamu wote nchini kutokana na kifo hicho.
Kwa mujibu wa taarifa yake jana, ni jambo la kusikitisha kumpoteza kiongozi huyo ambaye bado taifa lilikuwa likimhitaji, hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.
Alisema Mufti atakumbukwa kwa upole, unyenyekevu na kutopenda makuu wakati wa uhai wake ambapo alikuwa tayari kumsikiliza kila mtu bila kujali dini au kabila lake.

No comments: