MIGIRO, MWANAFUNZI WACHUKUA FOMU ZA URAIS

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro jana alichukua fomu ya kuwania Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, hivyo kufikisha idadi ya makada 36 wa chama hicho wanaowania urais, lakini pia akiwa mwanamke wa nne kuthubutu kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.

Mbali ya Dk Migiro, wengine waliochukua fomu ya kuwania urais jana ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe anayesomea Shahada ya Uzamili katika Utumishi wa Umma, Malick Malupu (34) na Joseph Chagama (45) ambaye ni kada wa chama hicho.
Dk Migiro ambaye alikuwa ameongozana na mumewe pamoja na mwanasiasa mkongwe nchini, na Mbunge wa viti maalum, Anna Abdallah, alisema CCM imetoa fursa kwa wanachama kujitokeza ili kupata ridhaa ya kuongoza kumtafuta kiongozi wa nchi.
Pia waliojitokeza watatoa fursa kwa wanawake vijana na wasichana kusimama mabegani mwao.
“Tunaishukuru CCM kwa kufanya wengi tujitokeze kwa kuweka mazingira ya kufanya wengi zaidi wajitokeze,” alisema kada huyo aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nchini, kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), nafasi aliyoitumikia hadi mwaka jana aliporejea nchini na kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Alisema wanaCCM wamejitokeza huku akiwataka wanachama wa CCM wengi zaidi kujitokeza kumdhamini.
Alipohojiwa nini vipaumbele vyake, alisema Ilani ya CCM ndiyo dira kwani hata ilani inayotengenezwa sasa imebeba maeneo mengi, kujenga msingi wa uchumi wa kisasa wa taifa linalojitegemea, sekta ya uzalishaji, miundombinu, mazingatio maalumu kuhusu muungano.
“Ilani itakuwa imefanya tathimini na kuweka mikakati ya kuendeleza yaliyofanyika.”
Alisema akipata ridhaa nyenzo yake itakuwa ni ilani ya CCM kwani hata taarifa ya Benki ya Dunia inaonesha  uchumi umekuwa ukikua kwa kiwango cha asilimia 6.4 hadi asilimia saba.
Alisema hali hiyo inaashiria kuna maendeleo, kukua kwa uchumi ni kiashiria cha jitihada za serikali.
Dk Migiro alisema ikipatikana fursa ya kuongoza atatumia ilani ya CCM kwani ni nyenzo kubwa katika kufikia maendeleo ya kweli; “Pamoja na ilani msingi utakuwa kuhakikisha manufaa ya mafanikio hayo yanafikia wananchi walio wengi, kazi iliyo mbele itakuwa ni kuhakikisha wananchi wengi wananufaika,” alisema.
Kwa upande mwingine, alitoa masikitiko yake kutokana na kifo ha Mufti wa Tanzania alitoa pole za dhati kwa Watanzania wote na kwa familia yake.
Alisema uwezo wa mtu kiutendaji haupimwi kwa umri japo ana umri wa miaka 34, bado anaona ana nafasi ya kuwa mgombea.
Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 39 (1) (b) (d)  kinasema mtu anayestahili kushika nafasi ya Urais awe ametimiza miaka 40.
“Katiba inatakiwa mgombea awe ametimiza miaka 40 kwa tafsiri ya Kiswahili lazima mgombea awe na miaka 40 na asizidi au kupungua na kwa tafsiri hiyo hata wale wagombea wengine waliovuka miaka 40 hawana sifa,” alisema.
Alisema Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere aliiwakilisha nchi kwenye baraza la Umoja wa mataifa (UN) akiwa na  umri wa miaka 33. Alisema hata alipohojiwa alisema kuwa asipimwe kwa umri bali kwa utendaji wake na pingamizi hilo likaondolewa.
Malupa alisema iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania ataboresha kilimo. Alisema sekta ya kilimo ni sekta mama inatakiwa kupewa msukumo mkubwa.
Pia alisema atapandisha hadhi vyuo vya kilimo ili viweze kutoa wataalamu wengi zaidi ambao watakwenda kutoa msukumo mkubwa kwa wakulima na kuongeza uzalishaji. Malupu alisema atahakikisha sekta ya elimu na michezo zinakuwa bora.
Alipohojiwa ni wapi alipopata fedha za kulipia fomu alisema miongoni mwa waliomchangia fedha za kuchukua fomu ni wanachama wa upinzani na aliongeza kuwa, ameamua kugombea nafasi hiyo ili aweze kutumikia watanzania kwani ana uzoefu kwenye uongozi ambapo miongoni mwa nafasi anazoshikilia mpaka sasa ni nafasi ya Uenyekiti wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Morogoro.
Chagama ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema akichaguliwa na chama chake na hatimaye kuwa Rais wa Tanzania, atarekebisha mfumo wa utekelezaji wa haki, huku akiahidi jambo atakaloanza nalo kuwa ni kushughulikia suala la ajira kwa vijana na kurekebisha mfumo wa utekelezaji wa haki.
Akizungumzia elimu yake, alisema alipata shahada yake ya kwanza ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Bugema, Uganda, huku shahada ya pili akiipata katika Chuo Kikuu cha Wales, Lampeter nchini Uingereza na shahada ya tatu alisoma Chuo Kikuu cha Surrey, Uingereza ingawa hakuweza kuhitimu kwa kile alichosema ni kutokana na tatizo la kimazingira .
“Mimi ni mtaalamu wa jinai na ninaweza kusimamia haki, unapofikiria uchumi
wa nchi lazima kusimama kwenye mstari na wananchi wajue haki zao,” alisema na kuongeza kuwa, wananchi wana matumaini na CCM hivyo anaamini ni miongoni mwa wanaofaa kwa Urais wa nchi.

No comments: