BINTI WA MIAKA 9 APAMBANA NA MAMBA KWA DAKIKA 30 MPANDA

Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka tisa ameonesha ujasiri wa kipekee kwa kumwokoa mama yake mzazi, Magreth Ibrahim (50) kuuawa na mamba baada ya kupambana na mnyama huyo kwa zaidi ya nusu saa.

Mama huyo mkazi wa kijiji cha Karema, mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Mpanda,  kwa sasa amelazwa katika Hospitali  ya wilaya ya Mpanda mjini Mpanda kwa matibabu  baada ya mkono wake kunyofolewa na mamba aliyemshambulia wakati akifua  kando  ya Mto Ikola.
Akimweleza Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima aliyemtembelea  hospitalini hapo  masaibu yaliyomsibu, alisema anamshukuru sana binti yake mwenye umri wa miaka  tisa aliyeweza kuokoa  maisha yake  licha ya kuwa  amenyofolewa  mkono na mamba huyo.
Akisimulia  mkasa huo, Magreth alieleza kuwa juzi  akiwa anafua kando  ya mto Ikola ghafla mnyama huyo  aliibuka majini  na kumpiga  usoni na mkia wake.
“Mamba huyo aliibuka ghafla mtoni  na kunichapa usoni  na mkia wake nami  nikaangukia  majini  ndipo  aliponidaka mkono wangu  na  kunivutia mtoni ….binti yangu  aliyekuwa  jirani yangu alipoona  niko karibu kuliwa na mamba  kwa ujasiri  aliweza  kukabiliana naye …
Alinishika mkono mwingine na kunivutia nje huku akipiga kelele kumtisha  mnyama huyo ili aniachie hatimaye  akaunyofoa mkono wangu  na kutokomea  nao  mtoni ….” alieleza.
Aliongeza kuwa watu waliokuwa wakifua mtoni hapo  wengi wao wakiwa wanawake walifika eneo la tukio ambapo wakiwa na  binti yangu walimvuta na kumtoa nje  na baadae wakamkimbiza  hospitalini  mjini Mpanda  kwa matibabu.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Dk Joseph Mkemwa  amethibitisha kuwa hali ya mama huyo inaendelea kuimarika baada ya kupatiwa  matibabu.
Kwa upande wake, Mwamlima amepiga marufuku  wakazi wilayani humo kuoga au kufulia katika mito na  maziwa  ili  wajiepushe na visa vya kusambuliwa na mamba.

No comments: