Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto
amemjia juu Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja kwa kumtaja juzi mbele ya
Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma wakati akijitetea, kuwa Zitto alipewa fedha na kampuni ya PAP na NSSF.
Aliomba Sekretariati ya Maadili kuchukua kwa
uzito maoni ya Ngeleja na kama yana uzito kwa mujibu wa sheria na kanuni,
yafanyiwe uchunguzi.
Alisema yuko tayari kwa uchunguzi mahususi
dhidi yake kuhusu tuhuma zilizotolewa na nyingine zitakazotolewa na mtu yeyote,
ikiwemo madai hayo ya Ngeleja.
“Katika kujitetea mbele ya Baraza la Maadili
kuhusu tuhuma dhidi yake za kugawiwa mgawo wa fedha kutoka akaunti ya Escrow,
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja alisema kuwa ni kawaida wabunge kupewa
misaada na wafanyabiashara na taasisi za umma,” alisema Zitto.
Alisema Ngeleja alirudia tuhuma ambazo kwa
mujibu wa Zitto, zilizokwishatolewa huko
nyuma kwamba alipewa fedha na kampuni ya
PAP na shirika la NSSF.
“Hivyo narudia kutamka kwamba ninataka
uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo ufanyike mara moja, wenye ushahidi wapeleke
kwenye vyombo vya uchunguzi na niitwe mbele ya Baraza la Maadili kujieleza,”
alisema.
Zitto, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema licha ya yeye
kushambuliwa, vile vile wajumbe wa kamati wanashambuliwa.
“Nashambuliwa, tunashambuliwa! PAC tunasema
hatutetereki,” alisema na kusisitiza tuhuma hizo alizoshazifafanua
na hazina msingi wowote, zilikuwa siasa
za majitaka.
Aliendelea kusema, “Hata hivyo bado zimekuwa
zikijirudia rudia kwa malengo maalumu wanayoyajua wanaotoa tuhuma
hizo…Watuhumiwa wa ufisadi wa Escrow hawajazoea kuona taasisi za maadili
zikifanya kazi kwa namna ilivyo sasa na hivyo wanajaribu na watajaribu
kuhangaika, ikiwemo kutaka kila mtu aonekane ni mtuhumiwa kama wao”.
Alisema ndiyo maana Ngeleja ametaja watu
wakiwemo wafanyabiashara, kwamba huwapa fedha wabunge bila ushahidi.
Alisema akiwa mbunge ambaye maisha yake ya siasa, ameyatumia kupambana na ufisadi na
kuchochea mabadiliko kujenga misingi madhubuti ya uwajibikaji na kuimarisha
taasisi zake, yuko tayari kuchunguzwa.
Mbunge huyo alisema anaunga mkono kazi kubwa
inayofanywa na Baraza la Maadili kwa kusisitiza kwamba, ilipaswa kuwa
imefanyika kwa muda mrefu kwa kashfa mbali mbali zilizohusisha viongozi wa
umma.
Alisema katika kujenga misingi madhubuti ya
uwajibikaji nchini ni lazima kila kiongozi aheshimu taasisi kama Baraza la
Maadili. Alisema likiendelea kufanya
kazi kama inavyofanyika sasa, vita dhidi ya ufisadi itakuwa imepiga hatua na
porojo za kuzushiana mitaani, zitapungua.
Katika utetezi wa Ngeleja mbele ya Baraza la
Maadili, Ngeleja aliwasilisha kielelezo
cha tuhuma zilizowasilishwa bungeni na Kambi ya Upinzani na Mbunge wa Mtera,
Livingstone Lusinde dhidi ya Zitto kuwa alipokea zaidi ya Sh milioni 30 kutoka
Tanapa, NSSF na kampuni inayohusishwa na akaunti ya Tegeta Escrow ya Power Solution Limited (PAP.
Alisema
pamoja na tuhuma hizo dhidi ya Zitto kuwasilishwa bungeni na vielelezo
na kutaka Zitto afikishwe mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge, hakuna hatua zilizochukuliwa.
“Ndio maana nasema hata kama ningepokea msaada
huo kutoka VIP Engineering, haukuwa kwa ajili ya maslahi yangu kwa sababu ni
utamaduni uliojengeka kwa kampuni duniani kote kutumia sehemu ya faida zao
kusaidia jamii, lakini pia nisingekuwa mbunge wa kwanza kupokea msaada wa aina
hiyo,” alisema Ngeleja.
Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT) mwaka 2006 kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya tozo
ya uwekezaji (capacity charges),
zilizokuwa zinalipwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kabla hazijakabidhiwa
kwa anayelipwa, ambaye ni kampuni binafsi ya kufua umeme ya IPTL. Kabla ya kuzuka kwa mabishano kuhusu tozo
hiyo, TANESCO ilikuwa inalipa moja kwa moja kwa IPTL.
No comments:
Post a Comment