Maafa makubwa yameikumba Wilaya ya Kahama
mkoani Shinyanga baada ya watu 42 kufa papo hapo na wengine 82 kujeruhiwa,
kutokana na mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali, iliyonyesha katika Kijiji cha Mwakata Kata ya
Isaka.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alisema jana kuwa tukio hilo
halijawahi kutokea mkoani humo.
Baadhi ya majeruhi, akiwemo Paulina Malongo
aliyefiwa na wajukuu wanne, walieleza hali ilivyokuwa.
Shughuli za uokoaji ziliendelea hadi jana
chini ya Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, ambapo
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson
Mpesya alisema huenda idadi ya waliokufa na majeruhi, ikaongezeka.
Kamanda alisema mvua hiyo iliyosababisha
maafa, ilinyesha juzi saa 3 usiku katika kijiji hicho ikiambatana na upepo
mkali ulioangusha miti, kubomoa na kuezua nyumba, hivyo kusababisha vifo na
majeruhi hao. Inadaiwa wengi waliopoteza
maisha ni watoto.
Baadhi ya majeruhi waliolazwa katika Hospitali
ya Wilaya ya Kahama, walisema mvua ilikuwa kubwa ikiambatana na upepo mkali.
Walisema nyumba zilizoezuliwa na wakati huo huo upepo uling’oa miti.
“Tulikuwa tumelala majira ya saa tatu usiku
ghafla tulisikia upepo mkali ukiambatana na mvua kubwa ya mawe. Maji mengi
yaliingia ndani na ghafla nyumba yangu ilianguka na nimepoteza wajukuu wangu
wanne,” alisema Paulina Malongo, ambaye ni mkazi wa Kijiji hicho cha Mwakata.
Kamanda Kamugisha alisema majeruhi
walikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Kahama kwa ajili ya kupatiwa matibabu
wakati jitihada zaidi za uokozi zikiendelea katika kijiji hicho.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya
Kahama, Dk Joseph Ngowi akizungumza na
waandishi wa habari, alisema amepokea majeruhi zaidi ya 60 na kati yao watatu walifariki wakati wakiendelea na
matibabu hospitalini hapo.
“Hatuna idadi kamili ya watu waliojeruhiwa au
waliokufa na tumetuma madaktari wetu kwenda katika kijiji hicho kwa ajili ya
huduma ya kwanza pamoja na kufanya uchunguzi ili kubaini idadi kamili ya
waliofariki dunia,” alisema Ngowi.
Dk
Ngowi alisema kutokana na umbali
uliopo kutoka eneo la tukio hadi hospitali ya wilaya, wamelazimika kutuma jopo
la madaktari kwenda eneo la tukio, kubaini waliofariki na kuidhinisha maziko
kupunguza gharama kwa wananchi waliofiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya alisema Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Wilaya ilitegemea kukaa jana mchana kutathimini takwimu za uharibifu
wa mali na idadi ya nyumba zilizokumbwa na maafa .
Mpesya alisema Jeshi la Zimamoto na
Uokoaji kwa kushirikiana na
wananchi, wanaendelea na shughuli za
uokoaji na huenda idadi ya waliokufa
pamoja na majeruhi ikaongezeka katika tukio hilo.
Watu wapatao 3,500 wameathiriwa na maafa hayo
katika Kata ya Mwakata. Kwa upande wa
kaya zilizoathirika, 350 ni za Kijiji
cha Makata, 100 za Kijiji cha Ngumbi na kaya 50 za Kijiji cha Magung’hwa.
Athari zilizobainika papo hapo ni nyumba
kadhaa, kuezuliwa na nyingine kubomoka, hali ambayo imesababisha kaya husika
kukosa mahali pa kuishi. Aidha chakula cha akiba katika kaya hizo, kimeharibika na kingine kusombwa na maji.
Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za
rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ali Rufunga kuomboleza vifo vya watu 42 waliofariki
na majeruhi zaidi ya 82.
“Nimepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa
taarifa za vifo vya watu 42 waliopoteza maisha na wengine 82 waliojeruhiwa na
kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama kwa matibabu baada ya nyumba
zao kusombwa kabisa na maji kutokana na mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na
upepo mkali kunyesha,” alisema Kikwete.
Katika taarifa iliyotumwa na Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Ikulu jana, Rais Kikwete amesema msiba huo siyo wa
wana-Shinyanga pekee, bali ni wa taifa zima ambalo limepoteza nguvukazi muhimu
kwa maendeleo yake na ustawi wa jamii ya Watanzania kwa ujumla.
“Naomba upokee salamu zangu za rambirambi
kutoka dhati ya moyo wangu kwa kupotelewa ghafla na wananchi 42 kwa mara moja
katika Mkoa wako. Kupitia kwako, naomba rambirambi zangu na pole nyingi
ziwafikie wafiwa wote kwa kuondokewa na wapendwa, ndugu na jamaa zao,” alisema.
Rais Kikwete aliwaomba wafiwa wote wawe na
moyo wa uvumilivu, utulivu na subira wakati huu wa majonzi makubwa kwao
wanapoomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao.
Aliwataka kutosahau ukweli kwamba kazi ya
Mungu haina makosa. Aidha
amewahakikishia wafiwa wote kuwa yuko pamoja nao katika kipindi chote cha
kuomboleza msiba huu mkubwa kwao na kwa taifa.
“Namwomba Mola awawezeshe majeruhi wote wa
tukio hilo wapone haraka ili waweze kuungana tena na familia, ndugu na jamaa
zao na kuendelea na maisha yao kama kawaida”, alisema katika salamu zake za
rambirambi.
No comments:
Post a Comment