MAMBO MAGUMU KWA NGELEJA BARAZA LA MAADILI YA VIONGOZI


Mbunge wa Sengerema,  William Ngeleja amekiri mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kwamba, aliomba na kupokea Sh milioni 40.4 kutoka kwa James Rugemalira, kwa kujitetea alifanya hivyo kama ilivyo kawaida pia kwa wabunge wengine.

Ngeleja  alidai mbele ya baraza hilo kwamba, msaada huo aliopewa na Rugemalira hauna tofauti na  mingine aliyowahi kupokea kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa kama vile Reginald Mengi, Said Salim Bakhresa na Yusuf Manji.
“Msaada niliopewa na Rugemalira hauna tofauti na misaada mingine wanayopewa wabunge wenzangu au misaada mingine niliyowahi kupokea kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa kama vile akina Mengi, Bakhresa, Yusuf Manji, mashirika ya hifadhi ya jamii kama vile NSSF, PSPF, NHC, NHIF na benki ya CRDB na NBC,” alisema.
Alitoa utetezi huo baada ya kusomewa mashitaka na baraza hilo,  Dar es Salaam jana, ikidaiwa Februari 12, mwaka jana, alipokea kitita hicho cha fedha kutoka kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, kwa ajili ya maslahi yake kiuchumi, jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Getrude Cyriacus alisema mlalamikiwa ni Mbunge wa Sengerema ambaye kwa mujibu wa Sheria ni kiongozi wa umma, hivyo akiwa kama mbunge alikiuka maadili hayo ya viongozi wa umma kwa kuomba fadhila ya kiuchumi kwa Rugemalira kinyume cha Sheria.
Akijitetea, Ngeleja alitaka kufahamu endapo shahidi na baraza hilo kwa ujumla, linafahamu kazi na wajibu mahususi wa mbunge kwa wananchi wake.
Alikiri kupokea fedha hizo kutoka kwa Rugamalira kupitia kampuni yake ya VIP TZS Trustees na si VIP Engineering and Marketing Limited, na kusisitiza kwamba fedha hizo alizitumia kwa ajili ya maendeleo ya miradi ya jimboni kwake, ambayo haikupangiwa fedha katika bajeti ya Serikali kulingana na uhaba wa fedha uliopo.
“Sijawahi kuomba wala kupokea fadhila za kiuchumi kutoka kwa Rugemalira isipokuwa kama Mbunge wa Sengerema kwa nyakati tofauti kama wabunge wengine wanavyofanya, niliomba misaada ya kiuchumi kwa ajili ya kusaidia wananchi wa jimbo langu na Watanzania kwa ujumla,” alisisitiza.
Alisema amekuwa akipokea maombi ya misaada kama mbunge,  kutoka kwa wananchi mbalimbali yanayogusa maeneo kadhaa kama vile misikiti, makanisa, kuchangia vikundi vya wajasiriamali na hata kwenye michango ya miradi ya maendeleo, jambo linalomlazimu kuomba msaada zaidi kutoka kwa wafadhili.
Pamoja na kutaja wafanyabiashara na mashirika yaliyowahi kumsaidia, Ngeleja aliwasilisha vielelezo vya misaada  hiyo. Pia  aliwasilisha  kielelezo cha tuhuma zilizowasilishwa bungeni na Kambi ya Upinzani na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde dhidi ya Zitto kuwa alipokea zaidi ya Sh milioni 30 kutoka Tanapa, NSSF na kampuni inayohusishwa na akaunti ya Escrow ya Power Solution Limited (PAP).
Kwa mujibu wa Ngeleja, pamoja na tuhuma hizo dhidi ya Zitto kuwasilishwa bungeni na vielelezo na kutaka Zitto afikishwe mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, hakuna hatua zilizochukuliwa.
“Ndio maana nasema hata kama ningepokea msaada huo kutoka VIP Engineering haukuwa kwa ajili ya maslahi yangu kwa sababu ni utamaduni uliojengeka kwa kampuni duniani kote kutumia sehemu ya faida zao kusaidia jamii, lakini pia nisingekuwa mbunge wa kwanza kupokea msaada wa aina hiyo,” alisema.
Pamoja na utetezi huo wa Ngeleja, Cyriacus alisema utetezi uliowasilishwa na kiongozi huyo, hauna mashiko kisheria.
“Amejitetea kwamba fedha alizopokea zimetolewa kwa ajili ya maendeleo ya jimbo lake, lakini si kweli kwa sababu nyingine alichangia Kanisa Dar es Salaam, kutokana na hili naomba apewe adhabu kali iwe fundisho.”
Mwenyekiti wa Baraza hilo Jaji Hamisi Msumi, alisema baraza hilo limepokea na kusikiliza pande zote mbili na litawasilisha uamuzi wake kwa mamlaka husika ambapo itajulikana endapo mbunge huyo atahitaji kujibu mashtaka yanayomkabili au la.
Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Cyriacus, Februari 12, mwaka jana, Ngeleja alipokea Sh milioni 40.4 kutoka kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited yenye hisa asilimia 30 na Kampuni ya IPTL yenye mkataba wa kuuziana umeme  na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Alidai fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti namba 00110102652601 iliyoko katika Benki ya Mkombozi tawi la St Joseph jijini Dar es Salaam.
Shahidi  upande wa mlalamikaji,  ambaye pia ni Katibu Msaidizi Idara ya Viongozi wa Siasa, Uchaguzi na Maadili kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma,  Waziri Kipacha, alidai kitendo cha mbunge huyo kuomba na kupokea fedha hizo ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inayokataza kiongozi wa umma kuomba, kudai na kupokea fedha kwa maslahi yake binafsi .
Alidai kamati hiyo pia iliibaini mwaka 2007, Ngeleja  alikuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na ilipofika mwaka 2008 hadi 2012, alipanda na kuwa Waziri kamili wa wizara hiyo iliyokuwa ikisimamia utekelezaji wa mkataba baina ya Tanesco na IPTL wa kuuziana umeme.
“Kitendo cha baadaye mlalamikiwa kupokea fedha kutoka kampuni ya VIP yenye hisa asilimia 30 na kampuni ya IPTL yenye mkataba wa kuuziana umeme na Tanesco ni kujiingiza kwenye mgongano wa maslahi,” alidai Kipacha.
Katika hatua nyingine, aliyekuwa Mkurugenzi wa Huduma za Sheria katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma, amewasilisha ombi la kutaka Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, kuahirisha kusikiliza shauri linalomkabili, kutokana na kesi ya msingi inayoendelea Mahakama Kuu.
Mujunangoma alitakiwa kuwasilisha utetezi wake dhidi ya mashitaka yanayomkabili mbele ya baraza hilo. Mashitaka hayo ni kuendelea kuwa mshauri mwelekezi wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited akiwa na wadhifa wa Mkurugenzi wa Huduma za Sheria katika Wizara ya Ardhi.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Mujunangoma kupitia wakili wake Jamhuri Johnson, aliwasilisha  hati ya pingamizi la shauri hilo kuendelea kusikilizwa na baraza hilo hadi kesi ya msingi iliyofunguliwa Mahakama Kuu itakapokamilika.
“Naomba kuwasilisha pingamizi juu ya uwezo wa baraza hili kuendelea kusikiliza shauri hili kulingana na uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu wa kuzuia suala la akaunti ya Escrow kujadiliwa na chombo chochote, hadi pale kesi ya msingi itakapoamuliwa,” alidai Johnson.
Alidai wanafahamu baraza  lilishapokea pingamizi kama hilo kutoka kwa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na uamuzi wa kulitupia mbali ukatolewa, hivyo na mlalamikiwa huyo, anaomba achukue hatua zilezile alizochukua Chenge za kukata rufaa Mahakama Kuu.
“Tunajua kuwa baraza lilishatoa uamuzi dhidi ya pingamizi la Chenge kuwa lina uwezo wa kuendelea kusikiliza shauri lake, na sisi tunaomba pia tukate rufaa Mahakama Kuu. Bado tunaamini hili baraza halina uwezo huo kulingana na uamuzi wa Mahakama Kuu,” alisisitiza.
Mwenyekiti wa Baraza hilo Jaji Hamisi Msumi, alitaka kufahamu endapo mawakili hao pia wanawasilisha pingamizi sawa na la Chenge, aliyedai baraza hilo limezuiwa na amri hiyo ya Mahakama Kuu na endapo Mujunangoma amehusishwa moja kwa moja katika kesi hiyo ya msingi ya Mahakama Kuu.
Akijibu, Wakili  Johnson alidai mteja wao si mhusika wa moja kwa moja katika kesi hiyo ya Mahakama Kuu isipokuwa mashitaka yaliyofunguliwa katika kesi hiyo yanafanana na yaliyowasilishwa na baraza hilo dhidi ya mteja wao.
“Lakini pia mwenyekiti kuna kesi nyingie inayomkabili mteja wetu katika Mahakama ya Kisutu sawa na hii bado inaendelea, nahofia asije akaadhibiwa mara mbili, kwani mlalamikiwa aliyesimama mbele yako si kiogozi wa umma alishavuliwa madaraka yake,” alisema.
Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Hassan Mayunga, alidai pingamizi hilo halina mashiko kwa kuwa tayari baraza hilo lilishatoa uamuzi kwamba linayo mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
“Tunachofanya hapa kama baraza ni uchunguzi kwamba mlalamikiwa ana kesi ya kujibu au la, sheria inasema wazi tunaweza kusikiliza shauri hili ilimradi mlalamikiwa asihukumiwe,” alisisitiza.
Jaji Msumi baada ya kupokea faili la kesi inayomkabili Mujunangoma Kisutu na kupokea hati ya pingamizi hilo, aliahirisha shauri hilo hadi kesho atakapolitolea uamuzi.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya baraza, Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mwarabu Talle, alidai kitendo cha Mujunangoma kuwa mshauri mwelekezi huku akiwa kiongozi wa umma, ni ukiukaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, inayokataza kiongozi wa umma kujiingiza katika mgongano maslahi.
Aidha alidai mashitaka mengine yanayomkabili Mujunangoma ambaye tayari amesimamishwa wadhifa wake wa ukurugenzi ni kutumia wadhifa wake wa ushauri wake kisheria anaoutoa katika kampuni ya VIP na Mabibo, Wines and Spirit na kujipatia maslahi ya kifedha jumla ya Sh milioni 423.4 kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
“Fedha hizo ziliingizwa katika akaunti ya mlalamikiwa namba 00120102602001 iliyoko kwenye Benki ya Mkombozi tawi la St Joseph jijini Dar es Salaam,” alidai Talle.
Aidha alidai mashitaka mengine ni pamoja na mlalamikiwa kutotamka maslahi aliyokuwa nayo katika mkataba wa Tanesco na IPTL kupitia kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, kinyume na matakwa ya Kisheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Alidai mlalamikiwa huyo pia hakutamka madai yake aliyokuwa anaidai kampuni ya VIP na Mabibo Beers, Wines and Spirit kwa Kamishna wa Maadili kwa kipindi cha mwaka 2013 kinyume na sheria hiyo ya maadili.

No comments: