Simba jioni ya leo ilirudia ugonjwa wake wa sare baada
ya kutoka 0-0 na Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo wa duru la kwanza baina ya timu hizo
uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mwaka jana timu hizo zilifungana
mabao 2-2.
Mabao ya Simba yalifungwa na Shaaban Kisiga na
Amis Tambwe kipindi cha kwanza, huku yale ya Coastal Union yakifungwa na Rama
Salim na Yayo Lutimba yote kipindi cha pili.
Msimu huu umekuwa si mzuri kwa Simba, ambapo
imekuwa ikipata matokeo yasiyoridhisha, ingawa mchezo wa wiki iliyopita
ilishinda mabao 2-1 dhidi ya JKT Ruvu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, hivyo
kuwapa imani mashabiki kwamba wangeibuka na ushindi leo.
Kutokana na matokeo hayo Simba imefikisha
pointi 17 ikiendelea kuwa nafasi ya nane, huku Coastal ikifikisha pointi 18 na
inashika nafasi ya saba.
Katika mchezo huo mashabiki walishuhudia
kosakosa nyingi za kila upande kwa washambuliaji kushindwa kutulia
walipokaribia lango.
Simba ilipata nafasi kadhaa za kufunga, lakini
washambuliaji wake, Emmanuel Okwi, Danny Sserunkuma na Elias Maguli walikosa
umakini.
Nayo Coastal Union ingeweza kupata bao kama
ingetumia nafasi kadhaa ilizopata, lakini washambuliaji wake wakiongozwa na
Rama Salim na Hussein Sued walishikwa kigugumizi kila walipomkaribia kipa Ivo
Mapunda.
Mabeki wa Coastal jana walikuwa na kazi moja
tu kuwadhibiti washambuliaji Waganda wa Simba, Okwi na Sserunkuma wasilete
madhara.
Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo jioni ya leo
Uwanja wa Jamhuri Morogoro, timu ya Azam ilitoka sare ya bao 2-2 na Polisi
Morogoro.
Mabao ya Azam yalifungwa na Brian Majwega na
Kipre Tchetche wakati yale ya Polisi yalifungwa na Cristopher Edward na
Selemani Kassim.
Kwa matokeo hayo Azam imefikisha pointi 23
sawa na Yanga, lakini yenyewe ikiwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na
kufungwa, hivyo kuongoza ligi hiyo.
Kabla ya mchezo wa Azam wa jana, Yanga ilikuwa
ikiongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 23 na Azam ikiwa nafasi ya pili. Timu zote
sasa zimecheza mechi 12.
Matokeo ya mechi ya Simba dhidi ya Coastal
Union na Azam dhidi ya Polisi ni furaha kwa mashabiki wa Yanga, ambao kama kesho Jumapili
timu yao itaifunga Mtibwa Sugar itafikisha pointi 26 na kukaa tena kileleni.
Mapema wiki hii, nahodha wa Yanga, Nadir
Haroub alisema dhamira yao ni kufanya vizuri huku wakiombea Simba na Azam
zifanye vibaya.
Uwanja wa Nangwanda Sijaona, timu ya Ndanda FC
nayo ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Stand United, huku JKT Ruvu ikifungana
bao 1-1 na Mbeya City Uwanja wa Azam Chamazi.
Bao la JKT Ruvu lilifungwa na Ally Billali
wakati la Mbeya City lilifungwa na Kenny Ally.
No comments:
Post a Comment