Taasisi inayoshughulika na mambo ya Utafiti wa
Kupunguza Umasikini (Repoa) ni miongoni mwa taasisi nne za Tanzania ambazo
zimeorodheshwa kwenye ripoti ya dunia kuwa ni taasisi zinazofanya vizuri katika
masuala ya utafiti, ufuatiliaji na ushauri.
Ripoti hiyo ambayo imetayarishwa na wataalamu
kutoka Chuo Kikuu cha Pennsylavania, imezitaja taasisi nyingine kuwa ni Taasisi
ya Utafiti ya Uchumi na Jamii (ESRF), Taasisi inayoshughulika na Utafiti wa
Mambo ya Teknolojia (ATPS) na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).
Kwenye ripoti hiyo ambayo imezigawa taasisi
hizo kwenye kanda, kwenye nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara ambako
kumeorodheshwa taasisi 65
zinazoshughulika na utafiti wa uchumi na 46 zinazoshughulika na sayansi na
teknolojia, Repoa imeshika nafasi ya 18 kwenye kundi la taasisi za mambo ya
uchumi.
ESRF kwenye kundi hilo imeshika nafasi ya 42
na ATPS imeshika nafasi ya 51 huku Costech imewekwa kwenye kundi la taasisi za
mambo ya sayansi na teknolojia ambako imeshika nafasi ya 44. Katika ukanda wa
Afrika Mashariki, Repoa imeshika nafasi ya tatu.
Mpango huo unahusisha taasisi zinazoshughulika
na utafiti kwa ajili ya kutumika kutunga
sera mbalimbali za nchi na umebatizwa jina
la Think Tanks & Civil Societies Program umefanywa na taasisi ya
Lauder ya Chuo Kikuu cha Pennsylavania na umehusisha 6,600 na unalenga
kuzitathmini zinafanya nini na msaada wake kwa nchi husika.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya dunia, waandaaji
wamehojiana na watu 20,000 wakiwemo waandishi wa habari, watunga sera, watu wa
kawaida na wahisani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo
kwa hapa nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa Profesa Samuel Wangwe
alisema taasisi za utafiti na ushauri
zimeongezeka duniani; lakini kwa miaka ya hivi karibuni baadhi ya taasisi hizo
zimepungua kutokana na baadhi yake kusimamisha shughuli zake.
"Lakini mahitaji ya taasisi hizi
yameongezeka kwa vile watu wanaotaka
kupata taarifa nje ya mfumo wa serikali umeongezeka, kwa hiyo kazi
iliyoko mbele yetu bado ni kubwa," alisema.
Profesa Wangwe (pichani) alisema pamoja na mahitaji
hayo, taasisi hizo za utafiti zinakabiliwa na ukosefu wa fedha kutokana na
serikali kutozifadhili na hivyo kutegemea fedha za wahisani. Alisema kuna haja
ya Serikali kuzitambua taasisi hizo kama ilivyo kwa nchi ya Botswana.
No comments:
Post a Comment