MOTO WATEKETEZA KILA KITU KANISANI KIGOMA

Watu wasiojulikana wamelichoma moto na kuliteketeza Kanisa la Evangelical Assemblies of God wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma na kuteketekeza kila kitu kilichokuwemo ndani ya kanisa hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Venance Mwamoto amesema kuwa tukio hilo la mwanzoni mwa wiki hii, limeacha athari kubwa za mali na kwamba hakuna mtu yeyote ambaye amepata madhara kuhusiana na uharibifu.
Mwamoto ambaye ni Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kakonko, alisema kuwa bado haijajulikana hasa sababu ya kuchomwa kwa kanisa hilo.
Lakini, alibainisha kuwa sababu mbili kubwa, ikiwemo ya mgawanyiko wa viongozi na masuala ya kisiasa yanaweza kuwa chanzo cha tatizo hilo.
Alisema zipo taarifa za masuala ya kisiasa kufanywa na baadhi ya viongozi wa kanisa hilo, ikiwemo vyombo vilivyokuwa vinatumika kwenye kampeni kwa mgombea wa  uenyekiti wa kijiji hicho kupitia chama cha NCCR – Mageuzi, ambaye ni kiongozi wa kanisa na ambaye alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kijiji.
Alisema kuwa masuala hayo ya siasa na mgogoro wa viongozi wa kanisa, yanafanyiwa kazi kwa kina ili kubaini ukweli.
Alisema kwamba kiongozi mmoja wa kanisa hilo, anashikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama akituhumiwa kuhusiana na uchomaji huo .
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma, Jafari Mohammed alithibitisha tukio  hilo na kwamba uchunguzi kujua sababu hasa za kuchomwa kwa kanisa hilo, unaendelea.

No comments: