Timu ya soka ya Simba ya Dar es
Salaam imejikuta ikiangukia pua baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Mbeya City katika
pambano la Ligi Kuu ya Vodacom lililomalizika muda mfupi uliopita kwenye Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika pambano hilo lililoshuhudia mwamuzi
Abdallah Kambua kutoka Shinyanga akitoa penalti mbili kila upande katika dakika
za nyongeza, Simba ikitandaza soka safi iliwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao
1-0 lililowekwa kimiani na Ibrahim Salum Hajib dakika ya 45+2.
Bao hilo lilitokana na mpira wa
adhabu ndogo umbali ya takribani mita 20 kutoka langoni mwa Mbeya City baada ya
Awadh Juma kufanyiwa madhambi.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi
huku vijana wa Mbeya City inayonolewa na Juma Mwambusi wakizinduka na kulisakama
lango la wapinzani wao Simba kama nyuki na hatimaye juhudi zao zikazaa matunda
katia dakika ya 77 baada ya kusawazisha bao kupitia kwa Hamad Kibopile.
Kibopile alifunga bao hilo kwa
kutumia makosa yaliyofanywa na mabeki wa Simba kuchanganyana na kipa wao, Manyika
Peter.
Wakati kila shabiki akiamini mechi
hiyo itamalizika kwa sare, dakika ya 90+2 vijana wa Mbeya City wakapata penalti
baada ya kipa wa Simba Manyika kumkamata mguu Raphael Daudi akiwa katika
harakati za kufunga. Yussuf Abdallah akauweka mpira kimiani na kuiandikia timu
yake bao la pili.
Kama filamu vile, dakika moja baada
ya bao hilo mwamuzi akaizawadia Simba penalti ambayo hata hivyo ikashuhudia
shuti la beki Nassor Masoud ‘Chollo’ likigomba mwamba wa juu na kutoka nje.
Hii ni mechi ya kwanza kwa kocha wa
Simba, Goran Kopunovic kupoteza baada ya kushinda 2-0 dhidi ya Ndanda na kutoka
sare ya 1-1 dhidi ya Azam.
Kwa matokeo hayo, Simba sasa inabaki
na pointi zake 13 kutokana na mechi 11, huku Mbeya City ikifikisha pointi 15
kutokana na mechi 11.
No comments:
Post a Comment