Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Tanzania Bara), Mwigulu Nchemba amekubali
kuitikia wito wa kusitisha ziara zake za kichama katika mikoa na wilaya
mbalimbali nchini, kama alivyoagizwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman
Kinana.
Katika barua yake ya Januari 18, mwaka
huu, Kinana alimwagiza Mwigulu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mbunge wa
Jimbo la Iramba Magharibi mkoani Singida,
kusitisha mara moja ziara zote na
kwamba endapo atataka kufanya hivyo, atalazimika kutoa taarifa na kupata
kibali.
Akizungumza jana na gazeti hili, Mwigulu
alikiri kupokea barua hiyo, na kusema hana tatizo na kusitisha ziara zake za
kichama, kwani ni maagizo halali ya mamlaka ya juu yake kichama.
“Haya ni maelekezo, na siku zote kwa kuwa
nafanya kazi kwa mujibu wa Katiba, sioni tatizo kupokea maelekezo rasmi ya
kiofisi…aliyeniagiza ni kiongozi wangu katika chama, nitafanya hivyo,” alisema
kiongozi huyo kijana, lakini machachari katika ulingo wa siasa.
Katika siku za hivi karibuni, amekuwa
akipasua anga kwa kutumia helikopta katika ziara zake alizofanya mikoa ya Tanga
na Morogoro.
Mwigulu alisema amekuwa akipokea mialiko
mingi ya kichama, hivyo anajikuta akitumia muda wake wa ziada wa siku za
mwishoni mwa wiki kufanya ziara, lengo likiwa kutenganisha muda wa utendaji
wake katika chama na serikalini.
“Ndiyo maana nilikuwa nafanya ziara za
kichama siku za mwisho wa wiki pekee…na baada ya Morogoro pia nimealikwa
Kigoma, Mafia (Pwani), Kagera, mikoa ya
Kusini na Njombe. Kwa ujumla mialiko ni mingi, lakini nitaifanya kwa kufuata
maelekezo.
“Sitavunja sheria za chama wala za nchi
hata siku moja, nitawatumikia wananchi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa,”
alisisitiza Mwigulu.
Barua hiyo ambayo Kinana alimwandikia
Mwigulu tarehe 18 Januari mwaka huu,
mwaka huu ilisomeka hivi: “Umekuwa ukifanya ziara nyingi katika mikoa na wilaya
bila ushirikishwaji kamili wa Makao Makuu, Mikoa na hasa Kamati za Siasa. Wewe
pia umeonesha kwa kauli na mienendo yako kujiandaa kugombea nafasi ya Urais
kupitia CCM. Ziara hizi zina mwelekeo wa kampeni, jambo ambalo ni kinyume na
maadili ya Chama. Nakuagiza kuzisitisha ziara zote. Iwapo utataka kufanya ziara
yoyote ya Kichama itabidi kwanza uniarifu na upate kibali changu. Nakuagiza
utekeleze agizo hili mara moja”.
Hata hivyo, mara zote alizoulizwa kuhusu
kuwania Urais mwaka huu, Mwigulu amekuwa haweki wazi dhamira hiyo kama
inavyoelekezwa.
Lakini, amekuwa akisisitiza amekuwa
akiombwa kufanya hivyo na makundi ya watu mbalimbali, wakiwemo wanasiasa,
wasomi, wakulima na wafanyakazi, vijana, wazee, wanawake na wanaume.
No comments:
Post a Comment