SHIBUDA AJIENGUA CHADEMA


Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), amesema hatagombea ubunge kupitia Chadema katika Uchaguzi Mkuu ujao, kwa   kuwa amechoshwa na kauli za vitisho na kejeli dhidi yake, zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho.
Amesema hayo jana kwa nyakati tofauti, wakati akizungumza na wazee wa Mji wa Maswa na Malampaka wilayani humo, alipokuwa akijibu swali lao kuhusu hatima yake ya kisiasa ndani ya Chadema, baada ya chama hicho kutishia kumfukuza.
Alipoulizwa na wazee ni chama kipi atagombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu ujao, alisema wakati ukifika atasema kwani kwa sasa bado anatimiza wajibu wake wa kutetea wapiga kura wake ambao wengi
wao ni wakulima na wafugaji na yuko tayari kufukuzwa ndani ya Chadema kwa kuwatetea wao.
Alisema kuwa aliingia katika chama hicho kwa hiari yake baada ya kukataa dhuluma alizodai kufanyiwa na CCM na kudhani ndani ya Chadema kuna demokrasia na ukombozi wa kweli, lakini alichokikuta ni tofauti kwani kila siku amekuwa akipata misukosuko kutoka ndani ya chama hicho.
"Mie niliingia Chadema kwa hiari yangu baada ya kuona dhuluma zilizokuwa ndani ya CCM, chama kilichonilea kisiasa, nikaona heri
niende Chadema ambako nilidhani kuna demokrasia na ukombozi wa kweli, lakini nilichokikuta humo ni tofauti kwani kila siku wazee wangu
mnasikia napata misukosuko isiyo na maana," alisema.
Alisema pamoja na misukosuko hiyo, amekuwa kimya muda mrefu kiasi kwamba kuna wakati vijana ndani ya chama hicho walimtukana matusi, wakatoa maneno mbalimbali ya kumdhalilisha kwa kumwita ‘Msaliti’ na ‘Pandikizi wa CCM’, huku viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho, wakikaa kimya bila kuchukua hatua.
"Pamoja na shutuma zote zinazotolewa juu yangu na kupachikwa majina mbalimbali kuwa mie ni ‘Msaliti’ mara ni ‘Pandikizi la CCM’, lakini hata siku moja sijawahi kuitwa katika Kamati Kuu ya Chadema na kuhojiwa.
“Nimekuwa nikitukanwa hadharani na vijana wa Chadema mbele ya viongozi wa juu wa chama,  hawachukui hatua… mie mtu mzima hapo natafsiri kuwa wametumwa na viongozi hao ili kunifanyia fitna hizo," alisema.
Akizungumzia tuhuma zilizotolewa juu yake za kukiuka msimamo wa kutohudhuria vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, uliowekwa kwa wajumbe wa Bunge hilo kutoka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alisema tuhuma hizo hazina msingi wowote kwani hajahudhuria kikao hicho wala hakuchukua posho.
Alisema alifika mjini Dodoma akitokea Dar es Salaam akiwa njiani kwenda katika Jimbo lake la Maswa Magharibi na alipita bungeni  kufuatilia fedha za matibabu kutokana na kusumbuliwa na mguu.
Akiwa bungeni Shibuda alisema alijaza fomu za matibabu kwa kuwa wabunge wanatibiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Bunge kwa kipindi chote cha uhai wa ubunge wao.
"Mie ni kweli nilipita Dodoma nikitokea Dar es Salaam kuja huku jimboni na nilifika Ofisi za Bunge ili nipatiwe fedha za matibabu kwani nasumbuliwa na mguu na siye tunatibiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Bunge kwa kipindi chote cha ubunge sasa kosa langu la kuitwa msaliti hapa ni lipi?
“Hata hiyo posho wanayodai nimeichukua iko wapi? Labda wameweka katika akaunti ila mie nasisitiza sijachukua posho wala kuhudhuria kikao hicho," alisema.
Alisisitiza kuwa tangu habari hizo zianze kuandikwa na kutangazwa katika vyombo vya habari, hajawahi kuulizwa na kiongozi yeyote wa Chadema, isipokuwa amesikitishwa na kauli ya Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, kutishia kumfukuza ndani ya chama kwa usaliti.
"Uongozi ni kutanguliza hekima na busara katika kufikia uamuzi, uongozi si Magereza na hata Magereza wafungwa wana haki zao, Tundu Lissu amekuwa nani katika nchi hii… anaongea kama kasuku hafanyi utafiti anakurupuka na kuongea na kutoa matamko? Mie nitamtaka athibitishe tuhuma hizo anazozitoa dhidi yangu. Nasema Chadema si baba wala mama yangu," alisema.
Alisisitiza kuwa amechoka kusikia hukumu dhidi yake kila siku kupitia vyombo vya habari kutoka kwa viongozi wake wa Chadema, huku akitoa mfano kuwa alipounga mkono nyongeza ya posho ya Bunge,  aliitwa ‘Msaliti’, lakini leo wabunge wote wakiwemo wa Chadema waliogomea wanachukua posho hiyo.
"Wazee wangu niliposema bungeni posho iongezwe, niliitwa mie ‘Msaliti’ na wabunge wa Chadema lakini leo kila mmoja muulizeni hata huyu Kasulumbayi (Sylvester, Mbunge wa Maswa Mashariki, Chadema), ambaye tunaye hapa kwenye kikao kama hachukui posho hizo.
“Hata huyo Tundu Lissu anayeongea sana anachukua, hata Mbowe (Freeman, Mwenyekiti wa Chadema) alikataa gari la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, lile la Serikali lakini hadi leo analitumia… mbona yeye haitwi ‘Msaliti’?” Alihoji Shibuda.
Akizungumzia uhusika wake katika kundi la Ukawa, Shibuda alisema kuwa yeye si sehemu ya kundi hilo na wala hajawahi kuelimishwa kuhusu kundi hilo, bali anakumbuka kuwa kupitia viongozi wa juu wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR –Mageuzi, walikubaliana katika kikao kuwa wabunge wa vyama hivyo watoke bungeni na wasishiriki vikao hivyo.
"Muislamu hawezi kutetea Uislamu kama hajui nguzo saba za Uislamu na pia huwezi kuwa Shekhe bila kupitia Madrasa na hata katika Ukristo,
huwezi kuutetea Ukristo kama hujui Biblia na hukusoma mafundisho… na mie siwezi kuwa Ukawa wakati sijaelimishwa kuhusu kundi hilo,” alisema.
Lissu alipopigiwa simu na gazeti hili ili atoe ufafanuzi, alisema taarifa kwamba Shibuda amepokea posho katika Bunge Maalum la Katiba, alizipata kwa waandishi wa habari.
Alipoulizwa kama alijaribu kuthibitisha taarifa hizo, alisema taarifa hizo zimeelezwa kwa waandishi wa habari na Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis Hamad.
Lissu alisisitiza kwamba Shibuda alisaini posho mara moja, na ndio maana Katibu wa Bunge hilo, aliwaambia waandishi wa habari na yeye kupata taarifa hizo kupitia magazeti.
Kuhusu Shibuda kutogombea Ubunge kupitia Chadema, alisema  angemshangaa kama asingetoa ujumbe huo, kwani amekuwa akienda kinyume na msimamo wa wenziwe tangu siku ya kwanza ya kuanza kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Shibuda kwenda kinyume na wenzake hajaanza leo, ameanza siku ya kwanza tu wakati Rais Jakaya Kikwete alipozindua Bunge na hajabadilika, kwa hiyo kutamka msimamo wake ni sawasawa tu,” alisema Lissu.
Alisema Shibuda anajua mambo yake bungeni hivyo wangeshangaa kama bado angekuwa na nia ya kugombea nafasi yoyote kupitia chama hicho.

No comments: