ASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA ZA KUMLAWITI MTOTO WA MKEWE

Mkazi wa eneo la Majengo Mjini Manyoni, Juma Saidi (32) anashikiliwa na Polisi akituhumiwa kumlawiti mtoto wa mkewe.
Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 14, anasoma Kidato cha Kwanza katika  shule moja ya sekondari wilayani Manyoni na inadaiwa alifanyiwa kitendo hicho juzi saa 6 usiku nyumbani kwao.
Inadaiwa baba huyo wa kambo wa mtoto huyo ambaye jina na shule anakosoma vimehifadhiwa, alifanya kitendo hicho baada ya mkewe kusafiri.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela alidai mwanamume huyo alimlawiti kwa nguvu kijana huyo na kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri.
Katika hatua nyingine, polisi mkoani mkoani hapa inashikilia watu wengine watatu kwa tuhuma ya mauaji. 
Kamanda alitaja watuhumiwa hao kuwa ni Mlani Janila (55), Nchinja Ngaja (69) na Jagali Nchinja (37); wote wakazi wa Kijiji cha Mtavira wilayani Ikungi, mkoani hapa.
Wanadaiwa  Agosti 9 mwaka huu saa 1.00 jioni katika kitongoji cha Muguaghana, kijiji cha Mtavira, walimuua mwanakijiji mwenzao, Kwisu Funuki (30).
Inadaiwa siku ya tukio, Kwisu alionekana akinywa pombe ya kienyeji nyumbani kwa mtuhumiwa wa kwanza Mlani Janila.
Wakati akiendelea kunywa pombe, inadaiwa ulizuka ugomvi kati ya Funuki (marehemu) na Nchinja (mtuhumiwa) ambao uliamuliwa.
Hata hivyo, baada ya muda, Funuki aliokotwa na wasamaria wema akiwa amekufa karibu na nyumbani kwake huku pembeni kwake kukiwa na kopo la kunywea pombe ya kienyeji ijulikanayo kwa jina la “mtukuru".
Uchunguzi wa awali kwa mujibu wa kamanda, unaonesha alichomwa kifuani na kitu chenye ncha kali. Hivyo watu watatu aliokuwa akinywa nao pombe wanashikiliwa kwa uchunguzi.

No comments: