WATU 19 TAABANI KWA KUFUTURU SAMAKI WENYE SUMU

Watu 19 wa familia moja wakazi wa shehia ya Sizini, Tumbe wilaya ya Micheweni, wamelazwa katika hospitali ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba baada ya kula samaki aina ya Pono na Puju wanaodhaniwa kuwa na sumu na kusababisha kupata ugonjwa na kuharisha na kusumbuliwa na matumbo.
Tukio hilo limetokea juzi  majira ya saa 12:30 jioni katika Shehia ya Sizini baada ya watu hao wa familia mmoja kula samaki hao wakati wa futari na kusababisha  hali zao kuanza kubadilika.
Baadhi ya ndugu wa jamaa waliolazwa hospitalini wamesema kuwa hali za ndugu zao zilianza kubadilika usiku majira ya saa saba na hivyo kuwakimbiza hospitalini.
“Huyu samaki hakuvuliwa na watu waliomla, lakini alitoka sehemu nyingine kama ni zawadi, na bahati mbaya baadhi ya watu waliokula walianza kupata matatizo,” alieleza Ali Abdallah Hamad mkazi wa Micheweni.
Daktari wa hospitali ya Micheweni Pemba ambaye hakutaka jina lake kutajwa katika vyombo vya habari alikiri watu hao kula samaki wenye aina fulani ya sumu ambayo bado haijafahamika.
“Kwa sasa siwezi kuzungumza lolote, muda ukifika nitazungumza nanyi, lakini sio muda huu,” alisikika daktari dhamana wa hospitali hiyo akiwaambia waandishi wa habari.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kaskazini Pemba, Shekhani Muhammad Shekhani alithibitisha kutokea kwa tokeo hilo na kusema kuwa majeruhi wanaendelea na matibabu katika hospitalini hapo.
“Tukio la watu kula samaki anayedaiwa kuwa na sumu tumelipata na kwa sasa watu 19 wamelazwa katika hospitali ya Micheweni na wanaendelea na matibabu hali zao zinaendelea vizuri,” alisema kamanda.

No comments: