WANAODAIWA KUSHAMBULIA GARI LA MAGEREZA WAPANDISHWA KIZIMBANI

Watu wawili wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la kushambulia gari la magereza kwa risasi, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni wakikabiliwa na mashitaka matatu.
Watuhumiwa hao, Peter Mushi (36) dereva na Godlisten Mongi (40) ambaye hati ya mashitaka imemtambulisha kwamba ni mhandisi, walipandishwa kizimbani jana kwa mashitaka ya kula njama, unyang’anyi wa kutumia silaha na shambulio la kudhuru mwili.
Wakili wa Serikali, Matarasa Alungo alidai mbele ya Hakimu Anipha Mwingira kwamba Julai 2 mwaka huu, maeneo ya Mikocheni karibu na Hospitali ya Regency, Kinondoni, washitakiwa walikula njama kufanya uhalifu.
Alungo alidai katika mashitaka ya pili Mushi na Mongi waliwavamia askari wa magereza WP 481 CPL Dotto na Dorin Damas na kuwapiga kwa kutumia silaha ya moto.
Katika mashitaka ya tatu, alidai watuhumiwa hao walimshambulia kwa kumpiga Dorin katika uso wake na kumsababishia maumivu mwilini.
Washitakiwa walikana mashitaka hayo na upelelezi wa shauri hilo haujakamilika. Walirudishwa rumande baada ya kushindwa masharti ya dhamana na kesi itatajwa tena Agosti 8 mwaka huu.
Wakati huohuo, watuhumiwa Mushi na Mongi wamepandishwa tena kizimbani katika mahakama hiyo, wakikabiliwa na mashitaka ya mauaji.
Mshitakiwa wa tatu katika kesi hiyo, raia wa Burundi, Maulid Nkurunziza (23) hakusomewa shitaka mahakamani hapo baada ya Wakili Musini Mussa kueleza kuwa  yupo gerezani na angefuatwa huko kusomewa shitaka lake.
Mussa alidai mbele ya Hakimu Joyce Mushi kwamba, Mei 23 mwaka huu, maeneo ya Kunduchi Silver Wilaya ya Kinondoni, washitakiwa walimuua Edwin Humphrey, dereva wa pikipiki.
Washitakiwa wawili hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka kusikiliza kesi ya mauaji. Washitakiwa walirudishwa rumande hadi Agosti 8 mwaka huu.

No comments: