VIONGOZI WOTE WA JUU CHADEMA KIGOMA WAJIENGUA

Waliokuwa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa Kigoma wamejiuzulu nyadhifa zao zote ndani ya chama hicho kwa kile wanachoeleza kukiukwa kwa misingi ya Demokrasia ndani ya chama hicho ambayo ndiyo msingi wa kuanzishwa kwake.
Akitoa tamko la viongozi hao kujiuzulu nyadhifa zao ndani ya chama hicho, Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Kigoma, Jafari Kasisiko alisema kuwa chama kimeacha msingi wake wa kutekeleza demokrasia na badala yake viongozi wachache wa chama hicho kujichukulia madaraka na kuongoza chama kibabe.
Katika mkutano huo, mwenyekiti huyo wa Chadema aliongoza na aliyekuwa Katibu wa chama hicho Mkoa Kigoma, Msafiri Wamalwa na Katibu wa Baraza la Wanawake (BAWACHA) mkoa Kigoma, Marunga Masudi na kueleza kuwa  baada ya kujitoa Chadema wanatarajiwa kujiunga na chama kipya cha ACT.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Kasisiko alidai kuwa viongozi wa juu wa chama hicho wamekuwa wakitumia ubabe katika kukiongoza chama hicho na kuzuia demokrasia kuchukua mkondo wake.
Kasisiko aliyejiunga Chadema wakati wa harakati za kuanzishwa kwa vyama vingi baada ya kujitoa CCM mwaka 1985. Alisema walipigana kuhakikisha Chadema inasimama na kuwa chama cha upinzani kinachoheshimika, lakini kwa sasa chama hicho kimeondoka kwenye misingi yake kuwa chama cha watu wengi na badala yake kuwa chama cha watu wachache ambao wanakiendesha chama hicho kama kampuni yao.
Kwa upande wa Wamalwa, alisema ameamua kujiuzulu nyadhifa zake ndani ya chama hicho kwa sababu kwa hali ya sasa, licha ya uvumilivu wa muda mrefu wamechoshwa na hatua ambazo viongozi wanakiendesha chama hicho.
Naye Marunga alisema vurugu zilizokuwa zikianzishwa na viongozi wa juu wa chama hicho ndicho kiini cha yeye kuamua kuchukua uamuzi wa kujiuzulu na kwamba hajashinikizwa kuchukua uamuzi huo.

No comments: