SABA WAPANDISHWA KORTINI KWA MADAI YA WIZI WA TANZANITE

Wafanyakazi saba wakiwemo vigogo wawili wa Kampuni ya madini ya Tanzanite One ya Mirerani, Simanjiro, mkoani Manyara wanaotuhumiwa kuiba madini yenye uzito wa kilo 40 ya Sh bilioni 10 wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo.
Wafanyakazi hao ni pamoja na vigogo wawili wa kampuni  hiyo George Kisambe (38), Mkuu wa Idara ya kamera za CCTV na Mlinzi Mkuu wa Idara ya Upelelezi na Uchunguzi wa kampuni hiyo na Mlinzi Mkuu, Jonathani Nyange (52) ambaye inadaiwa kuwa alikuwa  zamu siku ya tukio.
Wengine ni Hussein Ngobo (64), Sunday Nzogora (35), Erick Briygy ambaye ni raia wa Afrika Kusini, Rodney Ngovi (48) na Samweli Kajuma (29).
Akizungumza na mwandishi jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Deusdedit Nsimeki alisema uchunguzi wa awali na maelezo ya watuhumiwa wote yamepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mkoani humo.
Nsimeki alisema watuhumiwa wako rumande katika Mji wa Babati baada ya kuhamishiwa kutoka rumande ya Mji wa Mererani.
Kamanda alisema hata wakifikishwa mahakamani, watuhumiwa hao, uchunguzi zaidi utaendelea kujua kiini cha wizi huo na kama kuna wafanyakazi wengine wanahusika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzanite One, Douglas Swartz alipoulizwa kama kuna zawadi itatolewa kwa yeyote mwenye kujua chanzo na wizi huo na kujua madini yalipo, alisema kampuni haiwezi kufanya hivyo kwani jukumu zima la upelelezi wamelikabidhi Polisi.

No comments: