MEYA AMSHUTUMU MBUNGE KUTETEA WAMACHINGA

Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa amemtaka Mbunge wa Ilala, Musa Zungu kutafuta njia sahihi ya kuwasaidia wafanyabiashara ndogo maarufu kama wamachinga, lakini si kuwatetea waendelee kufanya biashara zao barabarani.
Aidha, amewataka viongozi kuwa wakweli kuwaeleza wafanyabiashara hao kufuata sheria na utaratibu na kuwasaidia kupata maeneo ya kufanya kazi yaliyo bora zaidi kuliko kuwatengenezea mazingira ya kuona wanachofanya ni sahihi wakati si sahihi.
"Zungu ni kaka yangu na mambo yote tunayoyafanya yanafanyika baada ya kukubaliana kwenye vikao na yeye ni mjumbe….. tunaazimia kwa pamoja mambo yote kwa hiyo ni sawa na kwenda tofauti na uamuzi tunaofanya pamoja," alisema Silaa katika mahojiano na kituo kimoja cha redio nchini.
Alisema kama lengo ni kuwasaidia wamachinga, iangaliwe njia sahihi badala ya kuwatetea kuendesha biashara zao barabarani au maeneo ya kutumiwa na waenda kwa miguu.
Zungu katika moja ya vikao vya Bunge, akichangia mjadala wa bajeti ya serikali ya mwaka 2014/2015 alisema kuna viongozi wametangaza vita dhidi ya wamachinga, mama na baba lishe kwa kupora bidhaa zao na kuvunja maeneo yao ya kazi na kulaani vitendo hivyo.
Silaa alisema katika mazungumzo ya vikao vya ndani, ilibainika kuwa machinga kutumia kati ya Sh 5,000 hadi Sh 7,000 kutoa rushwa kwa askari mgambo wasiondolewe maeneo yasiyofaa, na kwamba fedha hiyo kwa mwezi ni sawa na Sh 150,000 hadi Sh 200,000 na zinatosha kufanya biashara zao kuwa rasmi.
Alisema kwa msaada wa Benki ya TAB, wataanza kujenga masoko ya kisasa na hivyo wanataka kuongeza kasi ya ujenzi huo ili kuwatengenezea wamachinga kufanya biashara zao kwenye mazingira bora zaidi.
Silaa alitoa mfano Kariakoo eneo la kibunge la Zungu na eneo la kiutawala la Silaa na kitovu cha kibiashara cha Taifa kuwa haliwezi kuachwa bila utaratibu utakaowezesha jamii kuishi vizuri na mapato kuongezeka.

No comments: