BOMBA JIPYA LA MAJI KUTOKA RUVU CHINI MBIONI KUKAMILIKA

Ujenzi wa bomba jipya kutoka Ruvu Chini kwenda matangi yaliyoko Chuo cha Ardhi Dar es Salaam, unakaribia kukamilika.
Ujenzi wa bomba hilo lenye kipenyo cha mita 1.8 na urefu wa kilometa 56, unalenga kuongeza ufanisi wa usambazaji wa maji katika maeneo yanayohudumiwa na maji kutoka Ruvu Chini katika jijini hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam kuhusu miradi ya maji inayolenga kuimarisha huduma hiyo katika jiji hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi  wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa), Romanus Mwang’ingo alisema mradi umefikia asilimia 73 na kazi inatarajiwa kukamilika mwezi ujao.
“Mradi huu unaendelea vizuri na karibu utakamilika,” alisema Mwang’ingo.
Alisema mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya Sinohydro ya China, utagharimu Sh bilioni 120.2 kutoka Serikali ya Tanzania.
Kwa mujibu wa Mwang’ingo, kumalizika kwa mradi huo kutaleta faida kubwa hasa ikizingatiwa kuwa tayari upanuzi  wa Ruvu Chini ulikamilika na kukabidhiwa tangu Februari 2014.
Mradi huo wa upanuzi wa Ruvu Chini uligharimu Sh bilioni 60.35 kutoka Serikali ya Marekani kupitia shirika lake la Changamoto za Milenia (MCC).
“Kazi iliyofanyika ni kuongeza uwezo wa mtambo kutoka lita 180 kwa siku na kufikia lita millioni 270 kwa siku,” alisema na kuongeza kuwa bomba jipya kutoka Ruvu Chini hadi katika tangi hizo za kuhifadhi maji litasaidia kusafirisha ziada ya maji inayosukumwa.
Alisema tatizo la maji katika maeneo ya Makongo, Changanyikeni, Goba, Kimara, Mbezi, Kibamba na maeneo yenye mabomba maarufu kama ‘mabomba ya mchina’ kuwa ni uhaba wa maji kutoka mfumo wa Ruvu Juu. Pia kutokana na hali ya miinuko ambayo inazuia maji yasifike maeneo ya mbali.
Hata hivyo alisema hivi sasa mshauri mwelekezi kampuni ya WAPCOS ya India inafanya mapitio ya mfumo wa mabomba ili kuhakikisha maji yanafika maeneo yote, kwa kuweka vituo vya kuongeza msukumo na matangi makubwa ya ugawaji.
Wiki iliyopita Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla alifanya ziara katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam kukagua miradi ya maji inayoendelea kwa kasi.

No comments: