AUA MTOTO WA TAJIRI YAKE NA KULA UBONGO

Simanzi na vilio vilitawala jana katika Kijiji cha Samanga, Kata ya Marangu Mashariki wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, baada ya mtu mmoja kumuua kwa kumcharanga mapanga mtoto wa bosi wake ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya Marangu Hills Academy, Francis Fortunatus (9) na kisha muuaji kula ubongo wa mtoto huyo.
Kama hiyo haitoshi, mtu huyo anayetajwa kuwa ni mfanyakazi katika familia ya mtoto aliyeuawa, baada ya kula ubongo alianza kujifyeka sehemu zake za siri kwa awamu, huku akila kila kipande alichokikata bila ya hofu ya damu iliyokuwa inamchuruzika kwa wingi.
Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alipozungumza na mwandishi jana.
Alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 1:20 asubuhi nje ya lango la kuingilia nyumbani kwao, wakati mwanafunzi huyo akielekea shuleni.
Kamanda Boaz alimtaja mtuhumiwa aliyefanya mauaji hayo kuwa ni Lawrence Flavian (20).
Alisema kutokana na shambulio hilo,  mtoto huyo alipoteza maisha papo hapo, ambapo mtuhumiwa naye alifariki dunia muda mchache baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Kilema, iliyopo Moshi Vijijini.
“Ni kweli nimepata hizi taarifa za mauaji ya kikatili, ni kwamba mwanafunzi  wa darasa la tatu wa shule ya Marangu Hills Academy, Francis Fortunatus (9), ameuawa na mfanyakazi wao  kwa kumcharanga kwa mapanga kichwani na kisha kula ubongo wake, pia mtuhumiwa naye amekufa baada ya kujifyeka uume wake na kuula," alisema Boaz.
Kamanda huyo wa polisi alisema chanzo cha tukio hilo imebainika kuwa mtuhumiwa alikuwa na ugonjwa wa akili, ambapo jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa kina, na miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Kilema iliyopo Marangu.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Shule ya Marangu Hills Academy, Thomas Malulu alisema kuwa mwanafunzi huyo aliuawa akiwa njiani kwenda shuleni hapo, yapata umbali wa mita 100 kutoka lilipo lango kuu la kuingilia shuleni.
Alisema baada ya kumtambua marehemu kuwa ni Francis Fortunatus walimsaka muuaji huyo na kumkuta akiwa amejificha karibu na nyumbani kwa marehemu akiwa ametapakaa damu baada ya kujifyeka sehemu zake za siri.
Baadhi ya majirani walioshuhudia tukio hilo, Pantaleo Meela na Richard Kimambo, walisema wakati tukio hilo linatokea baba mzazi wa mtoto huyo, Fortunatus Urassa alikuwa safarini akielekea mkoani Singida.
Mwandishi alimtafuta baba mzazi wa marehemu Francis, ambaye alisema mtuhumiwa alikuwa mfanyakazi wake katika kazi ya useremala, baada ya kumwajiri alipomaliza mafunzo yake...imenishtua sana kwa sababu sielewi nianzie wapi, inashangaza sana sikuwahi kujua kama alikuwa mgonjwa wa akili wala kubaini ukorofi wake kazini," alisema Urassa.

No comments: