SERIKALI YAANDAA KANUNI KUDHIBITI MATUMIZI YA MTANDAO


Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa wizara yake inatayarisha Kanuni, zitakazodhibiti matumizi mabaya ya mtandao wa intaneti, ikiwemo uwekezaaji wa picha chafu mtandaoni.
 “Serikali ipo tayari kuleta Kanuni za Online Content  na za kudhibiti picha chafu,” alisema Profesa Mbarawa, alipojibu swali la nyongeza  Mbunge wa Mkanyageni, Habib  Mnyaa (CUF). Swali la msingi liliulizwa na mbunge wa Mchinga, Said Mtanda (CCM). 
Mbarawa alisema Kanuni hiyo inatungwa na italetwa bungeni hivi karibuni ili kutoa mwongozo na  kudhibiti matumizi ya intaneti. 
Waziri huyo alisisitiza kuwa Tume ya Mawasiliano nchini (TCRA) ina mtambo na kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, wana uwezo wa kuchunguza na kubaini kiini na chanzo cha picha chafu na matumizi mengine mabaya ya intaneti. 
Katika swali lake la nyongeza, Mtanda alisema bunge lilishapitisha Sheria ya Usajili wa Simu, ambayo iliipa meno TCRA kuwa msimamizi wa mambo yote yanayohusu simu na intaneti nchini. 

Mtanda alisema TCRA wana uwezo huo, lakini wameshindwa kusimamia sheria hiyo na ndiyo maana kuna matumizi mabaya ya intaneti hivi sasa. 
Baada ya  majibu hayo ya Mbarawa, Spika wa Bunge, Anne Makinda alimhoji Waziri huyo kuwa “ Na yaliyotokea juzi, mmefanya nini?”. Papo hapo, wakasimama wabunge kadhaa akiwemo Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba (CCM), waliotaka kuuliza maswali ya nyongeza. 
Hata hivyo, Spika alisema muda uliotengwa kwa ajili ya swali hilo, ulikuwa umeisha, hivyo wabunge hao ikiwemo Komba, walilazimika kuketi chini, bila kupata fursa ya kutoa dukuduku zao. 
Katika swali lake la msingi, Mtanda alitaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali kukomesha wimbi kubwa la mmomonyoko wa maadili kupitia njia mbalimbali, hasa kupitia picha chafu katika mitandao.

No comments: