Mwanasheria Mkuu
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman, amesema
kushindwa kuanza kazi kwa Tume ya Pamoja ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
ndiyo chanzo kikubwa cha misuguano na kero za Muungano.
Othman alisema
hayo katika Baraza la Wawakilishi, wakati alipokuwa akijibu hoja mbali mbali za
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, waliokuwa wakitaka ufafanuzi wa kero za Muungano
na ufumbuzi wake, ikiwemo sababu za kutoanza kazi kwa Tume hiyo.
Akifafanua
zaidi, Othman alisema Tume huyo kwa
mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 133, ndiyo yenye
mamlaka ya kutunza fedha za Muungano wa Tanzania katika akauti maalumu.
“Fedha kwa ajili
ya shughuli za Muungano zitakuwa zikilindwa na kuhifadhiwa katika akaunti hiyo
kwa ajili ya matumizi ya mambo ya Muungano tu,” alisema Othman.
Othman ambaye
amekuwa mjumbe wa tume hiyo kwa muda mrefu sasa, alisema Sheria ya Kuundwa kwa
Tume hiyo ya 1996, bado haijafanya kazi
na kutekeleza majukumu yake ya kusimamia mwenendo wa kutunza fedha.
Alisema hajui
sababu za tume hiyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kutunza akaunti ya
Muungano kwa matumizi ya taasisi za Muungano kwa mujibu wa Katiba.
Kwa mujibu wa
Othman, kama Tume hiyo ingekuwa ikifanya kazi zake za kutunza akaunti ya fedha
za Muungano vizuri, kero za Muungano zinazojitokeza sasa zingekuwa historia.
“Chokochoko
zinazotolewa katika Muungano ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za Muungano
katika upande mwengine, zingeondoka kama akaunti hii ingekuwa ikifanya kazi
zake vizuri,” alisema.
Baadhi ya mambo
yaliyomo katika orodha ya Muungano ni mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa,
ulinzi pamoja na mambo ya ndani.
Hivi karibuni
akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa mwaka
wa fedha 2014-2015, Balozi Seif Ali
Iddi, alisema miongoni mwa kero za Muungano ambazo hazijapatiwa ufumbuzi hadi sasa
ni kuanza kazi Tume hiyo.
Suala la
kushindwa kufanya kazi kwa tume hiyo liliibuka katika Bunge Maalumu la Katiba,
katika kikao chake kilichofanyika Dodoma miezi miwili iliyopita na kuibua
mjadala mkubwa.
No comments:
Post a Comment